STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 10 Juni, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nchi za magharibi zimetakiwa kufanya jitihada zaidi kuhamasisha ukuaji wa viwanda katika bara la Afrika ili kuzalisha bidhaa zinazovutia masoko ya dunia badala ya kusafirisha malighali toka Afrika kwenda katika nchi hizo.
Wito huo umetolewa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Chama cha Wafanyabishara wa Ujerumani Wanaofanya Biashara Afrika uliofanyika mjini Berlin nchini Ujerumani.
“Ni lazima tuangalie mbali zaidi badala ya kusafirisha malighafi kutoka Afrika na kupeleka Ulaya na Marekani. Watafiti wa nchi zetu wasaidiwe kuhamasisha na kuongeza thamani ya bidhaa kwa masoko ya Ulaya na dunia”alisema.
Dk.Shein alisema wafanyabiashara na wenye viwanda wa nchi za magharibi ikiwemo Ujerumani hawana budi kutumia fursa ya mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji Zanzibar kuleta vitega uchumi vyao barani Afrika.
“uchumi wa Tanzania mwaka jana ulikuwa kwa asilimia 7 huko Zanzibar ukikuwa kwa kiwango hicho hicho ambapo kwa ujumla ukuaji wa uchumi kwa bara la Afrika kwa takwimu za mwaka 2012 ni asilimia 5.3”Dk. Shein alifafanua.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaalika wafanyanbiasha hao kuwekeza Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kuwaeleza kuwa mbali ya kuwepo mazingira mazuri ya uwekezaji lakini pia fursa za uwekezaji ni nyingi zisizo na ukomo.
“Zanzibar ina fursa nyingi za uwekezaji miongoni mwao ni sekta ya utalii ambayo tunawakaribisha wawekezaji kutoka Ujerumani kuja kuwekeza” alieleza Dk. Shein na kuzitaja baadhi ya sekta nyingie kuwa ni uvuvi wa bahari kuu pamoja na michezo ya baharini.
Aliongeza kuwa ni jambo la kufurahisha kuona baadhi ya wawekezaji kutoka nchini Ujerumani wameshaanza kuwekeza katika sekta ya utalii na sekta nyingine.
“hadi sasa wawekezaji kutoka Ujerumani wamewekeza kiasi cha dola milioni 72 katika miradi 21, miongoni mwao asilimia 55 ni katika utalii na asilimia iliyobaki ni uwekezaji katika majengo” Dk Shein alibainisha.
Kuhusu ukuaji wa sekta ya utalii Zanzibar, Dk. Shein aliwaeleza washiriki wa mkutano huo wakiwemo mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchi zao nchini Ujerumani kuwa idadi ya watalii imeongezeka hadi kufikia 311,891mwishoni mwa mwaka 2014 kutoka watalii 181,301 mwaka 2013 ikiwa ni ongezeko la asilimia 72.
“Zanzibar inajivunia amani na utulivu hivyo wageni wana uhakika wa usalama wao na utulivu wao wakati wote wawapo nchini” Dk. Shein aliongeza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara wa Ujerumani kuongeza juhudi kuinua biashara na nchi za Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa jumla.
“hadi sasa kiwango cha biashara kati ya Ujerumani na Afrika ni asilimia 2 tu ya biashara ya nje ya Ujerumani. Afrika tunahitaji biashara zaidi kuliko misaada”alieleza Dk. Shein na kuwahakikishia kuwa nchi za Afrika ziko tayari kufanya biashara na nchi hiyo.
Alikipongeza Chama cha Wafanyabiashara cha nchi hiyo kwa kuandaa mkutano huo kila mwaka na kwamba hiyo ndio njia nzuri ya kuhimiza biashara na uwekezaji kati ya nchi hiyo na Afrika.
Dk Shein aliwahakikishia wafanyabishara na wenye viwanda wa nchi hiyo kuwa nchi za Afrika zimedhamiria kuimarisha amani na utulivu hata hivyo alibainisha kuwa pale ambapo uwekezaji umesaidia kuinua uchumi wa nchi na kuongeza uwezo wa serikali kutoa huduma kwa wananchi wake utulivu huimarika zaidi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimaliza ziara yake ya siku nane nchini Ujerumani jana na kuondoka nchini humo kurejea nyumbani.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment