STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21.3.2016
MWENYEKITI wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Mhe. Jecha Salim Jecha leo amemtangaza rasmi Mhe.
Dk. Ali Mohamed Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba amechaguliwa kihalali
na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kupata kura 299,982 sawa na asilimi 91.4.
Akitangaza matokeo hayo huko katika
ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, Mhe. Jecha alisema kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar tayari
imeyathibitisha matokeo ya wagombea na imeridhia kuwa matokeo hayo ni sahihi na
hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, 1984 kifungu cha 34 na Sheria ya
Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 42 (4).
Kwa mujibu wa maelezo ya Mhe. Jecha
wapiga kura waliothibitishwa kwa kupiga kura baada ya uhakiki wa Daftari la
Kudumu la wapiga kura ni 503,580 ambapo wapiga kura waliopiga kura kumchagua
Rais wa Zanzibar walikuwa ni 341,865 sawa na asilimia 67.9 ya watu waliokuwa na
sifa ya kupiga kura.
Alisema kuwa kura zilizoharibika zilikuwa
ni 13,538 sawa na asilimia 0.4 ambapo kura halali alizopata kila mgombea
zilikuwa ni Mhe. Khamis Idd Lila wa ACT
WAZALENDO alipata kura 1,225 sawa na asilimia 0.4, Mhe. Juma Ali Khatib wa ADA-
TADEA alipata kura 1,562 sawa na asilimia 0.5, Mhe. Hamad Rashid Mohammed wa
ADC kura 9,734 sawa na asilimia 3.0.
Mhe. Said Soud Said wa AFP kura 1,303
sawa na asilimia 0.4, Ali Khatib wa CCK kura 1,980 sawa na asilimia 0.6, Mhe.
Mohammed Rashid Masoud wa CHAUMMA kura
493 sawa na asilimia 0.2, Seif Sharif Hamad wa CUF kura 6,076 sawa na asilimia
1.9, Tabu Mussa Juma wa D- MAKINI kura 210 sawa na asilimia 0.1, Mhe. Abdulla Kombo
Khamis wa DP kura 512 sawa na asilimia 0.2.
Wengine ni Mhe. Kassim Bakari Aly wa
Jahazi Asilia kura 1,470 sawa na asilimia 0.4, Mhe. Seif Ali Iddi wa NRA kura
266 sawa na asilimia 0.1, Mhe. Issa Mohammed Zonga wa SAU kura 2,018 sawa na
asilimia 0.6 na Mhe. Hafidh Hassan Suleiman wa TLP kura 1,499 sawa na asilimia
0.5.
Katika hotuba yake Mwenyekiti huyo wa
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar aliwaomba wafuasi wa vyama vyote vya siasa na
wananchi, kumuunga mkono Rais Dk. Shein na kushirikiana katika kupigania
maendeleo ya visiwa vya Zanzibar katika kipindi kijacho cha miaka mitano.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa
pongezi kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, chama cha CCM pamoja na wananchi wote
waliomchagua na wasiomchagua kwa kupanda ushindi huo wa kishindo.
Dk. Shein alisema kuwa anaheshimu na anathamini
sana heshima hiyo ya ushindi alioupata na kuahidi kuwa ataitumikia Zanzibar na
watu wake kwa nguvu zake zote tena bila ya ubaguzi.
Aidha, Dk. Shein aliahidi kutenda haki
kwa wananchi wote wa Zanzibar huku akihakikisha kuwa Zanzibar inapata maendeleo
makubwa sana .
Dk. Shein pia, aliwapongeza wagombea
wenziwe wote 13 wa kiti cha Urais wa Zanzibar na kueleza kuwa wamejitokeza na
wameamua na hatimae kuonesha uwezo wao hukua akieleza kuwa atatumia uzoefu,
uwezo alionao katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi.
Dk. Shein pia alikutumia fursa hiyo kutoa
pongezi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia ulinzi na usalama katika
kipindi chake chote cha uongozi wake sambamba na wakati wote wa uchaguzi wa
Zanzibar.
Sambamba na hayo, alitoa pongezi kwa
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama hapa nchini Mhe. John Pombe
Magufuli kwa kusimamia amani na utulivu kwani aliahidi hilo na ametekeleza
kwani kauli yake alikuwa thabiti.
Alisema kuwa amani itaendelea kudumishwa
na hatakuwa tayari amani iliyopo ivunjwe kwani Zanzibar inasifika kwa amani
iliyonayo, jina lake, historia yake na kwa hivi sasa inahitaji maendeleo ya
haraka haraka.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliahidi
maendeleo ya haraka kwa Zanzibar na kusisitiza azma yake ya kuuimarisha uchumi
wa Zanzibar kwa kwa kufikia asilimia 8 hadi 9 kwani lengo ni kupunguza
utegemezi kutoka kwa wahisani na badala yake Zanzibar itegemee rasilimali zake
ziliopo.
Dk. Shein aliomba mashirikiano sambamba
na kuishi kwa pamoja kwani Wazanzibari wote ni ndugu.
Mapema akitoa maelezo kwa niaba ya
wagombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar,
Mhe. Hamad Rashid aliwaomba wananchi wote wakiwemo viongozi wa kisiasa
kumpa mashirikiano makubwa Dk. Shein katika uongozi wake.
Mhe. Rashid alieleza haja ya kutafutiwa ufumbuzi
changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi hapa Zanzibar huku akieleza kuwa
huu ndio wakati wa kuvijenga vyama vyao sambamba na nchi yao kwa jumla.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment