MJASIRIAMALI katika mji wa Chakechake anaeuza
nguo, ambae hakupenda jina lake litajwe, akizungumza na waandishi wa habari
mjini Chakechake katika soko la Jumapili, ambae yeye hakuathiriwa na migomo
iliokuwepo kisiwani Pemba, (Picha na Abdi Juma, Pemba)
-Jinamizi
la ‘kidigitali’ kwa uchumi wa wanawake
-Wapo
waliokwisha uwaga umaskini, sasa warejea tena
Na Haji
Nassor, Pemba
“UMASKINI
nilishauwambia bayi….bayi…., lakini sasa naurejea taratibu maana…!!!!...’’,aliniambia
mwanamke mjasiriamali.
Yeye ni mcheshi wastani na mchangamfu wakati wote na hasa anapokuwa
kwenye biashara yake ya duka la vinywaji na vyombo vya matumizi ya nyumbani,
eneo la Wawi wilaya ya Chakechake ndani ya kisiwa cha Pemba.
Siti Rashid Salim (39), ni mrefu wastani, mwenye uso wa duwara
unaon’gaa wakati wote, ambae kwa sasa ameshatalikiwa na aliekuwa mume wake
miaka minne iliopita.
Alianaza biashara ya duka akitokea kwenye kilimo cha jembe la
mkono, tokea mwaka 2012, akiamini kuwa huko ataagana na umaskini.
“Naam….. biashara ya vyombo, juisi, soda na vitafunwa ilinikubali
kisawa sawa na mimi nilishaagana na umaskini kitambo, na maisha yangu yalikuwa
juu na nikawa mwanamke wa kutegemewa na familia’’,alituhadithia.
Nae kama walivyo watu wengine, aliamua kufanya biashara na kujikusanyia
idadi ya wateja wastani wa 40 wa siku moja, na wakati akifunga duka mishale ya
saa 3:30 usiku mapato hakuyaamini.
“Mimi ilikuwa nahesabu mauzo, na kisha najikuta na shilingi
150,000 hadi shilingi 160,000 na hapo sasa familia ilianza kuniangalia kwa
jicho la utajiri’’,alifafanua.
Nikizungumza nae kwenye duka lake eneo la Wawi, kwa muda wa saa
moja, bila ya kutokea mteja kutokana na kugomewa kwa sababu ya chama
anachokishabikia, anasema sasa yeye na umaskini yuko karibu mno mithili ya meno
na ulimi.
“Ahaa…duka lilikuwa limejaa hadi bidhaa nyengine kama chupa za
chai zilikuwa nimezipanga chini hadi nje barazani, sasa unaona… kama
lililoingia moto, hakuna liwalo na umaskini umeshanipiga mbeleko’’,alinieleza
kwa huzuni.
Mbeleko kwa Pemba ni kumchukua na kumuweka mgongoni mtu na hasa
mtoto, kwa kutumia kanga ama kitenge, ndivyo mjasiriamali huyu, anavyojifananisha
yeye na kurejea tena kwenye umaskini, baada ya kubaguliwa na wanakijiji
wenzake.
Kwenye biashara yake hiyo mchanganyiko, alininong’oneza kwa sauti
nyembamba huku akichezea chezea mkoba wangu wa kamera, kuwa uuzaji wa kinywaji
cha juisi pekee aliokuwa akiitengeneza mwenyewe, akiuza kati ya shilingi 35,000
hadi shilingi 40,000 kwa siku moja.
Kumbe ndoo nne za juisi kwa wakati huo kabla ya kugomewa,
zilimtosheleza kumudu gharama za kodi (pango) ya mlango, ambao ni shilingi 40,000
kwa mwezi mmoja.
Mwanamke huyu mfanyabiashara, ikifika mwezi Oktoba mwaka huu,
atakuwa ameshajikusanyia deni la kodi ya mlango la mwaka mmoja, la shilingi
480,000 sawa na shilingi 240,000 kwa kila miezi sita.
Maana kabla ya kususiwa na wateja wake, alikuwa akiuza wastani wa
shilingi 150,000 kwa siku, muda wa saa 15 anazofungua duka, kiasi ya shilingi
10,000 kwa kila saa moja, ambapo kwa sasa hazizidi shilingi 10,000 kutoka saa
1: 00 asubuhi hadi saa 3:00 usiku.
Ukifika ndani ya duka lake lililo nje kidogo ya mji wa Chakechake,
utakaribishwa na vikamba kamba, alizokuwa akifungia biashara za kuning’inia
sambamba na fremu za miti, zikiwa tupu alizokuwa akitunzia bidhaa.
Siti ambae ni mjane, anaeishi na mama yake wa kambo na baba yake mzazi
akiwa na watoto watano, wanaomtegemea na mmoja aliekuwa akimsomesha darasa la
kumi na mbili, sasa anaelekea kusita masomo kwa ukosefu wa ada kwenye shule
binafsi Unguja.
Pamoja na kuambiwa uso kwa uso na baadhi ya watu kwamba amegomewa,
lakini mwezi wa Machi mwaka huu, alibandikiwa karatasi ikitoa onyo kwamba
kusiwe na mtu atakae mnunulia mfanyabiashara huyo.
“Tangazo si ruhusa mtu yoyote kutumiya duka la siti atakaeonekana kazi
kwake’ ilieleza karatasi aliobandikiwa kwenye mlango wake wa duka.
“Mimi sitoachana na chama changu
kwa sababu wengine tu hawakipendi, wao wanachama chao na sisi tuna chetu, sasa
vyama na biashara havina uhusiano, maana vipo vingi kusudi mtu achague
atakacho’’,alilalamika.
Siti, ni mmoja tu lakini kwa mujibu wa Chama cha Mapinduzi CCM
Kisiwani Pemba, wapo wanawake 20 kisiwani Pemba, wakiwa wamegomewa biashara
zao, kutokana na kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi Machi 20 mwaka
huu, hapa visiwani.
Wilaya ya Wete, ikiwa na wanawake wafanyabiashara sita (6),
Micheweni tisa (9), Mkoani wawili (2) na wilaya ya Chakechake ikikusanya
wanawake wafanyabiashara watatu (3) nao walikumbwa na hasara kwa kugomewa.
Mwanaali Ali (40) wa shehia ya Kizimbani wilaya ya Wete, yeye
anasema biashara yake ya chakula bandarini wete, ameiaacha moja kwa moja,
kutokana na kugomewa na wateja wake.
“Ilikuwa mimi nauza wali,
mikate, harage, chai na maandizi, na kwa siku nilikuwa nikijipatia faida kati
ya shilingi 20,000 hadi shilingi 25, 000, sawa na shilingi 750,000 kwa mwezi
lakini sasa wapi’’,alifafanua.
Kabla ya kugomewa, hakuwa na tatizo la kuwahudumia watoto wake
watano, wanaomtegemea, ingawa kwa sasa, hana miundombinu sahihi ya kujiipatia
kipato.
Mwahija Al-masi Issa (25) wa kijiji cha Msuka Micheweni, akitoa
malalamiko ya kususiwa na wateja wake mbele ya Makamu wa Pili wa rais
alipowatembelea, alisema kwa sasa amelazimika kulifunga duka lake la chakula.
“Mimi kwa sasa nisharejea kwenye kilimo cha mwani, ambapo huko
hupata fedha kiduchu shilingi 150,000 kila baada ya kuuza mwani nilioushughulikia kwa
miezi mitatu, fedha nilizokuwa zikipata marambili kwa siku kwenye
duka’’,alisema.
Lakini Sakina Pandu Makame (50) wa Kiwani wilaya ya Mkoani, yeye
pamoja na kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio, wala hajapa mtikisiko wa
biashara yake, na anaendelea kula bata vyema.
‘‘Mimi nilikosa mauzo siku niliokwenda kwenye uchaguzi tu, lakini
sasa biashara yangu imeneemeka, sana na wala sijaona kwamba kuna wateja
wananikwepa, hakuna chama hapa kazi tu’’,alifafanua.
Fatma Kombo anaeuza biashara za nguo wa Chakechake mjini, wala
hajaona tofauti kwenye mapato yake ya siku.
Maana kabla ya kuwepo kwa taarifa za migomo alikuwa akiuza
shilingi 200,000 na sasa ana ongezeko la shilingi 25,000 katika mauzo yake.
“Migomo kwa kweli ipo, lakini mimi pamoja na chama nilicho, hakuna
kususiwa hapa, maana kila mmoja anataka ang’ae anapotaka kwenda kwenye chama
chake na nguo zangu ni za kiwango’’,alisema kwa kujiamini.
Wateja waliopo maeneo hayo, wanasema ipo kauli ya baadhi ya
viongozi wa vyama vya kisiasa wametoa matamko ya kuwataka wasishirikiane na
waliokubali kurejea uchaguzi wa marudio.
“Mimi lakini jina usinitaje, ni kweli chama kilitutaka
tusishirikiane na walioshiriki demokrasia, moja ni hilo la kutowanunulia bidhaa
zao’’,alisema.
Asha Mtende Hassan wa Wawi, anasema hawajali kuuporomoa uchumi wa
mwanamke mwenzao, maana wanatekeleza maagizo ya chama chao cha CUF, ya
kutoshirikiana na yeyote alieshiriki uchaguzi wa marudio.
Katibu wa CUF wilaya ya Chakechake Saleh Nassor Juma, anakiri kuwa
kutowanunulia wanawake biashara zao ni kuwaangusha kiuchumi.
“Unajua hakuna dawa tamu, hii ni chungu kwa uchumi wa wanawake,
lakini ndio maagizo ya chama chetu lazima tuyatii”,alisisitiza.
Katibu wa CCM Mkoa wa kaskazini Pemba Khadija Nassor Abdi, anakiri
kuwa wapo wanachama wake wanawake waliogomewa kwenye biashara zao, na hivyo
kuporomosha uchumi wao, ingawa chama kinajipanga kuwasaidia.
Lakini Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania ofisi ya
Zanzibar TAMWA, kupitia Mratib wake Mzuri Issa, hivi karibuni akizungumza na
vyombo vya habari, alisema lazima udhalilishaji wa aina hii upigwe vita.
“Mwanamke kumzuilia kushiriki uchaguzi, au kumlazimisha kuchagua
kiongozi anaetaka mwanamme au kumsusia biashara kwa sababu ya kutumia
demokrasia yake ni udhalilisha wa kiuchumi’’,alisisitiza.
Haki ya kufanya kazi imetajwa ndani Katiba ya Zanzibar ya
mwaka
1984, kwenye kifungu cha 21, ingawa kundi hili la wanawake kwa kususiwa kwao,
wananyimwa haki hii.
Mwenyekiti wa
Chama cha Wakulima taifa ‘AFP’ Said Soud Said, yeye anaona uchumi kwa kundi la
wanawake unaweza kuporoka iwapo mamlaka husika hazikuwajibika.
“Kama kuna vyama au taasisi nyengine ni vyema zikae meza moja, ili
kuondoa migomo, na kuona wanawake waliojiajiri hawarudi tena kwenye
umaskini’’,alishauri.
Sheikh wa msikiti wa kijiji cha Ole Mchangani wilaya ya
Chakechake, Khamis Hamad Ali, anasema hakuna namna ya kususia biashara kwa
wanawake, kwa sababu za mambo ya kisiasa.
“Mwanamke ametajwa vyema sana kwenye Qur-an tukufu na hata hadithi
za Mtume (S.A.W) kwamba anawajibu wa kufanya biashara, sasa lazimawapewe
ushirkiano.
Mchungaji Benjamen Kissanga wa KKKT usharika wa Chakechake
Vitongoji kwenye kongamano moja lililofanyika kituo cha huduma za sheria,
alisema kususiana haimo katika bibilia.
“Wala kanisa halina shaka juu ya mwanamke kujitegemea kwa kufanya
kama biashara, sasa wakianzisha kisha wakatemgwa kwa siasa ni kuwakabidhi
umaskini’’,alifafanua.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, anasema kama
ukimuelimisha mwanamke, ndio jamii hata kwenye uchumi hali iko hivyo.
Sasa wananchi niwashauri waache kuwakimbia baadhi ya wafanya
biashara wanawake wa sababu za vyama vyao, waangalie jinsi wanavyoweza
kuwarejesha kwenye umaskini.
Siti Rashid Salum, anashauri ili kuondoa migomo ya wafanyabiashara
wanawake ni kuhakikisha vyombo husika vinakaa meza moja ili kuondoa
siuntafahamu ya kisiasa.
Ingawa Mwanaali Ali, yeye anaona ili kuondoa hali hiyo, wanaoichochea
wakaelimishwe ili watambue athari za za muda mrefu na mfupi.
Aliekuwa mgombe urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha JAHAZI
ASILIA, Kassim Bakar Ali, anashauri kuwa, suala la vyama vya kisiasa lishughulikiwe
kwenye vikao, badala ya kuhamia kwenye kuwabagua wafanyabiashara.
Viongozi wa dini, nao wamewataka waumini wao kufuata miongozo ya
vitabu vyao wakati wote wa maisha yao, badala ya maagizo ya taasisi za vyama
vya siasa.
Sheha wa shehia ya Micheweni Dawa Juma Mshindo, anasema wakati
umefika kila jambo limalizwe kidemokrasia badala ya kuwaaumiza wanawake wenye
biashara.
Mara baada ya Oktoba 28 mwaka jana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar ZEC, Jecha Salim Jecha, kuyafuta matokeo ya uchgauzi mkuu wa vyama,
hali ya kisiasa hakitulia.
Ndio maana wapo waliosusiwa kwenye biashara zao na hasa baada ya
watu hao wakiwemo wanawake kukubali kurejea kwenye uchaguzi wa marudio
uliofanyika Machi 20 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment