Habari za Punde

Mgombea urais kupitia UKAWA Lowassa ataja vipaumbele kuelekea uchaguzi mkuu



Na: Hassan Hamad, OMKR.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mhe. Edward Lowassa amezitaja sekta za elimu, afya na kilimo kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vyake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Amesma sekta hizo ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi ambapo amesema sekta ya kilimo itasaidia kuongeza ajira kwa vijana wanaokabiliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu sasa.

Mhe. Lowassa ametaja vipaumbele hivyo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa Kampeni za Chama hicho unaovijumuisha pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Kuhusu sekta ya afya amesema iwapo atachaguliwa kuongoza nchi anaimarisha huduma za afya ili kuhakikisha kuwa hospitali zote nchini zinapatiwa vitendelea kazi vya kutosha yakiwemo madawa, sambamba na kuimarisha huduma za akina mama na watoto.

Vipaumbele vyengine ambavyo ni sehemu ya Ilani ya uchaguzi ya Chadema amesema ni miundombinu na mawasiliano ambapo amewambia wafuasi wa UKAWA na wananchi kuwa ataijenga upya reli ya kati, ili kurahisisha mawasiliano katika eneo hilo.

Mapema akizindua Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA, Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe, amesema mabadiliko yanayopiganiwa na UKAWA yana lengo la kuleta maisha mapya kwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki za binadamu.

Amesema Ilani hiyo ambayo ndio dira kwa vyama vyote vinavyounda Umoja wa UKAWA, imezingatia maslahi mapana ya Watanzania katika mazingira yaliyowazunguka.

Naye Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Frederick Sumaye amasema ameamua kujiunga na kambi ya upinzani ili kusaidia harakati za mabadiliko zinazopiganiwa na UKAWA.

Amesema Tanzania bado haijawahi kushuhudia mabadiliko ya kisiasa ndani ya mfumo wa vyama vingi, na kwamba UKAWA imejipanga vyema kuongoza mabadiliko katika uchaguzi mkuu ujao.

Aidha Mhe. Sumaye amemtaja Mhe. Lowasa kuwa ni mtu makini anayeweza kuongoza harakati za mabadiliko na kiongozi anayeweza kupambana na umaskiti unaowakabili wananchi.

Kwa upande wake mgombea mwenza wa Urais kupitia CHADEMA Mhe. Juma Duni Haji, amesema Chama hicho kinapigania mabadiliko ili kuondosha uonevu dhidi ya wananchi hasa wa kipato cha chini.

Ameidha ameahidi kutunza heshima za akina mama kwa kuimarisha huduma zao katika hospitali, ili kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua ambavyo vimekuwa vikiathiri maendeleo na ustawi wa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.