Habari za Punde

Zanzibar Press Club (ZPC) yafanya usafi hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo Chekundu

Na Mwinyimvua Nzukwi, 

Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) yaungana na Watanzania wengine kuadhimisha siku ya uhuru wa Tanzania bara (Tanganyika) kwa kufanya usafi katika hospitali ya wagonjwa wa akili Zanzibar iliyopo Kidongo chekundu, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa klabu hiyo Faki Haji Mjaka alisema kufanya hivyo pia ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alilolitoa siku chache baada ya kuingia madarakani.

Kwa mujibu wa agizo la Dk. Magufuli aliahirisha maadhimisho ya mwaka huu ya  sherehe hizo ambazo kikawaida huadhimishwa kwa gwaride rasmi la vyombo vya ulinzi na usalama, badala yake aliwataka watanzania waitumie siku hiyo kwa kufanya usafi wa mazingira yanayowazunguka ili kujiepusha na maradhi na namna ya kuidumisha dhana ya ‘uhuru na kazi’ iliyokuiwa ikitumiwa na waasisi wa taifa la Tanzania mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai uhuru wa iliyokuwa Tangayika ambayo kwa sasa ni Tanzania bara.
Mjaka uamuzi wa dk. Magufuli umeonyesha hisia za kizalendo na kwamba klabu yake imeamua kuiadhimisha siku hiyo mahali hapo ikiamini kuwa mbali ya kuyaweka mazingira ya eneo hilo katika hali ya usafi, pia itaihamasisha jamii kujitolea na kufanya kazi katika maeneo ya kijamii na kuondoa dhana ya unyanyapaa kwa makundi hayo ya kijamii.

“Wagonjwa wa akili ni miongoni mwa kundi linalohitaji uangalizi wa karibu wa jamii nzima mbali ya madaktari wanaowahudumia wagonjwa hao hivyo sisi kama sehemu ya jamii tumeona wajibu wa kuwa karibu nao japo katika siku hii muhimu katika historia ya taifa letu”, alisema Mjaka.

Aidha aliushukuru uongozi wa wizara ya afya na hospitali hiyo kwa juhudi wanazochukua katika kuiweka hospitali hiyo katika mazingira mazuri na kuwataka wadau wa habari na wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kuiadhimisha siku hiyo.

Siku ya uhuru wa Tanzania bara (Tanganyika) huadhimishwa kila ifikapo Disemba 9 kukumbuka juhudi za wapigania uhuru wa iliyokuwa Tanganyika ambapo kwa mwaka huu Tanzania itakuwa inaadhimisha miaka 54 ya uhuru huo uliopatikana mwaka 1961 kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.