Habari za Punde

Balozi Seif Afungua Semina ya Uchimbaji wa Mafuta na Kutembelea Ukumbi wa Maandalizi ya Baraza la Eid Firty

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifungua Semina  juu ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyofanyika katika ukumbi wa juu wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni.Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Mh. Salama Aboud Talib  na wa Pili kutoka Kulia ni Mwakilishi wa Kampuni ya Utafiti wa Mafuta na Gesi asilia ya Rakgas kutoka  Nchini Ras Al – Khaimah Bwana Kamal Ataya.
Mtaalamu wa utafiti na uchimbaji mafuta na gesi kutoka Kampuni ya Rakgas ya Nchini Ras Al – Khaimah Bwana Osama Abdel akityoa mada kwenye semina ya mafuta na gesi ilitotolewa kwa wawakilishi wa Zanzibar.
Haiba ya ndani inavyoonekana ya Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar ukiwa katika matengenezo makubwa ili utoe huduma za kisasa.
Mrakibu Msaidizi wa Mafunzo { ASP } Juma Makame wa Pili kutoka kulia mwenye shati la drafti akimpatia maelezo Balozi Seif  aliyepo kati kati juu ya harakati za kukamilika kwa matengenezo makubwa ya Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi hapo Kikwajuni Mjini Zanzibar. Wa kwanza kutoka Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza, wa kwanza kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Nd. Omar Hassan na nyuma ya ASP Juma Makame ni Msimamizi wa ujenzi kutoka KMKM LCDR Hamad Masoud Khamis.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais w Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza akimueleza Balozi Seif hatua zinazofanywa za kuimarisha eneo la nje ya Ukumbi huo.
(Picha na – OMPR)

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alisema ugunduzi wa Rasilmali ya mafuta na Gesi asilia kwa kiwango cha Kibiashara pamoja na usimamizi wake mzuri unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi na kuboresha hali ya maisha ya Wananchi.

Hata hivyo alisema rasilmali hizo zinaweza kuleta balaa endapo hazitasimamiwa vizuri na uadilifu wa hali ya juu ambapo matokeo yake kuibuka mizozo isiyokwisha na hatimae kuzaa umaskini kwa Wananchi walio wengi.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo kwenye semina ya siku moja juu ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyofanyika katika ukumbi wa juu wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema uzoefu unaonyesha wazi kwa nchi nyingi zinazoendelea kiuchumi hasa zilizomo ndani ya Bara la Afrika, ugunduzi wa nishati ya mafuta na gesi asilia umechangia kuzitumbukiza katika vita nchi zilizobarikiwa kupata neema hizo na kuviza ndoto za Wananchi wake kujikomboa kiuchumi.

Balozi Seif alisema Zanzibar ikijiandaa kuingia katika harakati za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ina nafasi nzuri ya kujifunza kutoka kwa nchi zilizofanikiwa vyema katika miradi hiyo kutokana na usimamizi makini.

“Bila shaka umakini wetu ndio utakaoiepusha Zanzibar na balaa inayoletwa na  miradi ya mafuta na gesi asilia. Sina shaka ye yote ile kutokana na umakini huo ulioanza ambao hautoitumbukiza Nchi yetu katika mizozo kama zilivyo nchi nyengine tunazendelea kuzishuhudia ”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kufanyika katika mazingira ya uwazi na uwajibikaji.

Aidha Balozi Seif alieleza kwamba Serikali pia imekusudia kuweka wazi Taarifa zake zote kwa vyombo vya Habari ili kila Mwananchi wa Taifa hili apate fursa ya kuelewa nini kinaendelea katika sekta hiyo ya nishati.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisitiza kwamba pale nishati za mafuta na gesi asilia zitakapogunduliwa katika kiwango cha kibiashara Serikali Kuu itashirikiana na vyombo vya Kimataifa vinavyosaidia kujenga misingi ya uwazi na umiliki ili nishati hizo zileta tija kwa Wananchi.

Aliishukuru na kuipongeza Kampuni ya utafiti wa mafuta na gesi asilia ya Nchini Ras al –Khaimah { RAKGAS } kwa uamuzi wao kuandaa semina hiyo kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao ndio wawakilishi wa Wananchi Majimboni.

Alisema Mafunzo yaliyomo ndani ya Semina hiyo yaliyokuja kwa wakati muwafaka yatawapa fursa pana Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kujenga uelewa mpana zaidi kuhusu nishati ya mafuta na geshi asilia.

Mapema Mwakilishi wa Kampuni ya Utafiti wa Mafuta na Gesi asilia ya Rakgas kutoka  Nchini Ras Al – Khaimah ambae pia ni Mshauri wa Mfalme wa Nchi hiyo katika masuala ya Mafuta Bwana Kamal Ataya amepongeza ushirikiano wa muda mrefu ulipo kati ya Zanzibar na Ras Al – Khaimah.

Bwana Kamal alisema  yapo matarajio makubwa  kwa Zanzibar  kutengemana katika uchumi wake kutokana na dalili zinazoonyesha uwepo wa rasilmali ya Mafuta na Gesi katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema Serikali ya Mamlaka ya Rais Al – Khaimah imejitolea kwa nguvu zote  kuunga mkono jitihada za Zanzibar za kutafiti rasilmali ya Mafuta na Gesi  na hatiae uchimbaji utakaosaidia kustawisha maisha ya Wazanzibari wote.

Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Semina hiyo Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Mh. Salama Aboud Talib ameipongeza Serikali ya Ras Al – Khaimah kwa kusaidia miradi ya maendeleo na Kijamii Zanzibar.

Waziri Salama alisema Taifa hilo la Bara la Kiarabu tayari limeshafadhili ujenzi wa visima vya maji safi na salama vipatavyo 150 Unguja na Pemba na kuwapunguzia ukali za changamoto ya maji Wananchi walio wengi hapa Zanzibar.

Mhe.Salama alielezea faraja yake kutokana na msaada huo uliokwenda sambamba na Nchi hiyo kusaidia miradi ya Sekta ya Afya pamoja na kufadhili nafasi za masomo ya elimu ya Juu Nje ya Nchi kwa wanafunzi wa Zanzibar.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamejadili Mada Nne zilizowasilishwa kwenye Semina juu ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi ambazo ni pamoja na mafuta na gesi, ushirkiano na majukumu, Leseni ya Zanzibar na Pemba   pamoja na Matayarisho ya Mkataba wa Mafuta na Gesi.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya matengenezo makubwa ya Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Ukumbi huo wa asili utatumika kwa ajili ya sherehe za Baraza la Iddi el Fitri zinazotarajiwa kufanyika Wiki Moja na Nusu ijayo baada ya kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaoendelea hivi sasa.

Matengenezo makubwa ya ukumbi huo yanafanywa kwa pamoja na Timu ya Wakandarasi wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya usimamizi wa Mkuu wa Ufundi wa Chuo cha Mafunzo Msaidizi Mrakibu wa Mafunzo ASP Juma Makame na LCDR Hamadi Masoudi Khamis.

Akitoa maelezo ya maendeleo ya matengenezo ya Ukumbi huo Mrakibu Msaidizi wa Mafunzo ASP Juma Makame alimueleza Balozi Seif  kwamba matengenezo hayo yatakamilika rasmi ifikapo mwezi 25 Ramadhan na kutoa fursa ya kutumiwa na Serikali kama ilivyokusudiwa.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseh Abdulla Meza alisema harakati za matengenezo ya Ukumbi huo zimekwenda sambamba na kulifanyia matengenezo eneo la nje katika kiwango cha Lami  ili kuweka haiba nzuri ya eneo hilo.

Alisema kazi hiyo inafanywa na wahandisi Wazalendo wa Idara ya Utunzaji na Utengenezaji wa Bara bara Zanzibar { UUB }.

Akitoa shukrani zake kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wahandisi hao wazalendo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi y Zanzibar itazingatia namna ya baadaye ya matumizi ya Ukumbi huo baada ya kumalizika kwa sherehe za Baraza la Iddi el –Fitri.

Balozi Seif alisema hatua hiyo itazingatiwa zaidi kwa kina kutokana na Historia ndefu iliyopo ya Ukumbi huo unaofanyiwa matengenezo makubwa kwa kipindi cha takriban cha wiki mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.