MABORESHO YA MIFUMO YA KODI.
Dkt. Nchemba alisema Serikali inalenga kufanya maboresho
ya mfumo wa kodi, ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo
na ada zinazotozwa chini ya sheria mbalimbali pamoja na
kuboresha taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya
Serikali ili kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa
kutabirika unaolenga kuchochea shughuli mbalimbali za
uzalishaji mali ndani ya nchi.
Mapendekezo ya kurekebisha mfumo wa kodi kwa mwaka
2025/26 yanatarajiwa kuiongezea Serikali jumla ya shilingi
milioni 4,260,023.77 ambapo baadhi ya mapendekezo hayo ni
kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye viuatilifu
vinavyotambulika kwa HS Codes 3808.61.00, 3808.62.00 na
3808.69.00, ili kuwapa unafuu wakulima ya kupata dawa za
kuua wadudu mashambani na hivyo kuongeza uzalishaji wa
mazao nchini.
Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye miamala ya
ununuzi wa bima mtawanyo inayofanywa baina ya kampuni
za bima na zile za bima mtawanyo ili kuongeza ushindani wa
kampuni za ndani, kukuza Sekta ya Bima na kuhamasisha
matumizi ya bima katika kukabiliana na majanga nchini.
Kutoza kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha asilimia
0 kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa kutumia
pamba inayolimwa nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja ili
kuleta unafuu kwa wakulima wa pamba na viwanda
vinavyotengeneza nguo nchini.
Kutoza kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha asilimia
0 kwenye mbolea inayozalishwa ndani ya nchi kwa kipindi cha
miaka mitatu ili kuleta unafuu kwa wakulima na walaji hasa
katika kipindi hiki ambacho dunia imetoka kwenye mdororo
wa kiuchumi duniani.
Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye mafuta ya
kula yanayozalishwa ndani ya nchi kwa kutumia mbegu
zinazozalishwa nchini kwa muda wa mwaka mmoja ili
kuendelea kuleta unafuu wa bei ya mafuta ya kula nchini.
Kufuta Msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani unaotolewa
kwenye ununuaji na uingizaji wa gaming supply. Hatua hii
inalenga kuleta usawa katika utozaji wa kodi kwa kuwa
michezo mingine kama vile mpira wa miguu ipo katika wigo
wa utozaji wa kodi ya ongezeko la thamani. Hatua hii
inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 322,022.5.
Kuweka sharti la msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani
kwenye matairi ya trekta yanayotumika kwenye shughuli za
kilimo yanayotambulika kwa HS Code 4011.70.00; dam liners
zinazotambulika kwa Heading 39.20; forks (HS Code
8201.90.00); reki (HS Code 8201.30.00); na shoka (HS Code
8201.40.00) kutolewa baada ya kupata ridhaa ya Waziri
mwenye dhamana ya masuala ya kilimo.
Kufuta msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye
lami zinazotambulika kwa HS Code 2713.20.00 na 2715.00.00
ili kuendana na azma ya Serikali ya kupunguza misamaha
isiyo na tija ili kulinda mapato ya Serikali na kupunguza
matumizi yanayohusiana na utoaji wa misamaha ya kodi.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi
cha shilingi milioni 85,606.2.
Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye magazeti
yanayozalishwa nchini pekee ili kupunguza gharama za
magazeti hayo na hivyo kuwezesha upatikanaji wa taarifa
muhimu. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni 1,274.4.
Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye gesi asilia
inayouzwa kwenda kwenye vituo vya kushindilia gesi kwa ajili
ya matumizi ya magari ili kuweka unafuu kwa wawekezaji,
kuvutia uwekezaji wa vituo vya kusambazia gesi asilia
iliyosindikwa kwenye magari na kupunguza utegemezi wa
mafuta na uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye matanki na
mitungi ya gesi ya kupikia zinazotambulika kwa HS Code
7311.00.10 pamoja na mitambo ya kuondoa hewa ukaa yenye
HS Code 8417.80.00 inayotumika katika uzalishaji wa mikaa
mbadala. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za
upatikanaji wa bidhaa hizi ili kuhamasisha matumizi ya
nishati safi ya kupikia nchini.
Kujumuisha masoko mtandao na huduma za masoko za
kimtandao kwenye wigo wa tafsiri ya neno wakala wa huduma
za kimtandao ili kutanua wigo wa kodi kwa kuweka ufafanuzi
utakaopelekea kutatua changamoto zilizopo katika utozaji na
usimamizi wa kodi ambapo tafsiri iliyopo sasa haijumuishi
huduma hizo katika utozaji kodi. Hatua hii inatarajia
kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
116,073.4.
Kuweka unafuu wa kutoza kodi ya mapato kwa kundi la
pikipiki ya miguu miwili, pikipiki ya miguu mitatu (Bajaji) na
magari ya kubeba mizigo yenye uzito usiozidi Kilogramu 500
ikiwemo Guta kwa kuweka utaratibu mpya wa kukadiria kodi
ya mapato kwenye vyombo hivyo. Maboresho ya viwango vya
kodi elekezi yanalenga kuweka unafuu wa kodi kwa kundi
husika na hivyo kurahisisha utekelezaji wa sheria.
Kupunguza tozo ya ushuru wa huduma kutoka utaratibu wa
sasa wa kutoza kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya pato ghafi
kwenda kiwango mfuto cha asilimia 0.25 ya pato ghafi. Lengo
la hatua hii ni kupunguza gharama za ufanyaji biashara na
uwekezaji nchini pamoja na kuendana na masharti ya Mpango
wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI).
Kupunguza kiwango cha ada ya ushuru wa hoteli (hotel levy)
kutoka asilimia 10 hadi asilimia 2. Lengo la hatua hii ni
kupunguza gharama za ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.
Kufuta ada za upakiaji (loading) na upakuaji (offloading)
zinazotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazohusiana
na usafirishaji wa mizigo. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama za ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili
kuendana na masharti ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya
Biashara nchini (MKUMBI).
Kupunguza ada ya usajili wa pikipiki za biashara kutoka
shilingi 340,000 hadi shilingi 170,000 kwa miaka mitatu
ambapo ada husika italipwa wakati wa usajili wa awali pekee.
Kupunguza ada ya leseni ya uendeshaji wa pikipiki, bajaji na
guta kutoka shilingi 70,000 hadi shilingi 30,000.
KUGHARAMIA BIMA YA AFYA
Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato
ili kupunguza nakisi ya kibajeti kwa kufanya marekebisho
katika sheria mbalimbali. Aidha inapendekezwa asilimia 70 ya
mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa
Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) na asilimia 30
ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.
Marekebisho hayo ni kama ifuatavyo:
Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA
147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kilevi
vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi kama
ifuatavyo: shilingi 20 kwa bia zinazotambulika kwa Heading
22.03; shilingi 30 kwa mvinyo unaotambulika kwa Heading
22.04, 22.05, na 22.06; shilingi 50 kwa spirits na vinywaji
vingine vinavyotambulika kwa Heading 22.08.
Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa,
SURA 147 ili kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye
huduma za mawasiliano ya kielektroniki kutoka asilimia 17
hadi asilimia 17.5.
Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Barabara na
Mafuta, SURA 220 ili kutoza kiasi cha shilingi 10 kwa kila lita
ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa pamoja na
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, SURA 123 ili
kutoza kiwango cha asilimia 0.1 kwenye thamani ya soko ya
madini.
Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya
Kubahatisha, SURA 41 ili kuongeza kiwango cha kodi kwenye
zawadi ya ushindi (Winning tax) kwenye michezo ya kubashiri
matokeo (sports betting) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15;
na kwenye michezo ya kasino ya ardhini (land based casino)
kutoka asilimia 12 hadi asilimia 15.
Kutoza magari na mashine (heavy machines) zinazoingizwa
kutoka nje ya nchi kama ifuatavyo: Shilingi 50,000 kwa
magari yenye ukubwa wa injini (CC) kati ya 0 -1000; Shilingi
100,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia
1001-1500; Shilingi 150,000 kwa magari yenye ukubwa wa
injini (CC) kuanzia 1501-2500; Shilingi 200,000 kwa magari
yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia 2501 na zaidi; Shilingi
250,000 kwa mashine (Excavators, Bulldozers, Fork Lifts)
zenye Heading 84.29 na 84.27.
Kutoza shilingi 500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa
huduma za usafirishaji kwa njia ya treni na kutoza shilingi
1000 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za
usafirishaji kwa njia ya anga. Hatua hizi kwa pamoja
zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa shilingi milioni
586,404.9.
KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA
Ili kuiwezesha nchi kuwa na sera bora za biashara na kuweka
mazingira mazuri ya ufanyaji biashara baina ya wazawa na
wageni, Serikali inatarajia kufanya marekebisho kwenye
Sheria ya Utoaji wa Leseni za Biashara ikiwemo:
Kufuta kifungu cha 3(4) kinachozipa nguvu mamlaka za utoaji
wa leseni za biashara kufunga biashara pale ambapo
wafanyabiashara wamekiuka masharti ya Sheria husika.
Lengo la hatua hii ni kuwaondolea kero wafanyabiashara na
pia kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kutofunga biashara.
Kuongeza kifungu cha 8(7) ambacho kinampa mamlaka
Waziri mwenye dhamana na masuala ya biashara kuainisha
shughuli za kibiashara ambazo hazipaswi kufanywa na
wageni.
Utaratibu wa utekelezaji wa kifungu hiki utafanywa kupitia
Amri (Order) itakayotolewa na Waziri ambayo itakua na
orodha ya shughuli za kibiashara ambazo hazipaswi kufanywa
na wageni.
Dkt. Nchemba alisema bajeti hii inaendeleza na kukamilisha
utekelezaji wa miradi, Kuchochea uchumi shindani na
shirikishi, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa viwandani na
utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea
maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu ili
kuhakikisha ufikiwaji wa malengo ya Dira 2025.
No comments:
Post a Comment