Habari za Punde

Muuzaji Bora na Umuhimu wa Kulinda Ubora wa Zao la Karafuu


Picha 1: Kushoto uwanikaji wa karafuu usio sahihi na kulia ni uwanikaji sahihi.
Baadhi ya Wananchi na Wakulima wa zao la karafuu  kijiji cha Mchangamtogo Pemba wakiangalia sinema ya elimu ya uimarishaji wa zao la karafuu

Na Ali Mohammed ZSTC.
Zanzibar ni miongoni mwa nchi zenye kutegema mazao ya kilimo katika kujenga uchumi wake.Wakati Zanzibar ikiwa inategemea zao la karafuu katika kukuza uchumi wake, nchi kama vileIvory Coast inategemea Kokoa na Kahawa, Ghana inategemea Kokoa, Ethiopia Kahawa, Uganda Kahawa, Kenya kahawa na Chai, Tanzania Bara inategemea Kahawa, Korosho na Chai.

Nchi ambazo zinategemea zao la karafuu kama ilivyo Zanzibar kwa kuwa sehemu ya pato la nchi na kukuza uchumi wake ni pamoja Indonesia, Madagascar,  Comoro, Sri Lanka, Brazil na India.
Sifa na Ubora wa mazao ya kilimo cha biashara katika kukuza uchumi ni kulinda ubora wa mazao hayo. Mazao yenye sifa ya ubora ndio yenye bei nzuri katika soko la ndani na nje. Sifa na Ubora ni kielelezo cha kulinda na kudhibiti mazao hayo katika soko la ndani na nje.
Nchi nyingi zimepitia katika hatua mbali mbali za Mageuzi katika uimarishaji wa Sekta za Kilimo ili kuzifanya sekta hizo kua endelevu kwa maslahi ya nchi  na wananchi wake.

Baadhi ya nchi, kilimo cha zao la karafuu hakikupewa kipaumbele sana kutokana na kuwa mchango wake katika jitihada za kukuza uchumi wa nchi husika ni mdogo.

Zanzibar - imetoa kipaumbele kwa zao la karafuu kwa kulifanya kuwa sekta inayomilikiwa na Serikali kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha uchumi.
Indonesia - Serikali inasimamia kwa karibu sana zao la karafuu kwa kuchukua hatua mbali mbali za kurekebisha kasoro zinazoonekana kuleta athari kwa zao hilo.  Usimamizi huo ndio ulioleta mafanikio ya kuwa wazalishaji wakubwa na ndio wanaongoza duniani.

Madagascar - ni jitihada za Wakulima wenyewe wanazozifanya ili kujiongezea kipato ila wanahakikisha suala la ubora wa karafuu zao linazingatiwa na linakuwa ndio kigezo cha ongezeko la thamani ya karafuu na kipato chao.
Comoro- Wao ni jitihada za Wakulima wenywe za kujiongezea kipato lakini juhudi zao zimekuwa zikizaa matunda kwani zimeifanya nchi hio kuwa ya nne (4) katika uzalishaji wa karafuu duniani.

India – Wakulima wanajitegemea wenyewe, na zao hilo hushuhgulikiwa na matajiri kwani kushughulikia kilimo cha mikarafuu ni kazi inayohitaji kujituma na uwezo wa kifedha.

Sri-Lanka – Inafahamika kwa uzalishaji wa viungo (spices) zikiwemo karafuu. Kwa ujumla nchi hii inasafirisha asilimia 56 (56%) ya viungo vinavyosafirishwa nje, inaingiza fedha za kigeni asilimia 80 (80%).  Kwa kiasi kikubwa Serikali inashughulikia mageuzi ya sekta hii hasa katika kudhibiti na kulinda ubora.

Mageuzi ya Sekta za Kilimo ndio yanayotoa mabadiliko ya mfumo wa uendelezaji, uimarishaji na usimamizi wa sekta za mazao ya kilimo katika nchi ambayo nayo hutegemea Sera za Biashara za nchi hizo.

Zanzibar inatekeleza mageuzi kwa kuiimarisha sekta ya karafuu ili iwe endelevu na yenye kuleta tija kwa nchi na wananchi wake kutokana na karafuu kuwa ni zao lenye faida kubwa.

Nia ya Serikali kwa zao hili ni kuwa endelevu na lenye kuleta tija zaidi kwa Wananchi ndio maana Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) limekuwa likichukuwa jitihada kubwa katika kuimarisha zao hilo na kulinda ubora.

Kwa lengo la kuhamasisha wakulima kulinda ubora wa zao la karafuu Shirika la ZSTC limeanzisha mpango maalum wa kuwazawadia wauzaji bora wa zao hilo, kila Wilaya ni lazima apatikaneMuuzaji mmoja bora ambapo huzawadiwa fedha taslim.

Je ni zipi Sifa za Muuzaji Bora wa zao la Karafuu?

Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu Ali Suleiman Mussa na Mkurugenzi Masoko wa Shirika la ZSTC- Zanzibar Salum Abdalla Kibe wamelezea kwa undani sifa na vigezo vya Muuzaji bora wa karafuu na umuhimu wa kulinda ubora wa zao la karafuu.

Uuzaji mwingi wa Karafuu
Muuzaji bora ni lazima awe ameuza karafuu nyingi kulinga na kumbukumbu za manunuzi za Shirika la ZSTC katika Wilaya husika aliyopo Mkulima. Lengo la kigezo hichi ni kuwashajihisha Wakulima kuitikia wito wa Serikali wa kuziuza karafuu zote katika vituo vya Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) na kuachana kabisa kuuza kwa magendo.

Kwa upande wake, Serikali imekuwa ikiahidi kuendelea na azma yake ya kuwapa Wakulima bei nzuri kila bei ya karafuu inapopanda kwenye soko la dunia na kuwalipa pesa zao taslim bila ya kuwakopa na bila ya kuchelewa.

Awe mmiliki wa Shamba au kukodi
Muuzaji bora ni lazima awe anamiliki shamba/mashamba au awe anakodi mashamba kwa njia za halali/kisheria. Lengo la kigenzo hichi ni kuweka haki, usawa na uadilifu katika bishara hii ya zao la karafuu.

Pia kigezo hichi kinaondoa tabia ya baadhi ya watu kununua karafuu mitaani kwa njia zisizokuwa rasmi ‘vikombe’ na kuondoa tabia ya wizi na ukataji wa mikarafuu mashambani kutokana na kuzoeleka kwa biashara hiyo ya ununuzi wa karafuu mbichi.

Watu wanaofanya biashara hiyo ‘Vishoka’ hawazingatiwi na Shirika la ZSTC na wala hawafahamiki kisheria, ni Shirika la ZSTC pekee lililopewa mamlaka ya kununua na kuuza karafuu.

Awe anaanika vizuri kwa kutumia vifaa vinavyotakiwa

Muuzaji bora wa karafuu ni yule anaezingatia ubora wa karafuu zake kwa kuanika vizuri, katika sehemu nzuri na safi. Awe anatumia majamvi kwa kuanikia, jamvi ni kifaa pekee kinachaoshauriwa na Shirika la ZSTC kutumika kwa kuanikia karafuu.

Karafuu zilizoanikwa vizuri kwa kutumia majamvi huwa na sifa nzuri za ubora kama vile kukauka vizuri, rangi nzuri ya kahawia, haitoki vichwa, harufu nzuri ya kuvutia na mara zote huwa ni daraja la kwanza ambapo mkulima hupata fedha nzuri.
Zifa hizo nzuri za ubora huwa haiwezekani kupatikana kwa karafuu zinazoanikwa barabarani, juu ya mabati na sakafuni ingawa baadhi ya Wakulima wanaanika katika sehemu hizo. Watu hao hawawezi kuwa bora kwa sababu wanahatarisha ubora wa zao la karafuu katika soko la nje na kushusha thamani yake.

Karafuu ziwe zinakauka vizuri kwa kiwango kinachotakiwa
Kwa mujibu wa viwango vya ukaukaji wa karafuu kwa Shirika la ZSTC, karafuu zinatakiwa zikauke vizuri na zisiwe na unyevu unaozidi aslimia 14 (14%). Kwa mujibu wa kiwango hicho Mkulima anatakiwa ahakikishe karafuu zake zinapata jua la kutosha sio chini ya siku tatu.

Wakulima wanapopeleka karafuu zao katika vituo vya manunuzi wakati zikiwa hazijakauka inavyotakiwa hupelekea usumbufu vituoni kwa kutakiwa kuanika tena na kama zikinunuliwa na kuhifadhiwa katika maghala karafuu hizo hupugua uzito kwa kiwango kikubwa na hata wakati mwengine kufanya ukungu.

Karafuu zake zinatakiwa kuwa safi
Muuzaji bora lazima azingatie suala la usafi wa karafuu zake, karafuu hizo zisiwe na vitu visivyohitajika. Kwa mujibu wa vigezo vya Shirika la ZSTC karafuu hazitakiwi ziwe na taka zinazozidi asilimia 4 (4%).

Kwa bahati mbaya wapo baadhi ya watu huwa wanachafua karafuu zao kwa makusudi kwa kuingiza unga wa makonyo kwa lengo la kuongeza uzito na wengine huanika barabarani ambapo karafuu hizo huchafuka kwa kuingia kokoto, lami, moshi wa magari na ushafu mwengine.

Uhuhimu wa kulinda ubora wa zao la karafuu
Kulinda ubora huongeza thamani ya zao la karafuu katika soko la nje na kupata bei nzuri. Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mpango wa kuipandisha hadhi karafuu ya Zanzibar kutokana na sifa zake za kipekee kupia mradi wa ‘Brading’.

Zanzibar sio nchi pekee inayozalisha zao la karafuu, kuna nchi nyengine kama vile Indonesia, Madagascar, Comoro, India, Sri-Lanka na Brazil nazo zinazalisha karafuu. Kulinda ubora kunapelekea karafuu za Zanzibar kuhimili ushindani katika soko la nje.
Zao la karafuu ni zao la uchumi wa nchi na ni zao la biashara hivyo linahitaji masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi. Kulinda ubora kunasaidia sana kukaribisha masoko mapya ya zao la karafuu.

Ni vyema Wakulima wa zao la karafuu wakatumia fursa ya mpango wa Shirika la ZSTC la kwazadia Wauzaji bora kuimarisha zao la karafuu kwa kulinda ubora wa zao hilo ili kuwa na uhakika wa soko na kuongeza tija.
​​
“Karafuu ni Uhai, Karafuu kwa Maendeleo ya Zanzibar”.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.