STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 20.9.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
leo amefungua miradi miwili mikubwa ya umeme katika visiwa vya Makongwe na Kisiwa
Panza huko Pemba na kusema kuwa hizo ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya kuhakikisha huduma zote muhimu ikiwemo ya umeme zinawafikia
wananchi popote pale walipo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati
tofauti katika uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa umeme katika visiwa vya
Makongwe pamoja na Kisiwa Panza vyote viliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.
Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Wizara, Bwana Shafi Haji Mussa, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
ZECO, Mkurugenzi na wafanyakazi wote wa ZECO pamoja na wafanyakazi wote wa
Shirika hilo.
Akiwa Kisiwa Panza Dk. Shein alisema kuwa
wapo walioamini na wapo wasioamini kama umeme umefika, aliwakumbusha kuwa hiyo
ni ahadi yake aliyoitoa mwaka 2010 wakati wa Kampeni za uchaguzi Chanjani
Chokocho katika uwanja wa Black Wizard ambapo aliahidi kuufikisha umeme kisiwa
Panza na Makongwe.
Alisema kuwa shughuli hiyo imepangwa kwa
muda mrefu, umeme umezinduliwa tayari na alisema kuwa amekuwa akifuatilia hatua
kwa hatua huku akisisitiza kuwa kazi ya kuleta maendeleo imefanywa pamoja
waliokuwemo serikalini pamoja na wananchi na hakuna atakaejisifu kuwa kafanya
peke yake.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa ipo siku
barabara ya kisiwa Panza itatengezwa kwa kiwango kinachohitajika kutoka Mtondooni
hadi Panza nayo itajengwa na kuwa ya kileo hukua akisema kuwa kufikishwa umeme
Kisiwapanza ni jitihada za watu wote na matokeo yake yanaonekana hivileo.
Alisisitiza kuwa tayari huduma zote
muhimu zimeshafika katika visiwa hivyo zikiwemo huduma za umeme,maji, afya
skuli pamoja na huduma nyengine muhimu.
Alisisitiza kuwa ipo haja ya kuwepo Gati
ndogo, ili wananchi wa sehemu hiyo waweze
kusafiri bila ya usumbufu na kueleza kuwa bado ana nia ya kutafuta
utaratibu mzuri zaidi wa uvukaji vizuri ili watu wa KiswaPanza wasafiri kutoka
Chokocho hadi KisiwaPanza."....muda ukifika nitakuja kulieleza vizuri
suala hili",alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa Biashara mbali mbali
zinazotegemea umeme zitashamiri sana katika visiwa hivyo na kuwataka wananchi
hao wafanye hivyo huku akiwahakikishia huduma hiyo itabadilisha maisha yao.
Alieleza kuwa maisha ya mwanaadamu
hubadilika mara baada ya kupatikana kwa umeme na kusisitiza kuwa Serikali ina mipango mengi iliyojiwekea katika upatikanaji
wa huduma hiyo huku akiwaeleza hatua zinazoendelea za mabadiliko ya mitambo ya
umeme hivi sasa nchini kote na aliwataka wasitaharudki na hilo.
Akieleza haja ya kutunzwa kwa miundombinu
ya umeme Kisiwani humo alisema kuwa ni pamoja na kutojenga karibu na nguzo,
kutochimba mchanga chini ya nguzo hizo hata vibanda vya mazungumzo na kuwataka
kila mmoja awe mlinzi. "....itunzwe ili tuweze Kuitumia sisi, watoto wetu,
wajukuu wetu, vitukuu vyetu..", alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali imo
katika jitihada za kutafuta umeme mbadala hapa Zanzibar kwani uliopo
unanunuliwa kutoka Tanzania Bara kwa fedha nyingi na kuwataka wananchi kulipia
huduma hiyo kwa ajili ya kuepuka usumbufu hapo baadae sambamba na Serikali
kupata fedha za kuulipia.
Serikali inafanya taratibu za kutendeza
umeme kwa taka, upepo, gesi au mawimbi ya bahari na hivi sasa wataalamu wamo
katika utafiti na baada ya muda si mrefu watatoa jibu. Aidha, alisema kuwa
hatua hiyo inakuja kutokana na kukua kwa shughuli za maendeleo Unguja na Pemba
zitakazohitajia huduma zaidi za umeme.
Alisema kuwa Shirika aliliagiza aliliagiza
Shirika la Umeme na kulielekeza kuwa wale waliokuwa hawana fedha wapatiliwe umeme
na watakuwa wanalipa kidogo kidogo deni hilo na kupongeza kutokana na
kuendeleza utaratibu huo.
Akiwa katika kisiwa cha Makongwe Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kueleza kuwa matukio hayo ni ahadi alizozitoa kwa
visiwa vya Makongwe na Kisiwa Panza kufikisha umeme ndani ya miaka mitano ya
uongozi wake na kuahidi kisiwa cha Shamiani, baada ya muda si mrefu nao
watapata huduma hiyo.
Alisema kuwa umeme utawasaidia kuimarisha
shughuli zao za maendeleo zikiwemo
kilimo, ufugaji, uvuvi, kutumia mashine za kusagia, mafriji, kuwa na vyombo vya
habari vitakavyowasaidia kupata habari mbali mbali za ndani na nje ya nchi yao.
Dk. Shein alisema kuwa ahadi ya kuleta
umeme katika visiwa vidogo vidogo aliitoa Dk. Shein na kusisitiza kuwa upelekaji
umeme katika visiwa ni muendelezo wa Sera za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ya kuhakikisha kuwa huduma zote muhimu ikiwemo ya umeme inawafikia wananchi
popote pale walipo.
Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati Mhe. Ramadhani Abdalla Shaaban aliwaomba wananchi wa Kisiwa Panza
pamoja na Makoongwe kuutumia umeme huo kwa maendeleo yao kwani umeme hivi sasa
sio anasa tena bali ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya binaadamu.
Aidha, alieleza kuwa kwa kutumia umeme
mwananchi ataweza kufaidika kwa kuhifadhi vyakula, samaki, kufanya biashara
ndoondogo na pia, wnafunzi wataweza kujisomea wakayti wa usiku kwa uhakika.
Alisema kuwa Wizara yake kupitia ZECO
wameweza kukamilisha mradi wa usambaza umeme katika kisiwa hicho ambapo kazi
zilizofanyika ni ujenzi wa njia kubwa za umeme za msongo wa 33kV zenye urefu wa
km tatu ambazo zimejengwa katika upande wa Chokocho na ndani ya Kisiwa Panza.
Kazi nyengine ni uwekaji wa vituo viwili
vya transfoma kila moja yenye uwezo wa 100kVA ambazo zimewekwa Mitondooni skuli
na Panza, ujenzi wa laini ndogo za umeme zenye urefu wa kilomita nne pamoja
na ulazaji wa waya wa baharini wenye
urefu wa kilomita mbili kutoka Chokocho hadi Mitondooni.
Waziri Shaaban alisema kuwa kazi za
usambaji umeme Kisiwa Panza zimegharimu jumla ya shilingi 1,128,810, 174.00
mchango ambapo kati ya fedha hizo shilingi 604,960,764.00 zilitolewa na
Serikali Kuu na Tshilingi 523,849,410 zimetolewa na Shirika la Umeme (ZECO).
Alisema kuwa waya wa baharini
umetengenezwa nchini Ufaransa katika kiwanda kinachomilikiwa na Kampuni ya
General Cable ya nchini Norway.
Kwa upande wa kazi za ushauri Waziri Shaaban alisema kuwa kazi za
ushauri wa matengenezo ya waya wa baharini pamoja na ulazaji wake zote za
kupeleka umeme visiwani humo zimesimamiwa na wataalamu wa ZECO na hivyo kupelekea
kuokoa kiasi cha shilingi milioni 363,832,917.00 fedha ambazo zingetumika
kuwalipa wataalamu kutoka nje kwa ajili ya kutoa Ushauri na Usimamizi wa kazi
za ulazaji waya wa baharini.
Kwa upande wa Kisiwa cha Makongwe Waziri
Shaaban alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuzindua mradi mkubwa wa umeme
kisiwani humo na kusema kuwa ni fursa
kwa wananchi wa Makongwe na pia, ndoto yao ya kupata umeme sasa imekuwa ya
kweli.
Alisema kuwa kazi za usambazaji umeme katika kisiwa cha Makongwe
zimegharimu jumla ya Shilingi 855,229,452.00 ambapo kati ya fedha hizo Shilingi
milioni 604,960,764.00 zimetolewa na Serikali Kuu na Shilingi milioni 250,
268,688 zzimetolewa na Shirika la umeme
Alitoa pongezi kwa wananchi wa Makongwe
ambao mara tu kufika huduma hiyo ambapo siku ya mwanzo waliungiwa umeme
wananchi 115.
Nao wananchi wa visiwaa hhivyo walitoa
pongezi zao kwa Rais Dk. Shein pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Za nzibar
chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kuwafikishia huduma hiyo muhimu sambamba na
huduma nyengine ambazo zimeshawafikia hivi sasa zikiwemo afya, maji, elimu na
nyenginezo.
Wananchi hao walieleza kuwa neema hizo
walizozipata ni lazima wamshukuru Mwenyezi Mungu na kumshukuru na kumuombea Dua
Dk. Shein kwa kuwajali na kuwathamini na kusisitiza kuwa uongozi wake ndani ya
miaka mitano umewaletea maendeleo makaubwa.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment