Habari za Punde

Mkurugenzi wa Vyama vya Ushirika Awataka Viongozi wa SACCOS Kufuata Wajibu Wao.

Na Miza Kona Maelezo Zanzbar .
Mameneja katika vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) wanapaswa kufanya wajibu wao kwa kufuata muongozo na taratibu ziliopo katika Vyama hivyo.

Hayo yameelezwa leo huko katika Ukumbi wa Kituo cha Elimu Mbadala Rahaleo na Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya Ushirika Khamis Daud Simba wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Mameneja 65 wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kutoka Wilaya zote za Unguja.

Amesema Vyama vya Ushirika vinahitaji uwepo wa uongozi imara na mgawanyiko wa madaraka ili kila mmoja aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Mkurugenzi Simba amesema erikali imedhamiria kuleta mageuzi katika Vyama vya Akiba na Mikopo ili viweze kuwa imara endelevu na vinavyoendeshwa kiujasiriamali hivyo Idara ya Maendeleo ya Ushirika imeandaa mpango wa kuzijengea uwezo Saccos hizo katika ngazi tofauti Unguja na Pemba.

Pia amefahamisha kuwa sera ya Ushirika imetayarishwa ili kuelekeza uendeshaji wa sekta hizo kwa lengo la kuviimarisha vikundi vya Ushirika na kuleta maendeleo nchini.

Aidha amesema Vyama vya Ushirika lazima vitambue kuwa vinawajibu wa kutoa huduma bora ili kila mwanachama aweze kupata faraja na kuwashawishi wengine  kujiunga na vyama vya akiba na mikopo kwa lengo la kujiendeleza kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Amefahamisha kuwa hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu Saccos za Zanzibar zimekusanya na kupata mtaji wa bilioni 6.9.

Mafunzo hayo yametayarishwa kwa kushirikiana na Program ya Miundombinu uongezaji wa Thamani ya Mazao na huduma za Fedha Kijijini ambapo mada mbali mbali zimejadiliwa ikiwemo Uchambuzi wa mikopo, Uhasibu na Utayarishaji wa Taarifa za Fedha pamoja na Ukuaji wa Data za Saccos.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.