Habari za Punde

Vijana Mali Iko Shambani

Imeandaliwa na George Binagi-GB Pazzo ambae ni Mwanahabari, Blogger na Mkulima (pichani).

Nimekaa nikatafakari sana kuhusu lile shairi liitwalo "Karudi Baba Mmoja" ambalo kwa wale waliosoma miaka iliyopita watakuwa wanalikumbuka shairi hilo ambalo tuliliimba tukiwa darasa la tatu.

Shairi linaeleza namna baba mmoja aliekuwa na watoto wawili alivyowasihi watoto wake ya kwamba mali iko shambani na si vinginevyo kama ambavyo wao walikuwa wakidhania.

Nikakumbuka utitiri wa vijana waliokimbilia mijini kusaka ajira na kuacha ardhi iliyojaa utajiri vijijini. Nikakumbuka namna baadhi ya vijana wanapiga hatua kimaendeleo baada ya kutambua kilimo kinalipa.


Ila nikakatishwa tamaa na changamoto za kilimo. Pembejeo hakuna. Bado wakulima kupangiwa bei ya mazao yao na sehemu ya kuyauza ni kero nyingine. Ila nikajipa moyo na kusema yote yatakwisha ikiwa wakulima tutaendelea kupaza sauti zetu kwa pamoja.

Changamoto ni nyingi katika kilimo ikiwemo ukosefu wa pembejeo na wataalamu wa kutosha kwani hata wachache waliopo baadhi yao bado wameng'ang'ania mijini na hivyo wakulima kushindwa kulima kilimo cha kisasa ambacho kwa sasa kina faida maradufu.

Lakini bado pamoja na changamoto hizo na nyingine nyingi, bado faida ni nyingi katika kilimo kuliko changamoto hivyo nikaona nitumie fursa hii kuwashauri vijana wenzangu kwamba tusikimbilie mijini kama bado hatujajua ama hatuna mipango thabiti inayotupeleka mijini maana mali na utajiri ziko vijijini kupitia kilimo.

Nikasema serikali nayo kupitia wizara ya kilimo ni vyema ikaboresha sekta ya kilimo ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo pamoja na wataalamu ili sekta hii iweze kuwa na mchango chanya kwa taifa ikiwemo kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.
Pamoja na kwamba mimi ni mwanahabari, pia ni mkulima na hapa ni baada ya maandalizi ya shamba lililopo Kata ya Kenyamanyori Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kupanda mahindi.

Tujikumbushe shairi la "Karudi Baba Mmoja".
1. Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali, Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili, Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali, Wakataka na kauli iwafe maishani.

2. Akatamka mgonjwa, ninaumwa kwelikweli, Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali, Roho naona yachinjwa, kifo kimenikabili, Semeni niseme nini, kiwafae maishani.
 3.Yakawatoka kinywani, maneno yenye akili, Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali, Urithi tunatamani, mali yetu ya halali, Sema iko wapi mali, itufae maishani?

4.Baba aliye kufani, akajibu lile swali, Ninakufa maskini, baba yenu sina hali, Neno moja lishikeni, kama mnataka mali, Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

5. Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali, Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili, Akili zetu nyembamba, hazijajua methali, Kama tunataka mali, tutapataje shambani?

6. Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli, Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali, Haya sasa buriani, kifo kimeniwasili, Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

7. Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili, Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili, Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli, Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

8. Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili, Wakakata na shauri, baada ya siku mbili, Wote wakawa tayari, pori nene kukabili, Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

9. Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali, Tangu zile za mibuni, hadi zitupazo wali, Na mvua ikaja chini, wakaona na dalili, Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

10. Shamba wakapalilia, bila kupata ajali, Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali, Wote wakashangilia, wakakumbuka kauli, Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

11. Wakanunua na ng'ombe, majike kwa mafahali, Wakapata na vikombe, mashine na baiskeli, Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali, Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

12. Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali, Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali, Wakakiweka kibao, wakaandika kauli, "KAMA MNATAKA MALI MTAYAPATA SHAMBANI".

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.