Habari za Punde

CCM Zanzibar Yasisitiza Ubunifu katika Uendeshaji wa Miradi Yake.

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
VIONGOZI na Watendaji wa CCM Zanzibar wametakiwa kuendelea kuwa wabunifu katika kuimarisha miradi ya maendeleo ya Chama hicho ili iwe ya kisasa na inayoendana na mazingira ya sasa kiuchumi.

Kimesema miradi hiyo inatakiwa kuimarishwa kwa lengo la kufikia hadhi na thamani ya CCM, hatua itakayotoa fursa ya mapato yanayotokana na rasilimali hizo kuwanufaisha wanachama wengi badala ya watu wachache.


Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vua katika mwendelezo wa ziara yake ya kuhakiki na kukagua mali za chama huko katika Mkoa wa Mjini Kichama Unguja.


Alisema ubunifu ndiyo nyenzo pekee ya kuongeza thamani ya miradi inayoanzishwa kwani itakuwa na miundombinu ya kisasa inayokubalika katika ushindani wa kibiashara.


Alieleza kwamba miradi mbali mbali iliyopo hivi sasa haipo katika mazingira mazuri ya kibiashara hali inayopelekea kupatikana kwa mapato kidogo, chanamoto inayotakiwa kufanyiwa kazi na wahusika kiutendaji.


“Naamini kwamba kama tutatumia rasilimali zetu vizuri kujiimarisha kiuchumi tunaweza kupiga hatua kubwa kiuchumi, kwani maeneo yetu kwa mfana kama tutajenga maduka na kumbi za mikutano za kisasa tunaweza kupata mapato mengi tofauti na yanayopatikana hivi sasa., alisema
Vuai.



Vuai alifafanua kwamba Rasilimali na Miradi ya chama hicho imetokana na nguvu za waasisi na wazee wa Afro Shiraz Party( A.S.P) kabla ya kuzaliwa CCM walionunua rasilimali za kudumu ambazo kwa sasa zinawanufaisha vizazi vya sasa, hivyo na viongozi na watendaji waliopo sasa kwa ngazi mbali mbali ndani ya chama hicho wanatakiwa kuiga mfano
huo.



Alisema CCM ni taasisi ya kisiasa lakini bado inatakiwa kuendelea kuwa na falsafa ya kufanya siasa na uchumi kama sera za chama hicho zinavyoelekeza, hivyo wahusika wanatakiwa kuwa na mipango mizuri ya uendeshaji wa miradi ya chama ili kuepuka marumbano yasiyokuwa ya
lazima ndani ya chama hicho.



“ Kwanza nakupongezeni kwa kuona umuhimu wa kuanzisha miradi lakini tunahitaji kufahamu kwamba suala la kuanzisha ni jambo moja lakini kuienzi na kuiendeleza ni mambo mengine na ya msingi yanayotakiwa kupewa kipaumbele.


Pia katika kuimarisha miradi hii ni lazima tuzingatie suala la uwazi hasa kupeana taarifa sahihi za vyanzo vya mapato na mipango mingine ya maendeleo kupitia vikao halali vya kikanuni ili Wana CCM na viongozi wengine wapate taarifa hatua itakayoepusha malalamikoi na shutuma zisizokuwa za lazima.”., alishauri Vuai na kuongeza kuwa miradi inayohusu fedha inahitaji uwazi na udilifu wa hali ya juu katika uendeshaji wake kwani inagusa maslahi ya umma nasi mtu mmoja.


Alieleza kwamba lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi na mbali mbali za chama ili kubaini changamoto zilizopo katika rasilimali hizo na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa maendeleo ya CCM.


Alisema toka ameanza kufanya ziara hiyo kuna baadhi ya maeneo amebaini kujitokeza kwa vitendo vya udanganyifu na utapeli vinavyofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu wanaohujumu mali za chama hicho kwa makusudi hali ambayo CCM haiwezi kuvumilia na itachukua hatua stahiki
dhidi yao.



Naibu Katibu Mkuu huyo, aliendelea kusisitiza viongozi wote
wanaoendesha miradi ya chama kujiridhisha juu ya mikataba wanayofunga na wawekezaji ama  wafanyabiashara, kuhakikisha inaenda sambamba na sera ya uchumi inayoelekeza miradi yote mikubwa kusimamiwa na Baraza
la Wadhamini la Chama hicho.



Aliongeza kwamba CCM Afisi Kuu Zanzibar ipo tayari kutoa ushauri wa kisheria juu ya umiliki na uendeshaji wa miradi mbali mbali ya Chama kwa nia ya kuziweka mali za CCM katika mazingira salama.


Aidha Vuai aliahidi kuhakikisha Changamoto, maoni na ushauri vilivyojitokeza katika ziara hiyo atahakikisha Afisi yake wanazifanyia kazi kwa haraka ili sehemu husika waweze kupata mrejesho utakaosaidia kusonga mbele kimaendeleo kama utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2015/ 2020 unavyoelekeza.



Nao viongozi wa maeneo yaliyofasnyiwa ziara katika Mkoa huo, wamepongeza hatua ya CCM kukagua miradi yao na kuahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo ushauri na maagizo yote yaliyotolewa na chama hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.