STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 7.1.2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema
tofauti za kisiasa Zanzibar kamwe zisitumike kuvuruga amani na utulivu ambayo
ndiyo siri kubwa ya maendeleo yaliyopatikana katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Dk. Shein ambaye alikuwa akizungumza na
wananchi wa Wete waliokwenda kumsalimia mara baada ya kagua ujenzi wa soko na
Ofisi ya Baraza la Mji Wete alisema kuwa suala la amani halina mbadala huku
akiahidi kuendelea kuisimamia amani ya Zanzibar na kusikitishwa na wale wote
wanaotaka kuvuruga amani kwa kisingizio cha kuiongoza Zanzibar.
Alisema kuwa amani na utulivu uliopo ndio
msingi wa maendeleo ya Zanzibar hivyo Wazanzibari wanapaswa kuienzi na kuilinda
kwa nguvu zao zote.
Dk. Shein alisisitiza kuwa kila mwananchi
anataka kuishi kwa amani na utulivu na kuwataka wananchi wa Zanzibar kutambua
kuwa wao ni ndugu na kuwasihi baadhi ya wananchi wanaotaka kuvuruga amani na
kuendelea kutisha wenzao kwani Zanzibar inaongozwa kwa Sheria na Katiba.
“watu wasihemkwe wala wasichagawe kwani
kila mmoja anataka kuishi kwa amani na utulivu sisi ni wamoja wa kusini Pemba,
Kaskazini Pemba wa Kusini Unguja na Kaskazini Unguja...tumetofautiana kwa kuishi
na kutafuta maisha tu”,alisema Dk. Shein.
Kwa upande wa mradi huo Dk. Shein
alirejea kauli yake kama aliyoizungumza wakati akiitembelea miradi kama hiyo
katika miji ya Wete na Chake kwa kusema kuwa hizo ni miongoni mwa ahadi zake
alizowaahidi wananchi za kuimarisha miji yote ya Zanzibar.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa
mradi huo wa (ZUSP) sio mradi uliozuka bali umebuniwa na Serikali na ni mkopo
wa Dola milioni 38 kutoka Benki ya Dunia.
Mapema Dk. Shein alikagua ujenzi wa
barabara ya Ole-Kengeja ambao ujenzi wake unaendelea na kwa maelezo ya Katibu
Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Dk. Juma Malik Akili barabara hiyo
inatarajiwa kuanza kutiwa lami mnamo mwezi Septemba mwaka huu,
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi wa
Baraza la Mji Wete Mgeni Othman Juma alisema kuwa ujenzi wa mradi huo wa soko
umeanza April 4 mwaka jana na unatarajiwa kumaliza April mwaka huu, kwa mkopo
wa Benki ya Dunia.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa katika soko
hilo kuna milango 35 ya biashara, milango 80 ya biashara ya mboga mboga,
milango 15 ya biashara nyengine, kituo cha mabasi, banda la kusubiria gari na
sehemu nyenginezo za kibiashara.
Katika maelezo hayo Tshs. Bilioni 1 zinatarajiwa
kutumika na kwa hivi sasa ujenzi wa mradi huo umeshafikia asilimia 60 huku
uongozi huo ukieleza kuwa lengo la mradi huo ni kufanya biashara na kuwalenga wafanyabiashara
kufanya shughuli zao katika mazingira bora.
Sambamba na hayo, alieleza kuwa hatua
hizo ni miongoni mwa juhudi za kupamabana na umasikini chini ni Dira ya 2020
pamoja na Mkakati wa Kukuza uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA).
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar
Khamis Othman aliahidi kuzishughulikia changamoto zilizopo hivi sasa katika
eneo hilo la ujenzi na kuahidi kupata mafanikio.
Ujenzi wa soko hilo ni miongoni mwa
mageuzi ya Serikali za Mitaa ambao utagharibu Dola laki 8.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment