Habari za Punde

UVCCM yamshangaa Sumaye kumpigia debe Lowassa


Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka amesema anamshangaa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kusaidia kampeni mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa.


Amesema uamuzi huo wa Sumaye ni sawa na pwagu kumfanyia kampeni pwaguzi. Shaka alitoa matamshi hayo jana katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za ubunge na madiwani jimbo la Mtwara Vijijini wakati akimnadi mgombea wa jimbo hilo kupitia CCM, Hawa Ghasia.



Mkutano huo wa kampeni ulifanyika katika kijiji cha Mo Pacha Nne mkoani hapa.



Alisema ni kituko kwa viongozi hao, ambao waliwahi kuwa viongozi wa juu wa serikali ya CCM na kushindwa kuleta ufanisi na matokeo chanya, sasa wakiwa Chadema kughilibu wananchi wakidai wana ubavu wa kuleta mabadiliko na maendeleo.



“Sumaye anapomfanyia kampeni Lowassa awe Rais ni sawa na pwagu kumfanyia kampeni pwaguzi, hawajui wafanyalo, hawatambui kama majina yao hayaheshimiki mbele ya jamii, walipewa nafasi za juu wakashindwa kuisukuma nchi kimaendeleo,” alisema Shaka.



Alisema Sumaye akiwa Waziri Mkuu wa Serikali chini ya awamu ya tatu ya Rais Benjamni Mkapa, usimamizi wake alisababisha halmashauri nyingi za wilaya nchini kupata hati chafu kwa mujibu wa ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.



Aidha, Shaka alifichua siri ya jina la Lowassa kukatwa na vikao vya CCM katika mbio za urais, huku akisema halikuwa jambo la bahati mbaya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.