Habari za Punde

Kilute: Kijana Anaesaka Maisha Mithili ya Simba Mkali Akiwa na Njaa Mshahara wa Shilingi 60,000 kwa mwezi Asema Acha Tu…….


Na Haji Nassor, Pemba

“NAFANYA kazi kama Punda saa 24, na kisha nalipwa shilingi 60, 000 kwa mwezi, lakini weee….siiachii, maana sina kazi nyengine na watoto wataka ramba ramba”, ni kauli ya kijana Kilute mlinzi katika mabwawa ya samaki Pujini Pemba.

 Moyo alionao kijana huyo ni adimu kwa vijana wengi wa walio, kuweza kufanya kazi hiyo na hasa kutokana na kima cha kushangaaza anacholipwa na tajiri wake kwa mwezi.

Yeye amemua kujichimbia kwenye mashamba hayo, yanayopigwa na jua kali, akiwa ameshatimiza miezi 48 sasa, akiendeleza kazi yake ya ulinzi ya kulinda mabwawa chini yakiwa na samaki

Yeye hutanga tanga, huku na kule saa 24, kuhakikisha hakuna mtu mbaya atakawezea kulidhuru shamba hilo, linalozalisha mamilioni ya shilingi kwa uvunaji wa samaki, akisaidiwa na tochi wakati wa usiku.

“Mimi hata usiku inabidi hakuna kulala, hapa kazi tuuu….nazungurukia mabwawa yote sita ya samaki, maana wapo wengine hunyemelea kutaka kuvua kwa wizi’’,alisema huku kijasho kikimtiririka.

Kilute, mzaliwa wa Bariad Tanzania bara miaka 28 iliopita, sasa ameshatinga eneo hilo la Pujini na familia yake yenye watoto wawili, ambao hulishwa kwa reheme za Muungu kila siku.

“Unadhani shilingi 2,000 kwa siku ninazolipwa hapa kwa kazi ya ulinzi, na maisha yenyewe makavu kama kigogo cha Mvinje, inawezekana kuiishi? si ndio hizo rehema za Muumba tu’’,alisema kwa masikitiko.


Nilipomuuliza, kwamba inakuwaje anaendelea kushilikia eneo hilo, tena kwa kazi hatari ya ulinzi, anasema hajakata tamaa, maana akiacha hapo hana sehemu nyengine itakayomfanya aendelee kuitwa baba.

Kilute mwenye sura ya bashasha, umbo la kazi na anaeonekana kijana wa kusaka maisha hadi kieleweke, anasema ili kuhakikisha jikoni kwake hakulali Paka, humlazimu kuomba kazi za nje.

“Mimi huwaomba wananchi wa hapa Pujini, kwa wale ambao mashamba yao yako karibu na kazi yangu, niwalimie na wanakubali, na hapo mimi hujihakikisha mkono kwenda kinywani’’,alinieleza.

“Kama ningetegemea hapa tu kwenye shamba la samaki na Chumvi, weweee…….ningekufa njaa, maana hapa hapanilipo hata kidogo, lakini sihami na nnafaraja huko mbeleni’’,alisema kwa kujiamini.

Kubwa kijana Kilute baba wa familia ya watoto wawili na mke mmoja, anasema faraja hiyo, kuona tajiri wa shamba hilo akianza harakati za kweli za kusogeza huduma ya umeme eneo hilo.

Umeme wewe utakusaidia nini kazi yako ya ulinzi, au utafungiwa taaa, hapana sasa tutazalisha chakula cha samaki hapa, na uzalishaji samaki utakuwa juu, na mimi naamini mshahara wangu utanenepa.

Kauli ya Kilute ilioenekana kukaribia matumaini yake, ilitibitishwa na Katibu wa ushirika huo wa ‘Siri fish farm and salt’’ Abdalla Salim Issa, akiwa nyumbani kwake, na kusema tayari jengo la kuzalishia chakula cha samaki lipo.

“Lengo letu kwanza tuufikishe umeme kule kwenye shamba letu, kisha tuzalishe chakula cha samaki hapo hapo, na hivyo uvunaji  wa samaki utaongezeka mara dufu, na mshahara wa Kilute nao utakuwa juu’’,alisema.

“Ni kweli mshahara wa mlinzi wetu ni shilingi 60,000 kwa siku mwezi, lakini kadri siku zikisongambele na pale paking’aa, basi na dishi lake kwa mwezi litatanuka’’,alisema Katibu.  

Yeye mwenyewe anakiri kwamba kazi ya ulinzi waliomuajiri kijana Kilute ni ngumu, lakini akasema, lazima usatahamilivu uwepo, maana sasa neema inakuja.

Kama wahenge walishasema, chanda chema huvishwa pete, sasa miaka michache ijayo, Kilute nae kwenye kazi yake ya ulinzi, atavishwa pete sio ya uchmba ni ya maendeleo.

Mwenyewe Kilute anaona kazi hiyo japo kuwa haikidhi haja kama anavyokusudia, lakini kwa sasa anaamini kwamba ‘baada ya dhiki kwake ni faraja na sio dhiki nyengine’’ na ndio yupo.

Anandoto kuwa, kama jengo la kuwekea mashine ya kuzalishia chakula cha samaki likimalizika, yeye atakuwa juu, kimaisha maana ameshaasikia tetesi kwamba, shamba hilo litafungwa kamera za ulinzi.

 Wizara nyeti Zanzibar hazina kamera za ulinzi CC-Camera, lakini kwenye shamba lako la kufugia samaki na uzalishaji chumvi mtazifunga  kamera hizo, nilimtupia suali hilo Katibu.

Huku akicheka cheka na kushika shika mikono yake, anasema naaam…..”shambani hapo lengo letu ni kufunga kamera hizo, ili kumpunguzia kazi, mlinzi wetu shababi.

Kumbe kilute sasa, ni sawa na kutoka kwenye ulinzi wa analogia sasa kucheza na dijitali, maana kweli zipo taasisi nyeti hadi jana, walinzi wake wanalinda kwa rungu la kipande cha Mvinje.

Hatua ya uwekaji wa kamera hizo maalumu, sio tu kumsaidia mlinzi wa shamba hilo, lakini pia ni kupambana na wale wanaorejesha nyuma nguvu za wenzao.

Kumbe hili la utafutaji wa kamera hizo, ulikuja baada ya mwaka juzi samaki 25,000 kuhujumiwa kwa kuwamgia sumu ndani ya mabwawa hayo, kisha mwaka jana watu wengine wasiofahamika kuwafungulia samaki wengine 18,000 kwenda bahari kuu.

Katibu anasema ufugaji wao wa samaki ni wa hadhi ya juu, maana walishatinga Beijin nchini China mara mbili, kupatiwa mafunzo ya kisasa, na kupiga hatua.

Balozi wa China nchini Tanzania, ameshawahi kukanyaga ndani ya eneo hilo la ufugaji wa samaki, ili kujionea nguvu za kisayansi walizowapa wanaushirika huo, na kisha kuzaa safari ya pili ya kujiunza.

Yote kwa yote Kilute na familia yake baada ya kuchuna uso kwa miaka kadhaa kwa kazi ngumu, inaelekea kwema, maana walishasema wahenga, panapofuka moshi pana moto.

Mzee Khamis Makame (60) wa kijiji cha Kibaridi Pujini anaeishi, urefu wa viwanjwa vitano tu vya mpira wa miguu hadi kwenye mabwawa hayo, ansema wenyewe wanafaidika na mshamba hayo.

“Kama kuna watu wanahujumu kile kinachofugwa, hao hawajui nini maana ya maendeleo na tulipaswa tumsaidie yule mlinzi, maana wakivuna samakini na sisi sote twaneemeka’’,alisema.

Mzee Khamis anasema, hata bei ya samakini wanaovuliwa kwenye mabwawa hayo ni rahisi ikilinganishwa na wengine, sasa lazimi ushirika huo watu wauunge mkono.

Hamad Ali Haji yeye anasema ushirika huo umeshapiga hatua kubwa, na sasa wananchi wa Pujini wamekuwa wakiutegemea kujipatia samaki na chumvi wakati wanapovuna.


Ama kwelii…..muombea ndugu kupata, nae haachi kunona, ni usemi uliowafuma ndani ya mionyo yao wananchi wa Pemba na hasa wanaobwaga ubavu kijiji cha Pujini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.