MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amezitaka mamlaka zinazosimamia kodi nchini, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), kuhakikisha mfumo wa kodi ni wa haki, uwazi na rahisi.
Ameyaeleza hayo katika ukumbi wa hoteli ya Verde, alipokuwa akizungumza kweye ufunguzi wa kongamano kodi na uwekezaji lililoandaliwa na wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango.
Mhe. Hemed amesema mamlaka hizo zina wajibu wa kuhakikisha mifumo ya kodi inakuwa ya kueleweka na yenye kuzingatia mazingira halisi ya biashara na uwekezaji, hatua itakayowezesha walipa kodi wanatekeleza wajibu wao kwa hiyari.
Sambamba na hayo, Mhe. Hemed ameziagiza mamlaka hizo kuwajenga uwezo watendaji wake kwa kuwaongezea ujuzi, jambo ambalo litaharakisha kufikiwa kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alibainisha kuwa kodi ni chanzo kikuu cha mapato ya serikali, ambapo kupitia mapato hayo serikali inatekeleza majukumu ya msingi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, utoaji wa huduma za afya, elimu na kuhakikisha amani na usalama kwa wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais, amesema kuwa serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka sera thabiti, sheria rafiki kwa wawekezaji sambamba na kuimarisha mazingira ya biashara.
Akifafanua zaidi kuhusu kustawisha mazingira ya biashara hapa nchini, Mhe. Hemed amesema serikali itaimarisha mfumo wa kodi usiokuwa na changamoto ambao utasaidia kukua kwa sekta hiyo na hatimaye kuongeza mchango wake katika maendeleo ya nchi.
Mhe. Hemed amesema serikali itaendelea kufanyia marekebisho maeneo ambayo yanaleta ukakasi katika mashirika ya umma na sekta binafsi, hatua ambayo itawezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyabiashara na wawekezaji kuendelea kutii na kutekeleza sera na sheria za kodi, hatua ambayo itawaepushia usumbufu usio wa lazima unaoweza kujitokeza.
Makamu huyo amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani ya Zanzibar hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo kwa upande wa serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha amani iliyopo inadumu.
Kwa upande wake, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema kongamno hilo limewashirikisha wadau wa kodi nchini na wawekezaji, ambapo watapata fursa ya kujadili namna watakavyoimarisha sera, sheria za kodi na uwekezaji ili kuepusha mkizano wa kifikra na kiutendaji.
Dk. Mkuya alifahamisha kuwa serikali inaendelea kufanya mageuzi ya sera na sheria kwa kuweka miundombinu imara na rafiki kwa walipa kodi na wawekezaji, ambayo itasaidia katika kuimatisha uchumi kupitia kodi zinazokusanywa hapa nchini.
Waziri Mkuya aliahidi kuwa maoni na mapendekezo yatakayotolewa katika kongamano hilo yatafanyiwa kazi hasa katika kuifanyia marekebisho bajeti ya ya mwaka 2025/2026.
Kingamano hilo la kodi na Uwekezaji limeandaliwa na Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango lenye lengo la kuchochea mabadiliko ya kiuchumi ndani na nje ya nchi, ambapo masuala ya kodi yamekuwa ni sehemu muhimu ya mabadiliko hayo.
Kwa upande wake Mwenyeki wa Jumuiya ya wafanyabishara Zanzibar ndugu Ali Amour amesema wanatambua umuhimu wa kodi katika kujenga uchumi wa nchi ambapo ameziomba mamlaka husika kuhakikisha wanapunguza mlolongo wa ulipaji wa kodi kwa wafanyakazi na wawekezaji na kuwepo kwa eneo moja ambalo litamaliza taratibu zote za ulipaji wa kodi na kutoa unafuu na usalama kwa walipa kodi na wawekezaji.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Zanzibar Women Chamber of Commerce bibi Najma Hussein amesema washiriki wa kongamano hilo watajadili fursa na changamoto katika masuala ya kodi jambo ambalo litasaidia kutoa mwamko wa wadau wa kodi kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kupelekea kunyanyuka uchumi wa nchi.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 09 Juni , 2025.
No comments:
Post a Comment