Habari za Punde

Qatar yakusudia kuwekeza Zanzibar

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Balozi wa  Qatar Nchini Tanzania Bwana Abdulla Jassim Al – Maadad aliyefika kusalimiana nae  ofisini kwake  Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi wa  Qatar Nchini Tanzania Bwana Abdulla Jassim Al – Maadad akisisitiza umuhimu wa Qtar na Zanzibar kuendelea kushirikiana katika masuala ya Utamaduni.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis Ame, OMPR

Qatar  imeelezea shauku  yake ya kutaka kuwekeza miradi ya Uchumi katika Sekta ya Utalii kupitia Taasisi na mashirika yake  kutokana na rasilimali pamoja na mazingira bora   ya uwekezaji yaliyopo  Zanzibar  katika azma yake ya kumarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa  Qatar Nchini Tanzania Bwana Abdulla Jassim Al – Maadad wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Abdulla Jassim Al – Maadad alisema yapo Mashirika na Taasisi kadhaa zinazojishughulisha na mausla ya sekta ya Utalii Nchini  Qatar  mbazo zinaweza kuitumia fursa ya uwekezaji iliyopo katika Visiwa vya Unguja na Pemba  kwa vile  miundo mbinu  ya sekta hiyo tayari imeshaimarishwa vyema na Serikali.

Alisema mazingira mazuri yanayovizunguuka Visiwa vya Zanzibar  katika uwekezaji yamempa  matumaini ya  kuitumia nafasi yake ya Kidiplomasia kujaribu kuyashawishi mashirika na Taasisi za Utalii Nchini mwake kuitumia nafasi hiyo adimu.

Balozi Abdulla Jassim Al – Maadad aliahidi kwamba uhusiano  wa kihistoria uliopo  kati ya Qatar na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla unastahiki kuimarishwa zaidi hasa kutokana na Wananchi wa pande hizo mbili kukaribia kushabihiana Kiutamaduni.

Alisema ipo haja kwa Taasisi za Utamaduni za pande hizo mbili  kufanya mazungumzo ya pamoja yatakayotoa fursa kwa vikundi vya utamaduni vya pande hizo mbili kutembeleana sambamba na kufanya maonyesho ya pamoja katika azma ya kudumia uhusiano huo.

“ Ipo mikataba kadhaa ya ushirikiano iliyowahi kutiwa saini na viongozi wa pande hizi mbili. Sasa si vibaya pia tukauangalia utamaduni ambao ndio Seka Mama inayochangia kuwaunganisha haraka Wananchi wa Mataifa mawili tofauti ”. Alifafanua Balozi wa Qatar Nchini Tanzania Bwana Abdulla Jassim AL-Maadad.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Balozi wa Qatar Nchini Tanzania kwamba Mataifa hayo  yanafanana  katika masuala ya kiutamaduni  jambo ambalo linastahiki kuimarishwa zaidi katika sekta ya uwekezaji.

Balozi Seif alisema Qatar kupitia shirika lake ya usafiri wa Anga inaweza kuanzisha safari za ndege zake kati ya Qatar na Zanzibar kwa vile Zanzibar tayari imeshaimarisha miundombinu ya uwanja wake wa Ndege katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.

Alisema Qatar ina uzoefu mkubwa katika kusimamia masuala ya usafiri wa Anga  jambo ambalo Wataalamu wake wanaweza kutumia fursa waliyonayo katika kufanya utafiti wa kuanzisha safari hizo.

Alifahamisha kwamba Zanzibar imekuwa kituo kikubwa katika usafiri wa Anga chenye uwezo wa kuwaunganisha wasafiri wa Kimataifa kuendelea na safari zao mahali popote Duniani.

Akizungumzia suala la Mabadiliko ya Tabia Nchi  yaliyopo Duniani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi wa Qatar Nchini Tanzania kwamba Zanzibar  imekuwa ikijiandaa na mikakati  mbali mbali katika kukabiliana na  mabadiliko yoyote ya Tabia Nchi yanayoweza kutokea.

Alishauri wataalamu wa Nchi hizo mbili wakaandaa mipango ya kushirikiana katika kufanya utafiti wa pamoja utakaosaidia nguvu zaidi katika kukabiliana na mabadiliko hayo kwa pande zote mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Ushirikiano wa Kimataifa uliopo unaoyaunganisha Mataifa ya Ghuba  ambao umeleta mabadiliko makubwa ya Kiuchumi kwa Mataifa hayo.

Balozi Seif alisema Dunia imekuwa ikishuhudia jinsi Mataifa ya Ghuba  yanavyozidi kuimarika Kiuchumi kutokana na ushirikiano huo unaochangia kuleta ustawi mzuri kwa raia wa Mataifa hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.