Habari za Punde

Dk Shein aitaka Wizara ya Afya kuhamasisha vijana kuchukua fani zote udaktari

                                                     STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
 
PRESS RELEASE
 
    Zanzibar                                                                                       05 Septemba, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Afya kufanya jitihada maalum za kuwahamisisha na kuwashajiisha vijana kuchukua masomo ya fani za udaktari ambazo wengi hawazipendelei ingawa ni muhimu na zinahitajika sana katika kuimarisha huduma za afya nchini.
 
Dk. Shein ametoa agizo hilo leo wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha kupitia Programu ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM (2015-2020)kwa sekta ya afya.
 
Katika kikao hicho kilichofanyika Ikulu, Dk. Shein ametahadharisha kuwa mipango ya kuimarisha na kupanua huduma za afya nchini hazitafikia malengo yaliyowekwa ikiwa baadhi ya fani zitakosa wataalamu kutokana na vijana kutopendelea kuchukua mafunzo katika baadhi ya maeneo ya utaalamu wa afya.
 
“Baadhi ya maeneo ya utalaamu yanakosa watu, kwa sababu vijana hawapendi fani hizo, hivyo ni wajibu wa Wizara kuwamasisha na hili si jambo geni kwani hata sisi wakati wetu tulifanya hivyo” Dk. Shein alieleza.
 
Miongoni mwa maeneo ya afya ambayo Zanzibar inakosa wataalamu kabisa au ni wachache sana ni pamoja na patholojia, wataalamu wa dawa za usingizi na maradhi ya koo.
 
Alifafanua kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imechukua hatua mbali mbali za kuimarisha huduma za afya, ikiwemo kuipandisha hadhi hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya Rufaa na kuzipandisha hadhi hospitali za koteji kuwa za wilaya ambapo zote hizo zinahitaji wataalamu wa kila fani ili ziweze kufikia hatua hizo.
 
Katika mnasaba huo, Dk. Shein ameiagiza Wizara hiyo kuunda mara moja kamati ya mafunzo ya Wizara ambayo itasimamia masuala yote ya mafunzo kwa watumishi kulingana na mahitaji ya rasilimali watu katika sekta hiyo.
 
Sambamba na agizo hilo ameitaka wizara hiyo kuunda haraka Kamati ya Dawa ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya dawa ikiwa ni pamoja na kuainisha mahitaji halisi ya dawa nchini.
 
Dk. Shein amewataka viongozi na watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa kila mmoja anafanyakazi kwa mujibu wa taaluma yake, uzoefu alionao na zaidi kujituma kwa bidii zaidi ili Wizara iweze kufikia malengo yaliyowekwa kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi, Dira ya Maendeleo 2020 na MKUZA II.
 
Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesisitiza haja ya Zanzibar kununua mashine ya kuchunguza vinasaba (DNA)kwa kuwa kifaa hicho ni muhimu katika kufanya uchunguzi mbalimbali wa kitaalamu.
 
“Ni mashine muhimu katika kufanya uchunguzi wa kila aina. Hapa kwetu kwa sasa tunaliona zaidi katika kuamua kesi za jinai lakini ni mashine ambayo vile vile inaweza kutumika katika kufanya tafiti nyingi” Dk Shein alieleza.
 
Katika kikao hicho, Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alieleza kuwa lengo makhsusi la Programu ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020ni kufikisha huduma za afya karibu na wananchi wote mijini na vijijini.
 
Alifafanua kuwa katika kutekeleza Ilani hiyo, wizara yake imebuni programu tatu kuu ambazo ni Kinga na Elimu ya Afya, Programu ya Tiba; na Programu ya Usimamizi wa Sera na Utawala.
 
Kwa hivyo ili kuhakikisha programu hizo zinafikia malengo, Waziri alieleza kuwa wizara yake inatekeleza miradi sita ya maendeleo ambayo ni pamoja na Mradi wa Kumalizia Malaria Zanzibar na Mradi wa Afya ya Uzazi na Mtoto.
 
Miradi mingine ni Mradi wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Ukoma, Mradi wa kuipandisha hadhi hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya Rufaa, Mradi wa Kupandisha hadhi hospitali za Koteji kuwa za Wilaya na Mradi wa Ujenzi wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz &sjka1960@hotmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.