STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.08.2016

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikipanga na kutekeelza mikakati mbali mbali
ya kukuza uwekezaji kwa kuweka mazingira mazuri yanayowavutia na kuwashajiisha
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wakiwemo ‘Diaspora”.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Kongamano
la tatu la Diaspora lililofanyika huko katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar
Beach Resort, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Katika hotuba yake
hiyo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali zote mbili zimepanua fursa za uwekezaji
katika sekta ya utalii, biashara, viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi wa bahari
kuu, ujenzi wa nyumba, na sekta nyengine mpya zinazoibuka katika uchumi wa nchi
ikiwemo sekta ya mpya ya gesi na mafuta ambayo kwa Zanzibar inatarajiwa kuimarika
katika miaka michache ijayo.
Dk. Shein aliwataka Wana
“Diaspora” kuendelea kuwa na ujasiri na wawe tayari kuzichangamkia fursa hizo
kama wanavyofanya wana “Diaspora” wa baadhi ya ambazo wameweza kuleta
mabadiliko makubwa katika nchi zao ikiwemo Ghana, Brazil, Ethiopia na Idia.
Katika utekelezaji wa
dhamira ya kuunganisha utalii na uwekezaji, Serikali zote mbili zimekuwa
zikipanga mikakati imara ya kuendeleza miundombinu kwa kuzingatia ukweli kuwa
miundombinu ndiyo daraja bora la kuziunganisha sekta zote za kiuchumi ikiwemo
sekta muhimu ya utalii.
“Nakushaurini mzitumie
fursa zilizopo za kitaalamu katika sekta mbali mbali, nchi yetu inahitaji
wataalamu katika nyanja nyingi hasa katika maeneo mapya ya kiuchumi yanayoibuka
na yale yaliopewa kipaumbele na Serikali zetu hivi sasa”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa kwa upande wa Zanzibar, Serikali imo katika hatua za mwisho za
kutayarisha Sera ya “Diaspora” ambayo itapitishwa wakati wowote kuanzia hivi
sasa ambapo baada ya kukamilika itafafanua na kuweka wazi dira na dhamira za
Serikali katika utekelezaji wa masuala muhimu yanayohusiana na Diaspora.
Alieleza kuwa Sera
hiyo itaelekeza njia bora za kutuma na kupokea fedha pamoja na kuimarisha
misaada ambayo wamekwua wakiitoaa kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya
maendeleo sambamba na kubainisha sheria na wahusika muhimu katika
kuyashughulikia masuala ya “Diaspora”.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliwanasihi Wana “Diaspora”
waendelee kuwa mabalozi wazuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi
wanazoishi pamoja na kuwa mfano wa tabia njema ili waendeleze sifa ya ukaribu,
urafiki na usalama ambayo Tanzania na raia wake wamejijengea na kutambulika
katika mataifa yote duniani.
“Zielezeeni sifa nzuri
za nchi yetu pamoja na watu wake”,alisema Dk. Shein na kuwataka Wana ‘Diaspora”
kuendelea kuishi kwa kuzingatia misingi ya urafiki na udugu huku mkiwa na
mapenzi makubwa baina yao pamoja na nchi yao ya asili.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwataka wana ‘Diaspora’ kuendeleza utamaduni wa kuja kutemebea nyumbani
kila baada ya muda, jambo ambalo ni muhimu na linaimarisha mapenzi baina yao na
ndugu, jamaa na wazazi wao.
Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kuwataka Wana “Diaspora” wakija nyumbani kufanya jitihada
za kuja na watoto wao ili nao wapate fursa za kuyaona mambo mbali mbali ili
waweze kuyathamini mambo ya nchi yao ya asili.
“Jengeeni utamaduni wa
kuja nyumbani mara kwa mara kwa ajili ya kufuatilia mambo yenu na fursa
zilizopo, msipende kuagiza, zingatieni ule usemi maarufu wa lugha yetu kuwa
“kuagiza kufyekeza”, aliongezan Dk. Shein.
Dk. Shein alitoa
shukurani kwa uongozi wa Ofisi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kwa kuandaa Kongamano hilo.
Mapema wakitoa neno la
utangulizi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Dk. Augustine Mahiga
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji
Gavu kwa nyakati tofauti walieleza kuwa Kongamano hilo ni la tatu kufanyika
ambalo la kwanza lilifanyika mwaka 2014 na la pili 2015 yote yalifanyika
Dar-es-Salaam.
Viongozi hao walitoa
shukurani kwa Taasisi za Umma na Taasisi binafsi pamoja na mashirika mbali
mbali ya serikali na yasiokuwa na serikali yaliosaidia kuchangia Kongamano hilo
pamoja na kulidhamini.
Waziri Mahiga alieleza
kuwa Kongamano hilo limelenga katika kuwahamasisha na kuwashajiisha Wana
“Diaspora’ kushiriki katika kuendeleza sekta ya Utalii nchini ikiwa ni njia
mojawapo ya kukuza uwekezaji hapa Tanzania.
Aidha, alieleza kuwa
kauli mbiu ya Kongamano hilo imeamuliwa kuwa ni “Bridging Tanzania Tourism and
Investment: A new Outlook”, yaani Kuiunganisha Sekta ya Utalii na ya Uwekezaji:
Mtazamo Mpya.
Nao Wana “Diapora”
walitoa pongezi zao kwa Serikali zote mbili na kueleza kufarajika kwao na
juhudi za Serikali hizo katika kuwashirikisha katika kupanga mipango ya
maendeleo yao ya nchi yao.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment