Habari za Punde

Tumeaza Utekelezaji wa Elimu Jumuishi - Tanzania.

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza jambo  na Waziri Mkuu wa  Norway, Mhe. Erna Solberg wakati wa  majadiliano kuhusu  utekelezaji wa  Lengo Namba Nne la Maendeleo  Endelevu kuhusu Elimu
Sehemu wa Washiriki wa Majadiliano hayo ambayo yalijikita zaidi katika kuhakisha ni kwa namna gani serikali zinatekeleza  utoaji wa elimu  jumuishi ,  nyenye  kiwango bora  pasipo kumwacha yeyote nyuma, changamoto zake na nini kifanyike.

Na  Mwandishi Maalum
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  imeanza kwa namna moja ama nyingine utekelezaji wa lengo namba Nne la Maendeleo Endelevu kuhusuElimu la Maendeleo Endelevu (SDG4) kwa kutoa elimu   bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ikiwa ni pamoja na kuifanya jumuishi kwa makundi yote ya jamii wakiwamo walemavu wa aina mbali mbali.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  katika Umoja wa Matifa, BaloziTuvako Manongi wakati wa majadiliano kuhusu utekelezaji wa lengo namba Nne ambalo ni kati ya Malengo 17  ya Maendeleo Endelevu, maarufu kama agenda 2030 yaliyopitishwa mwezi septemba mwaka jana na viongozi wakuu wa nchi na serikali.

Balozi Manongi alikuwa ni mmoja wa wazungumzaji wakuu katika majadiliano hayo, ambayo yalimhusisha pia Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Erna Solberg na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bi. Irina Bakova na yaliandaliwa kwa ushirikiano wa UNESCO na  UNICEF kama sehemu ya Mkutano wa Kilele wa Kisiasa wa Baraza   la Uchumi la Umoja wa Mataifa (ECOSOC) unaoendelea hapa Umoja wa Mataifa.


SGD4  pamoja na mambo mengine inatilia mkazo na kutoa kipaumbele cha pekee katika utoaji na upatikanaji wa elimu ambayo ni jumuishi, yenye ubora na inayowafikia makundi yote ya jamii, hususani watoto, wanawake na walemavu.

Akielezea namna Tanzania ilivyojipanga katika utekelezaji wa  SDG4 kwa sasa na kwa baadaye, Balozi Manongi amesema    Tanzania  imejipaga vema kisera, kisheria na kimkakati katika kuhakikisha kwamba kila mtanzania bila kujali ni wa kundi gani anapata fursa ya elimu na si elimu tu bali elimu yenye ubora wa hali ya juu na inayokidhi mahitaji na mazingira ya sasa.

Pamoja na kuainisha  sera na sheria mbali mbali ambazo serikali inazitekeleza katika eneo hilo la  elimu, Balozi Manongi anasema,  kuwa na sera nzuri, sheria nzuri na mikakati mizuri hakuwezi kuwa kigezo pekee cha kufanikisha utekelezaji wa  SDG4.

“Kwa Tanzania  tatizo siyo sera, sheria au  mipango na mikakati, tatizo ni raslimali fedha ya kutosha (bajeti) itakayowezesha utekelezaji wa SDG4 na malengo mengine kwa ukamilifu unaotakiwa”.Anasema Balozi

Kutokana na changamato hiyo ya ufinyu wa raslimali fedha,  Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa anasisitiza haja na umuhimu wa ushirikiano wa karibu baina ya Serikali Kuu,  Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kwa lengo la kuhakikisha kwamba hakuna yeyote atakayeachwa nyuma.

Akizungumzia zaidi utekelezaji wa  SGD4 achia mbali utoaji wa elimu  bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari, na kuhakikisha elimu inawafikia wote, Balozi Manongi amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba hivi karibuni Serikali imetangaza kutenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watu wenye matatizo ya ualibino.
“pamoja na changamoto mbali mbali serikali yangu inajitahidi sana kuyafikia makundi mbali mbali ya jamii,  wawe ni watoto wa kike,  watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ama jamii za wafugaji na wawindaji lakini pia  imekwenda mbali zaidi katika kuhakikisha kwamba jamii yenye mahitaji maalum nayo inafikiwa” akasisitiza Balozi Manongi.

Akizungumzia zaidi kuhusu uamuzi wa Serikali ya awamu yaTano ya kuifanya elimu ya msingi hadi Sekondari kuwa bure.  

Balozi amewaeleza wajumbe wa majadiliano hayo kwamba, maana ya uamuzi huo ni kuwa mtoto wa kitanzania atafaidika na elimu ya bure kwa miaka kumi na moja. Na vile vile Tanzania  inakuwa sehemu ya utekelezaji wa baadhi ya kipengele  cha SDG4 kinachopendekeza utoaji wa elimu  bure ili iwafikie watu wengi zaidi.

Washiriki wengine katika majadiliano hayo walikuwa ni Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Korea Balozi Oh Joon ambaye pia ni Rais wa ECOSOC, Waziri wa Elimu kutoka Bolivia Bw.Roberto Iván Aguilar Gómez, Bw.Guy Ryder, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO)  Mwakilishi wa Kudumu wa Ufalme wa Moroco katika Umoja wa Mataifa, Balozi Omar Hilale, Bi. Alice Albright kutoka Global Partnership for Education (GPE),BiSilvia Montoya, kutokaTasisi yaTakwimu ya  UNESCO na Bi. Josephine Bourne kutoka UNCEF.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.