Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Balozi mteule wa TZ nchini Kenya

 Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi John Michael Haule akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake kujitambulisha na kuaga rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Kidiplomasia.
Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi John Michael Haule akibadilishana mawazo na Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba uendelezaji wa Sekta ya Biashara kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamuhuri ya Watu wa Kenya chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki utafungua njia ya kuimarisha ustawi wa Wananchi wa pande hizo mbili.

Alisema Kenya na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu wa Kihistoria licha ya changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza katika baadhi ya wakati ambazo uwezo wa kuzitatua upo kwa kushirikisha mazungumzo ya pamoja baina ya Viongozi wa Nchi hizo mbili.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Kenya Balozi John Michael Haule aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha sambamba na kuaga rasmi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi John Michael kusimamia vyema uhusiano huo wa Kenya na Tanzania katika kuangalia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Utalii inayoonekana kushika kasi hivi sasa katika uchumi wa Mataifa mengi Duniani kwa.


Alisema kutokana na kuimarika vyema kwa miundombinu kwenye  Sekta ya Utalii hapa Zanzibar Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Kenya inastahiki kuandaa utaratibu maalum wa kuitangaza Zanzibar ili kuhamasisha wawekezaji wa Kenya kuanzisha Miradi yao ya kiuchumi.

Balozi Seif alifahamisha kwamba uhamasishaji huo pia ungefanywa katika kuwashawishi hata  wageni na watalii wanaoingia Nchini Kenya kutenga muda wao wa kuitembelea Zanzibar ili kujionea miundo mbinu na rasilmali za utalii zinazopatikana  Zanzibar.

Mapema Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi John Michael Haule alimueleza Balozi Seif kwamba Ofisi ya Ubalozi huo itajipanga kutoa huduma muda wote wa wiki kwa wageni na watalii watakaokuwa tayari kutaka kuitembelea Tanzania.

Balozi John alisema maafisa wa Ubalozi huo watakutana na watembezaji utalii Nchini Kenya kwa lengo la kuwaeleza nia ya Tanzania katika kutoa huduma za viza hata siku za mapumziko wakati inapobidi.

Balozi Mteule huyo wa Tanzania Nchini Kenya alimuhakikishia Balozi Seif kwamba atasimamia kwa nguvu zake  uwamuzi wa wawekezaji wa Kenya watakaoonyesha nia ya kutaka kuwekeza Vitega uchumi vyao katika Visiwa vya  Zanzibar.

Alifahamisha kwamba vielelezo alivyovipata wakati wa mazungumzo yake na Viongozi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA }  vitamrahisishia kazi yake kuifanya kwa ufanisi katika kuzitangaza fursa za Utalii zilizopo Visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.