Habari za Punde

Uzinduzi wa Mradi wa Afya Bora ya Mama na Mtoto Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Halima Maulid Salum akifungua warsha ya uzinduzi wa Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto katika Hoteli ya Mzson Shangani Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Idara ya Kinga na elimu ya  afya Dkt. Mohd Dahoma akizungumza na washiriki  waliohudhuria katika warsha ya uzinduzi wa mradi wa  Afya bora ya Mama na Mtoto katika ukumbi wa Hoteli ya mazson Shangani mjini Zanzibar.
Meneja wa Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto kutoka Shirika la kuhudumia watoto  Tanzania Dkt. Bernard Mbwele akitoa maelezo juu ya mtazamo wa mradi huo  kwa washiriki katika Hoteli ya Mazson Mjini Zanzibar.
Meneja Msaidizi wa  Shirika la kuhudumia watoto Dkt. Awrad Saleh akiwasilisha mada ya majukumu ya waangalizi na wakaguzi wa Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto wakati wa uzinduzi wake.
Daktari dhamana Kanda ya Unguja  Dkt. Fadhil Mohd akitoa mchango wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto katika Hoteli ya Mzson Shangani Mjini Zanzibar.
Baadhi ya washiriki katika  uzinduzi wa Mradi wa Afya ya mama na mtoto uliofanyika Hoteli ya Mzson Shangani wakifuatilia uzinduzi huo.

(Picha na Abdalla Omar /Maelezo Zanzibar.)

Na Ramadhan Ali./Maelezo Zanzibar.
Kiasi ya kinamama wajawazito 45,000 na watoto wachanga 75,000 kutoka shehia zote za Unguja na Pemba watafaidika na Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto unaosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto.

Meneja wa Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto kutoka Shirika la kuhudumia watoto Tanzania Dkt. Bernerd Mbwele akizungumza katika warsha ya uzinduzi wa mpango  huo  katika Hoteli ya Mazson, Shangani amesema lengo ni kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Amesema Serikali ya Canada kupitia Shirika la UNICEF limefadhili mradi huo kwa kipindi cha mika miwili na utavihusisha  vitengo vya Lishe, elimu ya afya kwa jamii na kitengo cha afya ya mama na mtoto pamoja na jamii zinazoishi ndani ya shehia husika.

Katika kufanikisha  Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto Dkt. Bernerd Mbwele amesema maafisa wa afya kutoaka vitengo hivyo vitatu watashirikiana na watu wakujitolea watakaochaguliwa kutoka ndani ya shehia na waangalizi maalum.

Amewataka viongozi wa shehia kuwa makini wakati wa kuwateua watu wa kujitolea ili wawe wenye uwezo na wanaoheshimika ndani ya jamii.


“Ili mradi huu uweze kufanikiwa tujiepushe kuchagua watu wa kujitolea kwa misingi ya itikadi za kisiasa tutafeli, muhimu tuchague watu wenye uweze wa kusaidia,” alisisitiza Dkt. Bernerd.

Ameongeza kuwa mradi utatoa mafunzo maalum kwa watu wa kujitolea ambao  kwa kushirikianana na maafisa wa afya watawapa ushauri mama wajawazito umuhimu wa kwenda vituo vya afya mapema kujua afya zao na kujiepusha na  tabia ya kujifungulia majumbani ili kuhakikikisha usalama  wakati wa kujifungua na watoto wanaozaliwa.

Mkurugenzi Idara ya Kinga Dkt. Mohd Dahoma amesema katika mradi huo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na waangalizi na watu wa kujitolea wa shehia watakuwa na jukumu la kuwafuatilia mama wajawazito hadi wakati wa kujifungua ili kuhakikisha wanapata huduma zote za afya na watoto watakaozaliwa hadi kipindi cha miaka mitano.

Amewataka wananchi kuunga mkono mpango huo ambao lengo lake kubwa ni kupunguza asilimia 44 ya vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Akizindua Mradi wa Afya bora ya mama na mtoto, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Halima Maulid amewakumbusha wafanyakazi wa afya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili kufanikisha mradi huo.

Amesema wafadhili wa maendeleo kwa kuthamini hadhi ya mama na mtoto wametoa fedha nyingi ili kuhakikisha idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vinapungua na hatimae kuondoka kabisa.

Amesema vitengo vya Lishe, elimu ya afya na kitengo cha mama na mtoto viliopo katika Wizara ya Afya vinatakiwa kuandaa mikakati kuhakikisha mama wajawazito wote wanajifungulia sehemu zenye huduma za afya na kuwashawishi kunyonyesha watoto wanaozaliwa maziwa ya kufua pekee kwa kipindi cha miezi sita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.