HOTUBA YA MHE. BALOZI
AUGUSTINE PHILIP MAHIGA, (MB) WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA
MASHARIKI WAKATI WA KUMKARIBISHA MHE. DKT. ALI MOHAMED SHEIN, RAIS WA ZANZIBAR
NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI WAKATI WA UFUNGUZI WA KONGAMAMO LA TATU LA
DIASPORA (3RD DIASPORA CONFERENCE) ZANZIBAR, 24 AGOSTI, 2016
Mhe.
Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la
Wawakilishi;
Mhe. Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mhe. Issa Haji Ussi Gavu, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar;
Mhe. Said Hassan Said, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Waheshimiwa Wabunge wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu wa Serikali zote mbili;
Waheshimiwa
Mabalozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi;
Wawakilishi
wa Mashirika ya Kimataifa;
Ndugu WanaDiaspora na Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
ASSAALAM
ALEYKUM,
Napenda kuchukua nafasi hii na kutoa shukrani za
dhati kwa Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi kwa kuwa mwenyeji wetu na kukubali kuwa mgeni rasmi katika
kongamano hili la Tatu la Diaspora. Uwepo wako katika Kongamano hili ni ishara
kubwa ya mapenzi ya dhati uliyonayo kwa Diaspora na kutambua umuhimu wa mchango
wao katika kuleta maendeleo ya nchini.
Vilevile, nawashukuru sana waandaji wa Kongamano
hili kwa ujumla wao pamoja na wadhamini
wetu ambao isingekuwa wao tusingeweza kufanikisha shughuli hii. Shukrani za
pekee ziwaendee Kamati ya Mapokezi, kwa mapokezi mazuri tangu tulipowasili hapa
visiwani Zanzibar, ninawashukuru sana na kuwapongeza kwa kazi nzuri.
Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwapa pole kwa
safari ndugu zetu wa Diaspora waliosafiri masafa marefu kutoka kila kona ya
dunia kuja kuhudhuria Kongamano hili
muhimu. Sina shaka mtafurahia ukarimu wa
visiwani na huduma mbalimbali mtakazo zipata katika kipindi chote mtakacho kuwepo
hapa Zanzibar. Karibuni sana mjisikie mko nyumbani maana mtu kwao ndio ngao.
Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilianzisha Idara ya Diaspora mwaka 2010 kwa
lengo la kuwatambua Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuwahamasisha katika kuchangia maendeleo ya nchi kwa kutumia
mitaji, ujuzi na elimu wanayoipata wakiwa nje ya nchi kwa manufaa ya Taifa lao.
Tangu ilipoanzishwa Idara, kumekuwa na jitihada mahsusi za kuwahamasisha
na kuwashirikisha Diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi. Kwa kuanzia,
Wizara yangu imekuwa ikiratibu
makongamano ya Diaspora ndani na nje ya nchi, na hatimaye Kongamano hili la
tatu linalofanyika hapa nchini.
Kwa ufupi lengo la makongamano haya ni kutengeneza mazingira
wezeshi ya kuwakutanisha Diaspora na Taasisi mbalimbali zilizopo nchini ili
kutumia nafasi hiyo kubadilishana mawazo, elimu na ujuzi katika kuleta
maendeleo nchini. Azma hiyo pia inalenga
kuongeza fursa za uwekezaji na kupanua soko la bidhaa la biashara
ndogondogo na za kati ndani na nje ya nchi.
Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana,
Kongamano la Mwaka
huu lina kauli mbiu isemayo ‘Bridging
Tanzania Tourism and Investment : ’A new Outlook :” kwa kiswahili tunasema kiunganishi cha
utalii na uwekezaji: mtizamo mpya ikiwa ni azma ya Serikali kuleta mwonekano
mpya wa kujenga Tanzania yenye matumaini ya uchumi wa kati. Diaspora wakiwa
wadau wa maendeleo wana nafasi kubwa ya
kuimarisha maendeleo ya utalii na sekta ya uwekezaji kwa mustakabali wa
ukuaji wa uchumi wa nchi yetu tukufu ya Tanzania.
Vilevile, Kauli
Mbiu hii imechaguliwa ili kuweka
msisitizo wa jitihada za Serikali katika
kukuza sekta ya utalii na uwekezaji katika uchumi wa nchi, ili kuongeza nafasi za ajira nchini. Tuna imani kuwa Kongamano hili
litakuwa ni chachu ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii na uwekezaji hapa
visiwani kwa kushirikiana na Diaspora wetu katika nchi wanazoishi.
Mhe. Rais,
Ndugu Diaspora,
Nachukua nafasi hii kupongeza ushirikiano na uratibu
mzuri baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar; kupitia Wizara yangu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, pamoja na Ofisi ya Rais –Zanzibar Ushirikiano huo umezaa matunda
mazuri na leo hii tunajivunia uwepo wenu Diaspora ambao ni wa kihistoria. Shukran kubwa zitolewe kwa wadau
na taasisi zilizoshiriki kutoa ufadhili ili kulifanikisha Kongamano hili.
Mhe. Rais,
Ndugu Diaspora,
Kongamano hili limeambatana na maonesho ya huduma
zinazotolewa na Taasisi mbalimbali kwa ustawi wa jamii ya Diaspora. Maonesho
hayo yameshirikisha wafadhili na vikundi vya wafanyabiashara, mashirika ya umma
na Taasisi binafsi, pamoja na Diaspora
wenyewe.
Aidha, katika siku mbili hizi kutakuwa na uwasilishwaji
wa mada zitakazotolewa na Watendaji Wakuu wa Wizara, Taasisi za Umma na Sekta
Binafsi. Lengo ni kuwapatia washiriki, hususan Diaspora ufahamu na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii na uwekezaji ambao
unachangia katika maendeleo ya nchi yetu
kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Ushiriki wa Kongamano hili unajumuisha vikundi
vya wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali za utalii, Diaspora waliorejea baada ya
kuishi ughaibuni kwa muda mrefu na wadau wengine kutoka taasisi za umma na binafsi
ziilizopo nchini.
Vilevile, kama ilivyokuwa mwaka jana, Kongamano la mwaka
huu limehudhuriwa na maafisa kutoka Ofisi za Balozi zetu nje ya nchi. Lengo la kuwashirikisha maafisa
hao ni kuhakikisha kuwa wanafuatilia utekelezaji wa maazimio yatakayopitishwa
hapa wakati Kongamano hili. Kwa kutambua
kuwa Balozi zetu ndio kiungo muhimu baina ya Serikali na Diaspora.
Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana.
Mwisho, naomba uniruhusu nichukuwe fursa hii kuipongeza
Kamati ya Maandalizi kwa kufanya kazi hii kwa ushirikiano mkubwa pamoja na
kuwashukuru kwa dhati Taasisi zote zilizodhamini Kongamano hili. Ni malengo
yetu tutaendelea kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja ili kulisukuma gurudumu
la maendeleo ya Taifa letu.
Bila shaka Diaspora wamehamasika vya kutosha na
kuthibitisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali na iko
tayari kuchukua kila hatua kuwashirikisha katika maendeleo chanya ya nchi yetu.
Baada ya kusema hayo naomba nimkaribishe Mhe. Dkt Ali
Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ili aweze
kufungua rasmi Kongamano hili na kuzungumza na Diaspora.
Asanteni
kwa kunisikiliza.
Karibuni sana Mhe. Rais:
No comments:
Post a Comment