Habari za Punde

Dk Shein apongeza kamati iliyosimamia utengenezaji meli ya MV Mapinduzi II

Na Khadija Khamis –Maelezo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein ameipongeza kamati ya usimamizi  iliyoshughulikia utengenezaji wa Meli Mpya Mapinduzi II kwa kuweza kukamilika kwake.

Pongezi hizo alizitoa leo huko Bandarini wakati wa uzinduzi wa Meli hiyo ya kisasa ya ambayo imetengenezwa na Kampuni ya Daewoo International  kutoka  Korea ya Kusini.

Alisema kuwa Meli hiyo ni mpya na yenye mitambo ya kisasa yenye uwezo mkubwa  ambayo haiyumbishwi, kwani ina vyombo maalumu vya kurekebisha mwenendo wa mawimbi mkondoni.

“Wananchi Msisikilize maneno ya mitaani kuwa Meli imeshatumika suala hilo halina ukweli, nawataka muje kuitembelea meli hiyo ili  kuweza kujionea wenyewe”. Amesema Dkt Shein.

Aidha alisema kuwa utaratibu wote wa utengenezaji tokea hatua ya awali hadi kumalizika kwake umeonyesha na Kampuni ya Daewoo ya Korea haiwezi kudanganya na kuihadaa Dunia na imeweza kugharimu Dola million 30.4 za kimarekani na ujenzi ulianza mnamo July 2013 hadi Disemba 2015 kuwasili Zanzibar.

Rais wa Zanzibar alisema kuwa kazi iliokuwepo  hivi sasa ni wananchi kuweza kuitunza  na kuihifadhi  meli hiyo ibakie kuwa na haiba na uzuri wake.

Aidha alisema kuwa Meli ya Mapinduzi II ni mpya na ya kisasa  yenye uwezo mkubwa wa kusafirisha abiria 1200  na mizigo tani 200.

Alifahamisha kuwa kukamilika kwa meli hii mabadiliko makubwa yameweza kufanyika katika shirika la meli na uwakala tiketi zinauzwa kwa njia za kutumia komputa abiria hawezi kuuziwa tiket mpaka awe na kitambulisho cha Mzanzibar ,Mtanzania au kwa mgeni awe shahada ya kusafiria.

Pia alieleza kuwa Serikali inategemea kuweka Bandari kubwa ya mizigo eneo la Maruhubi mpiga duri na tayari imeshaanza makubaliano na Serikali ya China kuanzia mwezi wa Januari au Febuari wanatarajiwa kuanza  kazi ya ujenzi.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Utengenezaji wa Meli ambae pia ni Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee amesema ameridhika na umalizaji wa meli hiyo na kutoa shukrani kwa wale wote waliokuwa sambamba katika kukamilisha kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.