Habari za Punde

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Atekeleza Ahadi Katika Jimbo Lake.

Na Othman Khamis OMPR.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba utulivu wa mwanafunzi wa kupata taaluma akiwa katika mazingira ya kukaa chini kamwe hautamuwezesha mwanafunzi husika kupata mafanikio yanayohitajiwa kielimu kitaifa na kimataifa.

Alisema juhudi za pamoja kati ya Wizara husika inayosimamia Elimu, Kamati za Maskuli, Waalimu pamoja na Wanafunzi wenyewe ndizo zitakazotoa muangaza utakaowapa fursa nzuri wanafunzi hao maskulini kusoma katika mazingira bora yanayostahiki.

Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi mifuko mia Moja ya Saruji na Fedha Taslim Shilingi Milioni 5,000,000/- za mafundi kwa ajili ya matengenezo makubwa ya jengo moja la Skuli ya Msingi Mahonda lilioko katika mazingira mabovu ya kutoa huduma kwa wanafunzi.

Balozi Seif  alikuwa akitekeleza ahadi aliyoitoa wiki moja iliyopita wakati wa ziara yake ya kukabidhi msaada wa Kompyuta kwa skuli ya Sekondari ya Mahonda ambapo amejitolea kushirikiana na washirika wa Maendeleo katika kuona changamoto zinazoikabili Skuli ya msingi na Sekondari ya Mahonda zinapatiwa ufumbuzi kadri ya hali ya uwezeshaji itakavyoruhusu.


Alisema hali ya mazingira ya baadhi ya Maskuli ikiwemo majengo, vikalio na hata vifaa vya maabara na Maktaba sambamba na Walimu bora lazima yaimarishwe ili kumuwezesha Mwanafunzi kupata Taaluma kwa utulivu zaidi.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliuhakikishia Uongozi wa Kamati ya Skuli, Walimu pamoja na Wanafunzi wa Skuli hiyo kwamba Uongozi wa Jimbo hilo utaandaa utaratibu maalum utakaowezesha kupatikana kwa vikalio kwa wanafunzi wa Skuli ya Msingi.

Aliendelea kusisitiza kauli yake aliyoitoa wiki iliyopita kwamba hatua ya awali itakayochukuliwa na Uongozi wa Jimbo hilo itahusisha vikalio mia moja kati ya mahitaji halisi ya vikalio 300 tatizo ambalo limekuwa likiziathiri pia skuli nyingi za hapa Zanzibar.

Balozi Seif aliwaasa Wanafunzi wa Kike kujitahidi kusoma kwa bidii wakilenga kujijengea mazingira bora ya ajira wakati wa maisha yao ya baadae ili kuondokana na utegemezi unaowasababishia kukumbana na udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia.

Alisema kutokana na mabadiliko ya dunia yaliyopo kwa sasa Mwanamke tayari ana fursa mbali mbali zinazomuwezesha kujiimarisha kimaisha ili aondokane na dhana ya uwepo wa mfumo dume unaofinya fursa zao katika nafasi mbali mbali zikiwemo zile za maamuzi.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pemba Juma ameushukuru mwanzo mzuri wa Baadhi ya Viongozi wa Majimbo hapa Nchini waliyoonyesha juhudi za awali za kuiunga mkono Wizara hiyo katika kuwajengea mazingira mazuri ya Kielimu Wanafunzi.

Mh. Riziki alisema Elimu bora kwa Mwafunzi wa Taifa hili inawezekana kabisa iwapo kila mwana Jamii atakuwa tayari kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha mazingira mazuri ya kumjengea mwanafunzi apate Elimu katika misingi inayotakiwa.

Naye Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi akisalimiana na wanafunzi hao wa skuli ya Msingi Mahonda alisema Skuli nyingi Nchini bado zina mahitaji mengi yanayowajibika kushughulikiwa kwa nguvu za pamoja.

Mama Asha alisema nguvu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa sasa  katika kuyashughulikia mahitaji hayo ni ndogo kiasi kwamba Wananchi wenyewe na washirika wa maendeleo ndio watakaokuwa `jibu sahihi la kuyatafutia ufumbuzi mahitaji hayo muhimu.

Mke huyo wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliwaahidi Walimu na Wanafunzi hao wa Skuli ya Msingi Mahonda kwamba tatizo linalowakabili wanafunzi hao la ukosefu wa vikalio litapatiwa ufumbuzi ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.

Alisema Skuli ya Mahonda iliyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja itakuwa ya mfano na kurejea kuwa Skuli bora na yenye hadhi kulingana na Historia yake tokea ilipoasisiwa Mwaka 1964 na kufunguliwa rasmi Tarehe 21/3/1967 ikianza na Madarasa Matatu na Wanafunzi 100.

Matengenezo makubwa ya jengo hilo la Madarasa Manne ya Skuli ya Msingi Mahonda linalotarajiwa kurejeshwa katika hadhi yake ya asili yanatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 13,000,000/- zitakazotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.