Habari za Punde

Iran kutoa fursa zaidi za mafunzo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar

 Mkurugenzi Mkuu kutoka Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Balozi Hussein Mollale Abdullahi akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Jengo la Baraza la Wawakilishi lilipo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu kutoka Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Balozi Hussein Mollale mara baada ya mazungumzo yao.

Wa kwanza kutoka Kulia ni Katibu wa kwanza Msaidizi wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Mjini Dar es salaam bwana Mohammad Dehghani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran imeahidi kuendelea kutoa fursa zaidi ya Mafunzo ya Elimu ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar katika mpango wake wa kuimarisha uhusiano uliopo kati yake na Zanzibar uliodumu kwa muda mrefu sasa.  

Fursa hizo zitazingatiwa zaidi katika fani ya Uhandisi kwa vile Visiwa vya Zanzibar tayari viko katika maandalizi ya utafiti wa mafuta na gesi ikijiandaa kuelekea katika uimarishaji wa Sekta ya nishati itakayosaidia kubadilisha uchumi wa Zanzibar katika miaka michache ijayo.

Mkurugenzi Mkuu kutoka Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Balozi Hussein Mollale Abdullahi alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Hussein alisema Iran kwa vile imebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi zilizopelekea kuongoza nafasi ya Pili katika uzalishaji wa mafuta na Gesi Duniani imejitolea kuunga mkono Mataifa Rafiki katika azma ya  Mataifa hayo kujenga uwezo zaidi wa kujitegemea.

Akizungumzia miradi ya kujitegemea Balozi Hussein alisema Taifa lake lilioko Mashariki ya Kati tarayi limeshatoa msaada mkubwa wa Vifaa na mashine kwa ajili ya chuo cha Amali kiliopo Mkokotoni ili kuwajengea uwezo vijana wanaopata mafunzo ya ujasiri amali kwenye chuo hicho.

Alisema Mafunzo ya Amali yanayojumuisha fani za ufundi, biashara pamoja na ujasiri amali ndio njia sahihi ya kumuandaa kijana mara amalizapo masomo yake ili apate uwezo mkubwa utakaomuwezesha  kujitegemea katika kuendesha maisha yake ya kila siku.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada wake mkubwa iliyotowa kwa Chuo cha Amali Mkokoni msaada ambao utaleta ukombozi mkubwa kwa kundi kubwa la Vijana kuweza kuwanyooshea njia ya kujitegemea wenyewe binafsi.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuanzisha vyuo vya  Amali Unguja na Pemba lengo likiwa kupunguza wimbi kubwa la ukosefu wa ajira ambalo Serikali Kuu pekee haina uwezo wa kuajiri vijana wote wanaomaliza masomo yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliiomba Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia Mkurugenzi Mkuu huyo kutoka Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Balozi Husseid kuendelea kuisaidia pia Zanzibar katika Sekta ya Afya.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya tayari imeshaanza matayarisho wa ujenzi wa Vitengo vya kutibu Maradhi ya Saratani pamoja na Moyo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mambo ambayo Iran inaweza kusaidia utaalamu na Madaktari kwa vile imeshapiga hatua kubwa katika fani  hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.