Habari za Punde

Ujumbe wa CCM Tawi la Makangira, Kinondoni wafanya ziara ya ujirani mwema Zanzibar

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Ujumbe Viongozi wa CCM Tawi la Makangira Kata ya Msasani, Wilaya ya Kinondoni Mjini Dar es salaam katika Banadari ya Malindi baada ya kumaliza ziara yao ya ujirani mwema Visiwani Zanzibar wakiwa wenyeji wa Tawi la CCM Vikokotoni Mjini Zanzibar.
 Katibu wa CCM Tawi la Makangira Kata ya Msasani Nd. Epi Fania Ngonyani akibadilishana mawazo na Balozi Seif akijiandaa na ujumbe wake kuondoka Bandarini Malindi kurejea Mjini Dar es salaam baada ya kumaliza ziara yao ya ujirani mwema.

Nyuma ya Ndugu Ngonyaji ni Mwenyekiti wa CCM wa Tawi hilo Ndugu Haroub Othman Mberwa.
 Balozi Seif akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM Tawi la Makangira Ndugu Haroub Othman Mberwa aliyeuongoza ujumbe wa Viongozi kumi wa Kata hiyo waliofanya ziara ya ujirani mwema hapa Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa Matawi mbali mbali Nchini Tanzania wanapaswa kuwa makini katika kuwachangua viongozi imara wakati utakapowadia wa chaguzi za Chama hicho ili kuirahisisha kazi ya ushindi CCM mwaka 2020.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Tawi la Makangira Kata ya Msasani Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam Ndugu Haroub Othman Mberwa wakati akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi hapo Bandarini Malindi Mjini Zanzibar.


Mwenyekiti Mberwa na Ujumbe wake wa Viongozi Kumi wa Kata ya Makangira Msasani ulikuwepo Zanzibar kwa ziara ya kuimarisha uhusiano mwema kati ya kata hiyo na wenyeji wao wa Tawi la CCM Vikokotoni lilioko Mji Mkongwe Zanzibar.

Ndugu Mberwa alisema wakati umefika kwa wana CCM kuendelea kuongozwa na Viongozi makini waliobobea hekima na busara kuanzia Matawi maeneo ambayo ni chimbuko halisi la upatikanaji wa Viongozi katika ngazi za Majimbo, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.

Alisema Chama cha Mapinduzi kimepata misukosuko mingi katika awamu tofauti za Uongozi zilizopita iliyosababishwa na baadhi ya Viongozi wenye sura mbili za maamuzi jambo ambalo lilipelekea kuwa na mgawanyiko na hatimae kuzalisha makundi yaliyozaa ufa ndani ya chama hicho.

Ndugu Mberwa alitahadharisha kwamba Wanachama wa CCM Matawini ndio wenye kauli na rungu za kuwachagua Viongozi watakaokuwa tayari kuwatumikia katika misingi ya uadilifu na ni vyema kuachana na tabia ya kubebana kwa kisingizio cha ukabila, uzawa na urafiki.

Alieleza kwamba tabia kama hizo ndizo zinazopelekea Viongozi wa Kitaifa kukumbana na wakati mgumu katika kutoa maamuzi ya hatma ya muelekeo wa kumpata Kiongozi wa kubeba dhamana ya kuwatumikia katika masuala yao ya Chama.

Naye Katibu wa Tawi la CCM la Makangira Kata ya Msasani, Wilaya ya Kiondoni Mkoa wa Dar es salaam Nd. Epi Fania Ngonyani alisema uwepo wa ujumbe wao hapa Zanzibar umejifunza mambo mengi yatakayosaidia kuimarisha chama chao kwa upande wa Tanzania Bara.

Nd. Ngonyani alisema matembezi ya sehemu za kihistoria pamoja na Mikutano ya hadhara ya kukutana na wanachama wenzao wa baadhi ya Matawi na hata Wilaya za Tanzania Zanzibar imewajengea heshima na upendo kati yao na wenyeji wao iliyopelekea pia kujadili mapungufu yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Alieleza kwamba katika mikutano hiyo ya uhusiano mwema pande hizo mbili zilipendekeza uwepo wa mikakati ya makusudi ya kujengewa uwezo zaidi wa uwezeshaji makundi makubwa ya vijana na wanawake ili washiriki vyema kwenye shughuli za uzalishaji.

Ziara hizo za kuimarisha uhusiano mwema kati  ya Matawi ya Chama cha Mapinduzi ya Vikokotoni Mjini Zanzibar na Makangira Msasani Dar es salaam hufanyika kwa kutembeleana kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.