Habari za Punde

Dk. Shein Aendelea Kusisitiza Amani Kisiwani Pemba.


Na Is-haka Omar, Zanzibar.

Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanziba Dkt.Ali Mohamed Shein amewapongeza Wanachama na viongozi katika wilaya ya Micheweni kwa kukiamini na kukiweka madarakani chama hicho katika
Uchaguzi Mkuu wa Marudio mwaka huu.



Dkt.Shein alisema kwamba ushindi uliopatikana katika uchaguzi huo umetokana na nguvu na nia za dhati za wananchi waliamua kwa pamoja kuichagua CCM kwa kura nyingi ili iendelee kuongoza dola.


Akizungumza  na mamia ya wafuasi wa CCM wakiwemo Mabalozi,wenyeviti na Makatibu wa matawi na maskani za Wilaya ya Micheweni Kichamanhuko katika ukumbi wa Chuo cha Kiislamu Pemba, alisema baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa marudio kwa sasa CCM inaendelea na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili wananchi wapate maendeleo endelevu.

Dkt.Shein alisema serikali ya awamu ya saba itendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza ama kupunguza  changamoto mbali mbali zilizopo katika nyanja za Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inakuwa miongoni mwa nchi yenye uchumi wa kati.

“ Nawapongeza sana wanachama wenzangu wa CCM mlioniamini na kunipatena dhamana ya uongozi nakuahidini kwamba sitowaangusha bali nitaendelea kuwatumikia kama nilivyowahi kuahidi katika mikutano yangu ya Kampeni zilizopita.

Pia nakukumbusheni jambo moja ambalo ni muhimu sana na tunatakiwa kulizingatia ambalo ni kulinda na kutunza amani na utulivu wa nchi yetu, kwani kufanya hivyo ndiyo siri ya mafanikio yetu.” alisisitiza Dkt.Shein na kuongeza kwamba licha ya kuwepo changamoto za kisiasa katika kisiwa cha Pemba bado wafuasi wa CCM wanatakiwa kuwa wavumilivu.

Alisema Zanzibar ili iweze kuvuka katika migogoro na vurugu zisizokuwa za lazima ni lazima iwe na kiongozi wa ngazi ya Urais anayejali utu na ubinadamu wa watu wengine na mwenye maono na uvumilivu mpana wa kisiasa na vigezo ambavyo anavyo yeye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.

Aidha Dkt. Shein amekerwa na kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CUF kwa kuwatenga na kuwagomea wafuasi wa CCM katika shughuli mbali mbali za kijamii kisiwani humo.

Alisema kwamba vitendo vya kuwabagua hadi kufikia hatua ya kuwachomea nyumba za kuishi havionyeshi sifa mbaya tu bali vinaidhalilisha jamii nzima ya Zanzibar na Serikali yake na kujenga taswira mbaya katika nchi zingine duniani.

Akizungumzua vipaumbele vya serikali ya awamu ya saba iliyopo madarakani kwa sasa ni kuimarisha dhana ya utawala bora, uwajibikaji na uwazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na uadilifu katika utekelezaji wa malengo ya serikali.

Alisema katika kuweka mipango na mikakati ya kuelekea Zanzibar kutoka katika kundi la nchi zinazoendelea na kwenda katika nchi zenye uchumi wa kati ni lazima serikali kupambana vikali vita vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma.

Alieleza kwamba baadhi ya ahadi alizotoa katika kampeni za Uchaguzi zilizopita za kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma wa kima cha chini alisema ahadi hiyo imeanza kutekelezwa kwa vitendo.

Kwa upande wa ahadi ya posho la shilingi 20,000 kwa wazee wenye  umri wa kuanzia miaka 70 ambao wamewahi kuwa watumishi wa umma ama hawakufanya kazi serikalini nalo limeanza kutekelezwa kwa baadhi ya maeneo ambayo taratibu zake zimekamilika.

Alisema jambo pekee la kulinda hadhi na heshima ya zanzibar ni Amani na utulivu wa kudumu kwani nchi itastawi kimaendeleo endapo hali hiyo itatawala nchini.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema chama hicho kima imani kubwa na kasi ya utendaji wa Dkt.Shein na wataendelea kumuunga mkono ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa miongoni mwa nchi
zilizoimarika kiuchumi katika ukanda wa Afika Mashariki na Kati.

Vuai aliwasihi viongozi mbali mbali waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio kuwa wabunifu katika utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo ili wananchi waendelee kukiunga mkono chama hicho.

Pamoja na hayo, Vuai amewapongeza wanachama wa CCM Pemba kwa ujasiri wao toka kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwaka 1992,wameendelea kuwa waaminifu kwa kukiunga chama hicho bila ya woga.

“ Licha ya vikwazo, vitisho na wakati mgumu wa kutengwa na kunyanyaswa na wapinzani lakini mmeendelea kuwa waaminifu kwa CCM nasi tunakuahidini kwamba tutakuwa nanyi daima katika kusimamia na kulinda
hadhi ya CCM.”, alifafanua Vuai.

Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema CCM ni chama kilichotokana na vyama vikuu vya ukombozi kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara hivyo kina historia na asili ya amani kwa miaka mingi na kinaendelea kusimamia utu na maisha ya watu kwa misingi ya haki na uadilifu.

Aidha aliwasihi wananchi wa Pemba hasa wafuasi wa CCM kuendelea kuwa watulivu wenye subira juu ya changamoto za kisiasa wanazokumbana nazo huku wakisubiri serikali na chama kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kutatua changamoto hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.