Habari za Punde

Balozi Seif azindua skuli mpya ya Msingi ya Mahuduthi Mkoani Pemba


Na Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kwamba matokeo ya Mitihani ya wanafunzi katika maskuli tofauti nchini yatakuwa mazuri siku zote iwapo wazazi watajenga utaratiu wa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao badala ya kusubiri kupelekewa matokeo ya mwisho wa mwaka.


Alisema ili wanafunzi waweze kufanya vizuri zaidi katika masomo yao ushirikiano wa karibu zaidi  utahitajika muda wote baina ya walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo baada ya kuizindua rasmi skuli mpya ya Msingi ya  Mahuduthi iliyomo ndani ya shehia ya Mkungu Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za Maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
mwaka 1964.

Alisema kazi ya mwalimu ni kumpatia masomo mwanafunzi wakati jukumu la mzazi ni kuhakikisha kile anachofundishwa mtoto na mwalimu wake skulini anakipatia muda wa kukidurusu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wazazi  na walezi kutoogopa gharama anazopaswa kusomeshwa Mtoto kwani huo ndio uwekezaji stahiki unaotakiwa kwa kizazi kitakachosimamia jukumu la uendeshaji wa Taifa hili hapo baadaye.

Balozi Seif alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshajipanga katika kuona wazee na wazazi hawachangii fedha katika ngazi ya elimu ya msingi pamoja na gharama zote za Mitihani kwa ngazi ya msingi na Sekondari.

Alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeshajipanga kutekeleza Tamko la Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuanzia mwezi huu wa Januari kwa kusambaza vifaa mbali mbali ikiwemo chaki, madaftari ya kuandikia na mabuku ya mahudhurio katika skuli zote za
msingi na sekondari za Unguja na Pemba.

Alifahamisha kwamba hivi sasa yapo mafanikio makubwa ambayo wananchi wenyewe katika maeneo yao wanastahiki kujipongeza akatolea mfano wa ongezeko la majengo ya skuli ndani ya Wilaya ya Mkoani ambalo wamelisimamia kwa nguvu zao na kupata msaada serikalini pamoja na washirika wa maendeleo.

Alisema Wilaya ya Mkoani kwa sasa ina Skuli 61 ambapo kati ya hizo 51 zinasimamiwa na Serikali kuanzia maandalizi hadi Sekondari ikilinganishwa na enzi za kabla ya Mapinduzi ambapo Wilaya hiyo ilikuwa na skuli 6 tu za msingi bila ya sekondari wala ile ya maandalizi.

Alieleza kwamba kasi ya uandikishaji wanafunzi imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia asilimia 32.7 ya uandikishaji wa watoto katika ngazi ya elimu na maandalizi, asilimia 107.6  ngazi ya elimu na msingi na asilimia 58.9 katika ngazi ya sekondari.

Hata hivyo alisema kwamba pamoja na mafanikio hayo lakini takwimu zinaonyesha wazi kuwa bado wapo watoto wengi wanaokosa haki yao ya msingi ya kupata elimu hasa katika ngazi ya maandalizi na sekondari.

Alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao skuli ili wapate haki yao ya elimu itakayolisaidia Taifa kupiga hatua za maendeleo kwa kuwa na wananchi walioelimika katika fani tofauti zitakazowapa weledi wa kuleta maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru na kuupongeza Uongozi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Milele Zanzibar Foundation kwa misaada mbali mbali unaotoa katika kuunga mkono jitihada za Serikali kuu Katika kuwaletea maendeleo Wananchi wake.

Alisema jitihada na uzalendo ulioonyeshwa na shirika hilo ni mfano mzuri wa kuigwa na kuuhakikishia kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar italipa msaada wowote unaostahiki katika juhudi zake za kusambaza huduma mbali mbali kwa wananchi wote.

Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi, Walimu na wanafunzi hao wa skuli ya msingi ya Mahuduthi Balozi Seif aliahidi kuisaidia skuli hiyo Kompyuta,Mashine za Fotokopi na Projector kwa lengo la kuiwezesha skuli hiyo iende na wakati wa sasa wa sayansi na teknolojia.

Akisoma risala ya Walimu, wazazi na wanafunzi wa skuli ya msingi ya Mahuduthi Mwalimu Suleiman Moh’d Haji alisema uamuzi wa ujenzi wa majengo ya skuli hiyo ulichukuliwa na wazee wa Kijiji hicho kwa nia ya kuwasaidia watoto wao kuondokana na usumbufu wa kufuata elimu katika skuli za mbali za Mtambile na Kengeja.

Mwalimu Suleiman alisema kazi za ujenzi skuli hiyo zilianza Tarehe 6 Febuari mwaka 2011 chini ya usimamizi wa sheha wa Shehia ya Mkungu ambapo baadaye Wananchi hao waliungwa mkono na Uongozi wa shirika la Milele Zanzibar Foundation katika  hatua za ukamilishaji.

Licha ya mafanikio hayo Mwalimu Suleiman alitanabahisha kwamba zipo changamoto zinazoendelea kuviza maendeleo ya skuli hiyo akizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uhaba wa walimu, upungufu wa maji safi na salamapamoja na vifaa vya kisasa vya kufundishia.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid alitahadharisha kwamba suala la kufanywa Siasa  kama ibada linaweza kuwaweka mahala pabaya watu wanaoamua kuacha shughuli za kuwapatia kipato cha kukidhi mahitaji yao na familia zinazowazunguuka.

Mh. Mwanajuma alisema wapo baadhi ya walimu maskulini wameamuwa kuendesha siasa kwa kuwaandaa wanafunzi wao wawe na tabia ya kupinga kila kitu kinachofanywa na kuagizwa na viongozi  na watendaji waliopewa jukumu au dhamana  na Serikali Kuu.

Aliwanasihi walimu wenye hulka kama hiyo kuelekeza nguvu zao katika kuwajengea mazingira bora ya kielimu wanafunzi wao ili lile lengo la Serikali ya Chama cha Ukombozi cha Afro Shirazy Party wakati wa kupigania ukombozi wa Visiwa hivi  liweze kufanikiwa.

Zaidi ya shilingi Milioni 300 zimegharamia ujenzi huo ambapo kati ya hizo shilingi Milioni 14 ni nguvu za wananchi na zile zilizobaki zilibebwa na Uongozi wa shirika la Milele Zanzibar Foundation.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.