Habari za Punde

Dk Shein akutana na Balozi wa Qatar nchini

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduuzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na mgeni wake Balozi wa Qatar katika Jamhuri ya Muunfano wa Tanzania Abdulla Jassim Al Maadad alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,[Picha na Ikulu.]
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduuzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na mgeni wake  Balozi wa Qatar katika Jamhuri ya Muunfano wa Tanzania Abdulla Jassim Al Maadad alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao,[Picha na Ikulu.]


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduuzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na Balozi wa Qatar katika Jamhuri ya Muunfano wa Tanzania Abdulla Jassim Al Maadad alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao,[Picha na Ikulu.]

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                      21 Septemba, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefanya mazungumzo na balozi wa Qatar Mheshimiwa Abdulla Jassim Al Maadadi na kueleza matumaini yake na ya wananchi wa Tanzania kuona uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaimarika kwa kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano.

Dk. Shein alisema Zanzibar imefurahishwa na uamuzi wa shirika la ndege la nchi hiyo-Qatar airways kuanzisha safari za moja kwa moja hadi Zanzibar na kueleza kuwa hiyo ni miongoni mwa hatua muhimu katika kukuza ushirikiano kati ya Zanzibar na nchi hiyo.

Alifafanua kuwa hatua hiyo imezidi kuiunganisha zaidi Zanzibar na nchi nyingine duniani hivyo kuimarisha biashara ya utalii nchini.

Dk. Shein alimueleza balozi huyo kuwa Zanzibar ni visiwa maarufu duniani na imekuwa ikivutia watu mashuhuri kutembelea kwa nyakati mbalimbali.  

Akizungumzia uwekezaji Dk. Shein amemueleza Balozi Maadadi kuwa Zanzibar ingependa kuona uwekezaji zaidi kutoka nchini Qatar unafanyika hapa Zanzibar katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii pamoja na sekta ya nishati.

“Tutafurahi kama Qatar itaweza kushirikiana nasi katika masuala ya mafuta na gesi. Tunaamini uzoefu wenu katika sekta hiyo utakuwa wa manufaa sana kwetu” Dk. Shein alimwambia Balozi Maadadi.


Alibainisha kuwa Zanzibar hivi sasa imo mbioni kujiandaa kuendeleza sekta ya mafuta na gesi na itahitaji ushirikiano kutoka nchi kama Qatar hasa katika kuwajengea uwezo wataalamu wake.

Alimueleza Balozi huyo kuwa sekta hiyo ya mafuta na gesi ni miongoni mwa sekta ambazo Zanzibar inakaribisha wawekezaji wakiwemo kutoka nchini Qatar ambao tayari wamekuwemo katika sekta hiyo kwa miaka mingi.

Katika mazungumzo hayo Mheshimiwa Rais alitumia fursa hiyo kuishukuru Qatar kwa misaada yake mbalimbali kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kueleza matumaini yake kuwa wananchi wa nchi mbili hizo watashuhudia manufaa zaidi kutokana na ushirikiano wa nchi zao.  
  
Kwa upande wake Balozi Abdulla Jassim Al Maadadi alimueleza Dk. Shein kuwa ana matumaini makubwa kuwa katika kipindi atakachokuwepo nchini ataweza kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi yake na Jamhuri ya Mungano wa Tanzania.

Alibainisha kuwa akiwa nchini atajitahidi kuona uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Qatar na Tanzania unapanuka kwa kuhimiza uwekezaji katika sekta mbali mbali pamoja na ushirikiano katika sekta ya utalii.

Balozi Maadadi alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa pamoja na ukweli kuwa Zanzibar ni maarufu ulimwenguni lakini bado kuna umuhimu kuitangaza zaidi Zanzibar kama kituo cha utalii ili watalii wengi zaidi hasa vijana waweze kuifahamu vyema na hatimae kutembelea kwa wingi.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.