Habari za Punde

Waazimia kuunda ‘Mussa Haji Foundation’


Na Salum Vuai, MAELEZO

WAANDISHI wa habari visiwani Zanzibar wamekuja na wazo la kuanzisha taasisi ya kumuenzi  mwanahabari mkongwe marehemu Mussa Haji Foum, aliyefariki dunia Septemba 24, 2016.

Wazo la kuanzisha taasisi hiyo kwa jina la ‘Mussa Haji Foundation’, lilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Hassan Abdalla Mitawi, wakati wa hitma ya mwandishi huyo aliyewahi kuifanyia kazi Sauti ya Tanzania Zanzibar (sasa ZBC).

Baada ya hitma hiyo iliyofanyika jana katika jengo la ZBC Radio Rahaleo, Mitawi alisema mtu aliyetumia muda wake mwingi katika tasnia ya habari pamoja na kuwafundisha wengine, hawezi kupita hivihivi bila kuwepo alama itakayotambulisha mazuri yote aliyoyafanya.

Mitawi alimsifia marehemu kwa namna alivyokuwa mchapa kazi, mwalimu kwa waandishi aliowatangulia, mpenda ushirikiano na wenzake pamoja na sifa ya kujiamini katika kazi.

“Mimi pamoja na nafasi za uteuzi nilizopata, lakini kwa marehemu Mussa Haji nimejifunza mengi na kuchota sehemu ya hazina ya maarifa aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” alieleza.

Alisema atahakikisha anasimamia vyema azma hiyo wanahabari watakapokuwa na nguzo imara kwa jina la marehemu ambayo inaweza kutumika kuzalisha na kuwaendeleza waandishi waliopo na watakaokuja.

Mkongwe wa tasnia ya habari Zanzibar Enzi Talib Aboud, alisema mtu hawezi kutaja majina ya wanahabari wakubwa bila kuwemo jina la marehemu Mussa Haji, ambaye alisema alijitolea maisha yake yote kuiendeleza fani pamoja na kujisomesha.

“Hata kifo chake kimemkuta akiwa kazini, hiki ni kielelezo cha mtu aliyethamini kazi yake, lakini la kufurahisha zaidi hakuwa mtu wa kuota kuvaa joho la ukubwa kwa kulilia vyeo,” alifahamisha.

Baadhi ya watoto wa marehemu waliohudhuria kisomo hicho, waliishukuru ZBC na wanahabari wote kwa kuonesha upendo kwa mzazi wao huyo, huku wakiomba wapatiwe zaidi taarifa zake ili iwe  kumbukumbu nzuri kwao na kwa wajukuu zake.

Mapema, mtangazaji wa ZBC Radio Sheikh Mlekwa Muhidin, akitoa mawaidha, aliwakumbusha watu wote kufahamu kwamba kifo ni faradhi isiyoweza kukimbilika kwani kiko mbele ya binadamu na sio nyuma yake.

“Kila unapofanya sherehe za kutimiza miaka kadhaa ya kuzaliwa, elewa kuwa unapunguza masafa kati yako na mauti ambayo yako mbele yako unayafuata, hivyo tujue maisha ya duniani ni mafupi na tujiandae kwa kesho,” alisema.

Marehemu Mussa Haji Foum aliyefariki dunia Septemba 24 baada ya kugongwa na gari na kuzikwa siku iliyofuata kijijini Pitanazako Kikombetele Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, alizaliwa mwaka 1943 na kuanza kazi ya utangazaji katika Sauti ya Unguja mwaka 1963.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.