Habari za Punde

Sintofahamu yaibuka Bungeni leo





Vurugu na sintofahamu imeibuka muda mfupi uliopita katika mkutano wa Bunge uliokuwa unaendelea mjini Dodoma.

Taarifa kutoka kwa waandishi wa habari waliokuwa ndani ya Bunge hilo zimeeleza kuwa polisi walilazimika kuingia ndani kuwatoa nje wabunge wa upinzani kufuatia maigizo ya mwenyekiti wa kikao hicho, Andrew Chenge, baada ya kukaudi amri ya kutoka nje.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa awali, wabunge wa upinzani walipinga kuendelea kwa mjadala wa Bunge wakitaka kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, sanaa na michezo, Nape Nnauye kuhusu TBC kutorusha ‘Live’ matangazo ya Bunge ijadiliwe kwanza.

Mwenyekiti wa Bunge alieleza kuwa huo haukuwa muda wa mjadala huo na kutaka Bunge liendelee na ratiba yake.

Hata hivyo, wabunge wanne pekee wa Upinzani ndio waliokuwa wametakiwa kutoka nje ya Bunge, lakini wabunge wote wa Ukawa waliwatetea na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali. Hivyo, Mwenyekiti aliamuru wote watoke nje ili wabunge wengine waendelee kujadili hotuba ya Rais.

Mwandishi wa East Africa Radio aliyekuwa ndani ya Bunge alieleza kuwa Mwenyekiti wa Bunge aliondoka kwenye kiti chake wakati vurugu hizo zikiendelea na waandishi wa habari waliagizwa kutoka nje.

Wakati wa kiako cha asubuhi Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge amelazimika kuahirisha kikao  cha Bunge mara mbili leo asubuhi baada ya wabunge wa upinzani kupinga hoja ya serikali ya kutorusha moja kwa moja shughuli zote za Bunge hicho kupitia TBC.

Vuta nikuvute hiyo ilitokana na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kutoa kauli ya serikali kuwa TBC itapunguza muda wa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kituo hicho cha luninga cha umma.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) akiungwa mkono na wabunge wenzake kutoka kambi ya upinzani, alipinga hoja hiyo ya serikali na kumtaka Chenge asitishe mjadala wa hotuba ya Rais John Magufuli hadi hoja hiyo ya serikali itakapojadiliwa.

Zitto alisema TBC ni mali ya umma na inaendeshwa kwa kodi za wananchi ambao wana haki kuhabarishwa bila kuangalia gharama zinazotajwa na serikali kwani kituo hicho hakiendeshwi kibiashara.

Huku Chenge akijitahidi kumtuliza ili ratiba ya Bunge iendelee kama ilivyopangwa, Zitto aliungwa mkono na Halima Mdee, Mbunge wa Kawe (Chadema) hali iliyomfanya mwenyekiti huyo aliyechaguliwa jana kusema ataagiza Kamati ya Uongozi kujadili mara moja.

Kana kwamba hiyo haitoshi, wabunge wa upinzani walimjia juu Chenge kutaka Bunge lisiendelee kujadili hotuba ya Dk Magufuli iliyorushwa ‘live’ mwishoni mwa mwaka jana, mara baada ya kuapishwa kuwa rais wa nchi.

Baada ya malumbano yaliyoambatana na kurushina vijembe baina ya wabunge wa kambi ya upinzani na wale wa chama tawala, CCM, Chenge alisitisha kikao cha Bunge kwa saa moja kutafakari hoja hiyo.

Hata hivyo Chenge aliyesitisha kikao cha bunge kupisha Kamati ya Uongozi kukutana na kutoa mrejesho baada ya saa moja alilazimika kuahirisha tena Bunge hadi jioni.

3 comments:

  1. Nape...nape.......una nini na nchi yetu ya aman lakini? toka lini nchi yetu ikafanya mambo kama hayo uliyoyafanya? au ni wewe na maamuzi yako?

    ReplyDelete
  2. Hayo ni maamuzi ya ccm sio nape.

    ReplyDelete
  3. Tatizo la nchi hii ni CCM siku chama hiki kikifa ndio mwanzo wa maendeleo ya taifa hili historia itatueleza kwa kuwa haisemi uongo.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.