Habari za Punde

Dk Shein: mafanikio ya zao la karafuu yanadhihirisha dhamira yetu ya kuliimarisha zao hilo

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                            29 Agosti, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa ongezeko kubwa la mapato ya wakulima wa karafuu katika kipindi cha miaka minne iliyopita ni uthibitisho wa dhamira ya kweli na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Saba kuimarisha zao hilo.  

Alibainisha kuwa katika kipindi hicho,wakulima wa karafuu nchini wamejipatia jumla ya shilingi bilioni 231.2 kutoka shilingi bilioni 42.6 miaka mitano kabla ya hapo ikiwa ni ongezeko la asilimia 359.4.

Akizindua Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu nchini jana huko katika viwanja vya Kiwanda cha Makonyo kilichoko Wawi chake-Chake, Pemba, Dk. Shein aliwapongeza na kuwashukuru wale wote walioshiriki katika kutekeleza programu mbalimbali na mipango ya serikali ya kuimarisha zao hilo hadi kufikia kiwango kilicho sasa.

“kazi ya karafuu si ya mtu mmoja bali ni ya ushirikiano na washirika wengi wakiwemo wakulima, Wizara ya Kilimo na Maliasili, Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) pamoja na wafanyabishara wa ndani na nje” alieleza Dk. Shein.

Alifafanua kuwa Serikali iliona haja ya kuwepo ushirikiano uliojengwa katika ukweli na kuaminiana kutoka kila upande serikalini, wakulima na wafanyabiashara ili kujenga mazingira mazuri ya biashara na hilo ndilo lililofanyika na kupelekea mafanikio haya makubwa yanayoonekana hivi sasa.


“Tulitaka tushirikiane na wafanyabiashara na leo tunao hapa, tulipambana na magendo kwa kutoa bei nzuri na leo mafanikio tumeleezwa hapa;hayo yote ni matokeo ya ushirikiano” Dk. Shein aliieleza hadhara hiyo iliyojumuisha pia wanunuzi wakubwa wa karafuu wa nje ya nchi na ndani.

Katika mnasaba huo alitoa pongeza maalum kwa uongozi wa ZSTC kwa kutekeleza kwa uhodari na kwa umakini mkubwa mpango wa mageuzi wa shirikia hilo ambapo matokeo yake shirika hilo sasa linajiendesha kwa faida na kuwa na uwezo wa kulipa kodi za serikali.

Kwa hivyo alisema uzinduzi wa mfuko huo ni hatua nyingine muhimu ya kuendeleza zao hilo na kuzifanya jitihada za serikali ya kuimarisha zao la karafuu kuwa endelevu na lenye kuleta tija kwa washiriki wote hususan wakulima.

“wakulima sasa wana matumaini makubwa na Mfuko huo kwa kuamini kuwa ni chombo muhimu katika kuendeleza zao hilo hivyo ni lazima kuzingatia masharti ya uendeshaji wa Mfuko kwa maslahi ya wote”Dk. Shein alisisitiza.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuhimiza suala la utafiti katika kila kipengele cha biashara ya zao la karafuu badala ya kujiekeleza tu katika masuala ya sheria na taratibu zilizowekwa huku akisisitiza suala la kuongeza thamani ya zao hilo na uzingatiaji viwango ili kulinda ubora wa zao hilo.

“Tukifanikiwa kuuza bidhaa ambazo zinatokana na karafuu, tutapata faida kubwa zaidi kuliko kuendelea kuuza zao hilo kama lilivyo ambapo wenzetu tunaowauzia wanalitumia kama malighali” Dk. Shein alieleza.

Akijibu ombi la Mheshimiwa Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui kuhusu kucheleweshwa kwa kupitishwa Muundo Mpya wa Utumishi na Mishahara ya Watumishi wa ZSTC, Dk. Shein alisema suala hilo analifahamu na linashughulikiwa na mamlaka zinazohusika.

Awali akizungumza kumkaribisha Mheshimiwa Rais, Waziri Mazrui pamoja kumpongeza Mheshimiwa Rais alimuomba aingilie kati ucheleweshwaji wa suala hilo ambalo limekuwa serikalini tangu mwezi Agosti mwaka 2013.

Katika maelezo yake, Waziri alieleza kuwa kuzinduliwa kwa Mfuko huo ni muendelezo wa maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa kwa wizara hiyo mwaka 2011 kuhusu uimarishaji wa zao la karafuu.

Alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake binafsi katika kuimarisha zao hilo juhudi ambazo zimerejesha hadhi ya zao hilo na kuonesha thamani ya mkulima wa karafuu nchini.

Aliuelezea kuwa mfuko huo ni moja ya nyenzo za kuimarisha zao la karafuu na kuwa wananchi wa Zanzibar wana kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kurejesha hadhi ya karafuu katika uchumi wa Zanzibar.

“Ni historia  kwa nchi yetu shirika sasa limesimama lenyewe. ZSTC tunayoicha leo iko vizuri na tuna kila sababu ya kuamini kuwa itaendelea kuimarika na kufanya vizuri zaidi ” alieleza Waziri Mazrui.

Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Rais alitoa vyeti maalum kwa wakulima bora na wauzaji bora wa karafuu. Alikabidhi hundi ya shilingi milioni 60 kwa Shirika la Bima la Zanzibar ikiwa ni kinga ya bima kwa wakulima wa karafuu watakaopata ajali wakati wa kuchuma zao hilo. 

Mapema akitoa maelezo ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bibi Mwanahija Almasi Ali alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana  katika biashara ya zao la karafuu ikiwa ni matokeo ya jitihada za makusudi za uongozi wa serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.
Dk. Shein alimaliza ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba hiyo jana ambako alizindua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuweka jiwe la msingi la hospitali ya Abdalla Mzee inayojengwa upya huko Mkoani Pemba.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.