Na Fatma Makame/Maida Hamza MCC
Wananchi wa kijiji cha Ndagaa
Wilaya Kati Unguja, wamelalamikia vitendo vya wizi wa mazao yao vinavyofanywa na
baadhi ya vijana wasiopenda kufanyakazi.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi mkaazi wa kijiji hicho bi. safia seif amesema vijana hao wasiopenda
kufanyakazi wanarudisha nyuma maendeleo yao na kushindwa
kufikia malengo waliyojiwekea.
Amesema vijana hao wamekuwa wakifanya
vitendo vya wizi wakati wa usiku mkubwa na imekuwa vigumu kuwakamata licha ya
juhudi za kuwavizia zinazofanywa na wakulima.
Ameongeza kuwa vijana hao wanapoingia
kwenye mashamba yao hawachagui mazao na hata mazao machanga huwa wanayachuma.
Amezitaka mamlaka husika
zikiwemo taasisi za kilimo na masoko yanayotumika kuuzia mazao kuangalia
bidhaa hizo na zile ambazo hazijafikia kiwango cha kuvunwa kuzuiliwa kuuzwa
katika masoko hayo ili kuepuka wimbi la kuuza mazao machanga.
Nae Bwana Salum Seif Hamad amesema
tabia ya kuibiwa mazao yao imekuwa ni ya muda mrefu sasa na bado
hawajapata dawa ya tatizo hilo.
Ameiomba serikali kutoa adhabu kali
kwa vijana wanaojishughulisha na wizi wa mazao ili kuwa fundisho kwa vijana
wenye tabia hiyo.
Ametoa wito kwa vijana
kujishughulisha na kazi yeyote ya halali inayoweza
kuwapatia tija bila kutegemea ajira kutoka serikalini.
Wachimbaji wa kifusi kwa ajili ya
kusaga kokoto wa kiwanda cha Mwera Pongwe wameiomba serikali kuboresha
miundo mbinu ya barabara inayoelekea katika kiwanda hicho ili kuinua
kipato chao na taifa kwa jumla .
Akizungumza na mwandishi wa habari Mkurugenzi
wa kiwanda hicho, Rashid Khatibu Hamad amesema barabara hiyo inasababisha
usumbufu mkubwa kwa wateja wao na baadhi ya gari hushindwa kufika.
Amesema kiwanda hicho kimekuwa msaada
mkubwa kwa vijana wengi kupata ajira na iwapo barabara hiyo itaboreshwa
kiwanda kinaweza kutoa mchango mkubwa zaidi kwa taifa .
Ameongeza kuwa tatizo jengine
linalokikabili kiwanda hicho, baadhi ya wateja wanakosa uaminifu,
baada ya kukopeshwa hushindwa kulipa kwa wakati jambo
linalorudisha nyuma maendeleo ya kiwanda hicho
Wanunuzi wa kokoto na kifusi wa
kiwanda hicho wameiomba serikali kuwapunguzia ushuru wamiliki wa kiwanda
hicho kwa vile wamekuwa wakinunua bidhaa hizo kwa bei kubwa kutokana na
kiwanda kulipa ushuru mkubwa.
Aidha wamewataka vijana
kujishughulisha na kazi za ujasiriamali na kuacha tabia ya kukaa
katika vikundi viovu bila kufanya kazi.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment