Habari za Punde

Serikali kuimarisha ustawi wa wazee
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba                                     1.10.2016
---
RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa kwa kuthamini michango ya wazee, katika kipindi hiki cha pili cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi, Awamu ya Saba, Serikali itahakikisha inaongeza kasi katika kupanga na kutekeleza mipango yenye lengo la kuimarisha ustawi wa wazee.

Dk. Shein aliyasema hayo leo  katika hafla ya Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, pamoja na kumpongeza Dk. Shein hafla iliyofanyika huko Gombani, Wilaya ya Chake, Mkoa wa Kusini Pemba na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo wazee kutoka maeneo mbali mbali ya kisiwa cha Pemba.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa hivi karibuni aliuita uongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto ofisini kwake Ikulu kwa lengo la kuja kumueleza jinsi Wizara hiyo ilivyojipanga katika kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchagauzi Mkuu wa mwaka 2015-2020, Ibara ya 165 iliyoainisha mambo muhimu ya kufanyiwa wazee.

Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatakiwa iyatekeleze kwa ajili ya wazee ni pamoja na kuhakikisha wazee wanatambulikana na kupatiwa huduma za matibabu bila ya malipo, kuhakikisha wazee wanapatiwa haki zao za kisheria na kupatiwa fursa sawa katika ngazi zote.

Mambo mengine ni pamoja na kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya ukatili vikiwemo mateso na mauaji, kuwawekea miundombinu na mazingira bora yatakayowawezesha kwenda wanapotaka na kutumia vyombo vya usafiri wa umma kwa gharama nafuu pamoja na kuweka utaratibu utakaowawezesha wazee kulipwa pensheni.


Dk. Shein alieleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa wazee katika kujenga misingi imara ya maendeleo hapa nchini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 iliandaa na kutekeleza mipango  imara ya kuwatunza, kuwaenzi na kuwaendeleza  wazee.

Alisema kuwa juhudi hizo za Serikali ambazo zinatekelezwa hadi hivi leo pamoja na utamaduni wa Zanzibar unaohimiza kuwa na mapenzi na wazee kwa kuwatunza na kuwashirikisha katika mipango ya maendeleo na kifamilia, zimeifanya Zanzibar kuwa ni miongoni mwa nchi bora katika bara la Afrika inayotekeleza vyema maisha ya uzeeni.

Dk. Shein alisema kuwa mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya 1964, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliwajengea wazee nyumba za makaazi, Unguja na Pemba kwa ajili ya kuwaenzi na kuwatunza pamoja na kuwapa huduma muhimu bila ya malipo mambo ambayo hadi leo  yanaendelezwa.

Pamoja na hayo, alieleza kufarajika kwake na kuanza kutekeleza kwa ufanisi mkubwa mpango wa kuwapatia pensheni maalum wazee wote wa Unguja na Pemba waliofikia umri wa miaka 70 bila ya kujali historia ya kazi walizokuwa wakizifanya huku akieleza azma ya serikali ya kuongeza fedha hizo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kupokea kwa masikitiko suala la udanganyifu uliofanywa na baadhi ya watendaji wa kuwaingiza baadhi ya watu waliokuwa hawana sifa, katika orodha za wazee wanaostahiki kupata malipo.

Kutokana na hilo Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto kulishughulikia tatizo hilo na kuwachukulia hatua watendaji wote walioshindwa kuwajibika na ambao wamelisababisha tatizo hilo.

Dk. Shein alisisitiza kuwa waliofanya vitendo hivyo si waadilifu na hawana sifa za kufanya shughuli hizo na kueleza kuwa watu hao wapo na ni lazima wachukuliwe hatua na wawajibishwe.
Dk. Shein alieleza kuvutiwa na kufurahishwa na kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya siku ya wazee, ambayo inasema ‘Chukua hatua, dhidi ya unyanyasaji wa wazee” na kusisitiza kuwa kauli mbiu hiyo inakwenda sambamba na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, udhalilishaji watoto na vitendo vyote vya ukatili katika jamii.

Alieleza kuwa hatua kubwa zimechukuliwa katika kulishughulikia suala la kiinua mgongo kwa wafanyakazi wa Serikali waliostaafu na kusema kuwa hivi karibuni mnamo mwezi Marchi kiasi cha Tsh. Bilioni 16.2 zilitolewa kwa ajili ya kuwalipa watu viinua vyao mgongo na wengi walifaidika hasa wale waliotaka kwenda Hijja.

Nae  Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Modelin Castiko wamo katika mchakato wa kuwapatia vitambulisho maalum wazee ili viweze kuwasaidia katika kupata huduma muhimu.

Waziri Castiko alieleza jinsi wazee walivyofarajika na hatua za Serikali zinazochukuliwa kwa ajili yao katika kuwasaidia katika maisha yao sambamba na kueleza haja ya kuwatunza na kuwaenzi wazee na watoto.

Mkurugenzi wa Shirika la Help Age International Tanzania Bi Amleset Tewodos alisema kuwa Umoja wa Mataifa mwaka huu umehakikisha kuwa na kauli mbiu ambayo itaondosha ubaguzi kwa wazee.

Alisema kuwa sherehe hizo zinakuja wakati mwafaka ambapo Rais D. Shein ameaweka peshenai ambayo ni huduma ya kwanza kutoklewa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa wazee.

Alielezaa kuwa kutolewa kwa pensheni jamiii itasaidia kuondoa umasikini na inatekeleza malengo endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa ambapo nchi zote duniani zimeamua kutekeleza hatua hiyo muhinu itayohakikisha afya na maisha bora kwa wazee.

Nao Wazee wa Zanzibar katika risala yao walieleza kuwa masuala ya wazee Zanzibar yalianza kushuhulikiwa kabla ya tamko la Umoja wa Mataifa kwani hatua za kuwatuza wazee na kuwasaidia ilianza rasmi mara baada ya Mapiduzi ya 1964 chini ya uongozi wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Wazee hao walieleza kuwa April 15, 2016 Zanzibar iliweka mfamo mpya wa kuwalipa pensheni jamii wazee, chini ya uongozi wa Dk. Shein kwani huo ni ukombozi wa kuondosha umasikini kwa wazee kwani pesa walizozipata wanaendesha miradi yao midogo midogo na kuwasaidia  katika maisha yao.

Wazee hao walieleza imani yao kwa Rais Dk. Shein pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuziomba Serikali hizo kuwa wazee wajulikane kuwa ni kundi tete na hivyo linahitaji kuwekewa mipango thabiti ya kuwaendeleza katika maisha yao.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.