Habari za Punde

Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini akutana na Dk Shein Ikulu

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe,Song Geum-Young alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa mazungumzo,[Picha na Ikulu.] 27/06/2016.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe,Song Geum-Young alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kumsalimia Rais,[Picha na Ikulu.] 27/06/2016.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe,Song Geum-Young alipofika Ikulu Mjini Zanzibar baada  mazungumzo yao,[Picha na Ikulu.] 27/06/2016.


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                       27 Juni, 2016
---

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Korea                              Mhe Song Geum-Young na kuzungumzia masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein na balozi Young walisifu jitihada za serikal
i za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea za kuimarisha uhusiano huo tangu nchi mbili hizo zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia miaka ya tisini.

“Tumefanya jitihada kubwa za kuimarisha uhusiano wetu na matokeo yake sasa nchi zetu zinashirikiana kwa karibu katika mambo mbalimbali katika nyanja za kidiplomasia, uchumi na maendeleo” Dk. Shein alimueleza Balozi huyo.

Alifafanua kuwa ushirikiano katika biashara na uwekezaji, elimu, afya na  kilimo ambayo ni kati ya maeneo yaliyowekewa mkazo katika ushirikiano ni maeneo muhimu kwa kuwa yanasaidia jitihada za kupunguza kiwango cha umasikini hivyo kujenga ustawi wa wananchi.


Dk. Shein alibainisha kuwa chini ya uhusiano huo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar ikiwemo imekuwa ikifaidika na misaada mbalimbali ambayo imekuwa chachu katika kuongeza kasi ya jitihada za wananchi wa Tanzania kujiletea maendeleo.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliishukuru Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Korea kwa misaada yake kwa Serikali na watu wa Zanzibar  na kuutaja mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji kuwa moja ya matokeo makubwa ya ushirikiamo kati ya nchi hiyo na Zanzibar.

“Kupitia mradi huu wa umwagiliaji, tunatarajia kutimiza lengo letu la muda mrefu la kujitegemea kwa chakula hivyo ni habari njema kwetu kuwa taratibu za kuanza utekelezaji wa mradi huu zitakamilika hivi karibuni” Dk. Shein alieleza.

Pamoja na mradi wa kilimo cha umwagiliaji, Jamhuri ya Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (KOICA) inaisaidia pia Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO) mradi wa ufugaji wa samaki wenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 3.4.

Dk. Shein alitambua mchango wa shirika la kazi za kijamii la Korea la SAEMAUL ambalo alisema limekuwa likifanya kazi nzuri za kusaidia maendeleo ya jamii katika maeneo ya vijijini hapa Zanzibar.

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Korea alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake inaupa kipaumbele uhusiano wake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ingependa kuona unaimarika siku hadi siku.

Alifafanua kuwa ujumbe maalum wa nchi hiyo utakuja tena nchini mwezi Julai 2016 kwa mazungumzo zaidi ya ushirikiano baada ya mkutano kama huo wa ushirikiano uliofanyika mwezi Aprili mwaka huu.

Balozi Young alieleza kufurahishwa kwake kuona zaidi ya vijana 80 wa kujitolea wa Kikorea wanashiriki hutoa huduma za kijamii katika sehemu mbalimbali za Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Alieleza kitendo hicho kuwa ni kilelezo kingine cha kuonesha na kuimarisha urafiki mzuri uliopo kati ya nchi yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mkutano huo Balozi Young alimhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza miradi yake ya maendeleo.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.