Habari za Punde

Kituo cha Elimu Mbadala Chadhimisha Kuadhishwa Miaka 10 kwa Kufanya Usafi

Na.Maryam Kidiko/ Takdir Ali –Maelezo Zanzibar.

Jamii imetakiwa kujijengea tabia ya kusafisha mazingira mara kwa mara ili kuweka  Mji  safi na kuepuka  maradhi mbali mbali ya mripuko hapa  Nchini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kituo cha Elimu Mbadala na Watu Wazima Bi.Hawa Seif Amour  katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika Jengo la Utangazaji ZBC Radio Rahaleo mjini Zanzibar.

Amesema kuwa usafi huo ni miongoni mwa shamrashamra za kuazimisha kutimiza miaka kumi tokea kuanzishwa Kituo cha Elimu Mbadala na Watu Wazima Raha leo.

Aidha Bi Hawa amesema kufanya usafi wa mazingira ni mwendelezo wa kuetekeleza wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, John Pombe  Magufuli wa kuweka Mazingira ya nchi katika hali ya Usafi na Usalama.

Nae Msaidizi wa Kituo hicho cha Elimu Mbadala na Watu Wazima Rahaleo kazija Mashie Ali amesema suala la usafi lina umuhimu mkubwa hivyo  kila mtu anawajibu wa kusafisha Mazingira yake yaliyomzunguka.

Amesema kuwa wapo tayari kutoa mashirikiano kwa hali na mali katika kufanya usafi kwa lengo la kutunza mazingira na kuhamasisha usafi katika jamii.

Kwa upande wake Sheha wa Raha leo Omar Saidi Juma ameziomba Taasisi zinazohusika na suala la usafi ikiwemo Manispaa na Ujenzi kuweza kuweka sheria ndogo ndogo ili kutumika kwa lengo la kudhibitiwa wale wote wanaoharibu Mazingira.

“Tayari kuna baadhi ya Shehia wameunda Vikundi maalum vya usafi ili kuweza kuimarisha usafi katika Mazingira na Vijana wameweza kujiajiri wenyewe kupitia Vikundi hivyo ” amesema Sheha huyo.

 Sambamba na hayo amesema Wananchi wanamuamko mdogo juu ya suala zima la mazingira hivyo ni muhimu kupewa elimu ili waweze kujuwa umuhimu wa kuweka Mazingira safi.

Sherehe hizo za kutimiza miaka kumi tokea kuanzishwa kwa Kituo cha Elimu Mbadala na Watu Wazima Rahaleo zinaazimishwa tarehe 20 mwezi huu katika Jengo lao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.