Habari za Punde

Maandalizi ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania 2016/2017 Yaanza Rasmi.


Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Fatuma Mrisho akielezea umuhimu wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 katika mkutano wa wadau wa utafiti huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Utafiti huo utafanyika nchi nzima kuanzia mwezi Agosti, 2016.
Mkurugenzi Mkazi wa ICAP Tanzania Dkt. Fernando Morales akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Utafiti huo utafanyika nchi nzima kuanzia mwezi Agosti, 2016.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria Mkutano wa Wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa (hayupo pichani) katika Mkutano wa Wadau wa Utafiti huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Utafiti huo utafanyika nchi nzima kuanzia mwezi Agosti, 2016. (PICHA NA EMMANUEL GHULA).
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa akihojiwa na waandishi wa habari katika mkutano wa wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Utafiti huo utafanyika nchi nzima kuanzia mwezi Agosti, 2016.(Picha na Emmanuel Ghula)

Na Veronica Kazimoto                                                                                      

Wito umetolewa kwa wadau pamoja na wananchi ili kushiriki kikamilifu katika kuwezesha upatikanaji wa takwimu rasmi nchini.                                                
Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 uliofanyika leo jijini Dar es Salaam,  Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wana mchango mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa takwimu rasmi nchini.

“Leo hii tumekutana na wadau mbalimbali wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu kwa ajili ya kujadili na kushauriana namna ya kufanya utafiti huu kwa ufanisi ili kupata takwimu bora zitakazosaidia katika kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo nchini”, amesema Dkt. Chuwa.


Dkt. Chuwa amefafanua kuwa utafiti huu unategemea sana ushiriki wa wananchi kwani wao ndio wadau na wahusika wakuu ambao wanapaswa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu rasmi zitakazosaidia Taifa katika kuboresha huduma za afya kwa manufaa ya watanzania wote.

Dkt. Chuwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu ipo katika harakati za kukamilisha maandalizi ya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania 2016/2017 ambao utaanza kufanyika nchi nzima kuanzia mwezi Juni mwaka huu. 

Aidha Dkt. Chuwa  amesema utafiti huu ni wa kipekee ukilinganishwa na tafiti zilizotangulia kutokana na kuongezeka kwa viashiria vitakavyo chunguzwa ikiwemo kuangalia kiwango cha CD4, kiwango cha maambukizi mpya, upatiakanaji wa huduma zinazohusiana na UKIMWI pamoja na kupima watoto wadogo wenye umri chini ya mwaka mmoja.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa utafiti huu kutasaidia Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini hasa katika kupambana na maambukizi mapya ya UKIMWI na namna ya kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa ICAP nchini, Dkt. Fernando Morales amesema utafiti huu ni wa muhimu katika kupima viashiria na matokeo ya UKIMWI kwa nchi ambazo zimekuwa zikipata msaada wa kupambana na UKIMWI kutoka Serikali ya Marekani.

“Lengo la Utafiti huu ni kupata viashiria ambavyo vinasababisha maambukizi mapya pamoja na kupima jinsi gani Taifa limeweza kupambana na ugonjwa wa UKIMWI nchini”, amesema Dkt. Morales. 

Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 unafanyika katika nchi Ishirini (20) Afrika ambapo kwa sasa nchi nane (8) zinaendelea na utafiti huu zikiwemo Zimbabwe, Zambia, Malawi, , Lesotho, Swaziland, Uganda, Namibia na Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.