Habari za Punde

Utumishi wa Watoto Bado ni Tatizo Nchini.

                                                   
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014 katika uzinduzi wa matokeo hayo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
 Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Dkt. Abdallah Possi akionyesha Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014. Uzinduzi huu umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango.


Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani nchini Tanzania, Azfar Khan akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014. (Picha na Emmanuel Ghula)
Na Veronica Kazimoto.                                                                                                       
UTUMIKISHWAJI wa Watoto bado ni tatizo kubwa nchini ambapo kati ya watoto watatu wenye umri wa miaka 5 - 17, mtoto mmoja anafanya kazi ambazo ni hatarishi katika maisha yake kiafya, kimwili na kisaikolojia.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Dkt. Abdallah Possi wakati wa uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014 uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam.


Matokeo ya Utafiti huo yameonyesha kuwa, kati ya watoto milioni 15 wenye umri kati ya miaka 5 – 17, watoto milioni 4.2 sawa na asilimia 28.8 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi.

Matokeo haya yameonesha kuwa hali ya utumikishwaji wa watoto umepungua kutoka asilimia 31.1 kwa mwaka 2006 hadi asilimia 28.8 kwa mwaka 2014.  

“Kutokana na matokeo ya utafiti huu, ni dhahiri kwamba, utumikishwaji wa watoto bado ni tatizo kubwa nchini na duniani kwa ujumla. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), asilimia 11 ya watoto wote duniani sawa na watoto milioni 264 wenye umri wa miaka 5 – 17 wanatumikishwa kwenye ajira za aina mbalimbali,” amesema Dkt. Possi.

Dkt. Possi amesisitiza kuwa ni wajibu wa jamii kuwekeza katika elimu kwa watoto kwa ajili ya kupunguza tatizo la utumikishwaji wa watoto ambao unakwenda kinyume na haki zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema utafiti huu umebainisha kuwa, watoto wanafanya kazi zaidi katika sekta za Kilimo, Misitu na Uvuvi ambazo zinaajiri asilimia 92.1 ya watoto wote wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi.

Dkt. Chuwa ameongeza kuwa watoto hutumia zaidi ya nusu ya muda wao sawa na asilimia 58.8 kwa siku nzima kujihudumia na kufanya usafi binafsi ambapo wasichana wameonekana kutumia asilimia 59.2 na wavulana hutumia asilimia 58.3 kujihudumia.

Aidha, shughuli za kujisomea kwa watoto ni asilimia 15.5 ambapo wavulana wanatumia muda mrefu zaidi kujisomea kwa asilimia 16.4 na wasichana hutumia asilimia 14.6 kujisomea.

Utafiti huu umebainisha viashiria vya hali ya watoto wanaofanya kazi za kiuchumi na zisizo za kiuchumi, hali ya utumikishwaji wa watoto pamoja na athari mbalimbali ambazo watoto wanapata kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi. 

Matokeo yameonesha pia, utumikishwaji ni mkubwa kwa watoto wasiosoma ikilinganishwa na watoto wanaosoma. Aidha, matokeo yameonesha utumishwaji ni mkubwa katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mjini.

Utafiti huu wa Utumikishwaji wa watoto wa mwaka 2014 ni wa tatu kufanyika nchini ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2001 na wa pili ulifanyika mwaka 2006.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.