Habari za Punde

Sheha wa Kinyasini Ajeruhiwa kwa Kuzuiya Ununuzi wa Karafuu kwa Njia ya Kikombe Pemba.

Na Masanja Mabula -Pemba 
SHEHA wa Shehia ya Kinyasini Wilaya ya Wete  Pemba Raiya Amour Othman amefikishwa katika hospitali ya Wete kwa matibabu  baada ya kupigwa na mwananchi wakati akizuia ununuzi wa karafuu kwa njia ya kikombe katika shehia hiyo .


Taarifa ambazo zimepatikana na mwandishi wa habari hizi zinasema kwamba Sheha huyo alichezea kipigo hicho kutoka kwa Faki Haji Faki  baada ya operesheni aliyoifanya kusaka wauzaji na wanaonunua karafuu kinyume na utaratibu .

Akizungumza na  mwandishi wa habari hizi katika Hospitali ya Wete wakati akipatiwa matibabu , Sheha huyo amesema kuwa alifikiwa na kadhia hiyo baada ya kuzuia kuchukuliwa kwa karafuu ambazo zilikuwa zimenunuliwa kwa magendo .

Amefahamisha kwamba baada ya kuhoji kibali ambacho hutolewa kuruhusu karafuu klusafirishwa kutoka Shehia moja kwenda nyingine , kijana aliyekuwa amezipakia kwenye pikipiki alizishusha na kukimbia .

"Nilikuwa katika oporesheni ya kawaida katika Shehia yangu , ambapo nilibahatika kukuta karafuu zimepakiwa kwenye pikipiki , nilihoji kibali na cha kushangaza mwenye pikipiki alizishusha na kukimbia nikaamini kwamba zilikuwa zimenunuliwa kwa magendo "alifahamisha .


Raiya aliendelea kufahamisha kwamba "Kitendo cha mwenye pikipiki kukimbia ,niliomba msaada kutoka Polisi kuja kuzipakia na kuzipeleka katika Shirika la ZSTC , lakini nilijikuta nikisukumwa na kuanza kupikwa " aliongeza .

Baadhi ya mashuhuda watukio wamesema kwamba baada ya karafuu hizo kushushwa Sheha ilibidi akae juu ya moja ya polo lililokuwa na karafuu wakati akisubiri Polisi wafike na ndipo alipovamiwa na kuanza kupigwa .

Alieleza kwamba alisikia sauti kutoka kwa mtu aliyemfahamu ikisema kwamba karafuu walizouza zimekamatwa hivyo kila aliyeuza anatakiwa kuja kupima na kuchukua karafuu zake kwani mnunuzi amezikimbia na kuziacha .

"Mimi nilikuwa karibu sana na tukio hilo ,na nilisikia sauti kutoka kwa mtu ambaye sikumfahamu ikisema , sheha amezikamata njooni kila mmoja achukuwe karafuu zake kwani dili limeingia mchanga " alieleza .

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Kamishina Msaidizi wa Polisi Hassan Nassir Ali ambaye amesema kuwa limetokea Novemba 23 mwaka huu , wakati Sheha huyo alikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria .

Amesema kwamba Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa za kukamatwa karafuu ambazo zilikuwa zimenunuliwa kinyume na sheria walifika katika eneo la tukio lakini walikuta kesi nyingine ya sheha huyo kupigwa .

" Jeshi la Polisi walifika mapema sana katika eneo la tukio kwa ajili ya kupatikia karafuu , lakini askari walipofika walikua kesi nyingine ya sheha kupigwa na tayari mtuhumiwa Faki Haji Faki ambaye kwa sasa anaendelea kuhojiwa na Jeshi la hilo " alifahamisha Kamanda .

Hivyo Kamanda Nassir amewataka wananchi kuheshimu Sheria za nchi kwa kujiepusha na vitendo ambavyo vimekatazwa na Serikali ikiwamo hili na kununua karafuu kwa njia ya vikombe na pishi .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.