STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 11.11.2016

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amezindua wodi Mpya ya Watoto na Wazazi katika hospitali ya
Mnazi Mmoja na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwekeza na kuongeza bajeti
yake ya kila mwaka katika sekta ya afya na elimu kwa kutambua kuwa maendeleo ya
taifa lolote lile yanaletwa kwa nguvu kazi yenye afya bora na yenye elimu.
Katika hotuba yake kwa
mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa majengo hayo yenye vifaa vya
kisasa, Dk. Shein alisema ujenzi wa majengo hayo ni kuendeleza dhamira ya
serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma
bora za afya.
Mbali ya kutekeleza
dhamira hiyo,Dk. Shein alibainisha kuwa kukamilika kwa ujenzi huo ni sehemu ya
utekelezaji wa ahadi yake ya kuipandisha daraja hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa
ya rufaa.
Alifafanua kuwa
kukamilikam kwa wodi hizo mpya itakuwa chachu katika kuendeleza mafanikio
yaliopatikana ya kupunguza idadi ya vifo vya watoto na akina mama vitokanavyo
na uzazi na sababu nyenginezo hapa nchini.
Katika hotuba yake Dk.
Shein alisema kuwa takwimu zinaonesha kwamba, uwiano wa vifo vitokanavyo na
uzazi umeshuka kutoka vifo 288 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2010 hadi vifo
236 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015.
Alisema kuwa kuwepo
kwa majengo hayo yenye nafasi ya kutosha, vifaa vya kisasa na mazingira yenye
faragha na stara ya kutosha, kutasaidia sana kuendeleza mafanikio yaliopatikana
katika kushajiisha kina mama kujifungulia hospitali na katika vituo vya afya.
Aidha, Dk. Shein
aliwahakikishia wananchi, kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kuitekeleza ahadi aliyoitoa ya kutoa huduma za afya bure kwa wazazi wote.
Alisema kuwa alitoa ahadi hiyo ili kuimarisha usalama wa
kinamama wanaojifungua na kuwapa fursa pana zaidi wale wenye uwezo mdogo wa
kuweza kufaidika na huduma hizo ili hatimae kwa pamoja kupata mafanikio yanayopatikana
ya kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi.
Pia, Dk. Shein
aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendelea kutoa huduma za chanjo kwa
watoto ili kuwakinga na maradhi mbali mbali pamoja na kuhakikisha huduma za
uchunguzi wa maradhi kama vile ‘X-ray’ ‘ultrasound’ na ‘CT-Scan’ na baadae
‘MRI’ zitaendelea kutolewa bure.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa shukurani kwa Serikali ya Uholanzi kwa kutoa ushirikiano wake
katika ujenzi wa wodi mpya ya wazazi na kuweka vifaa vipya vya kutowa huduma za
kujifungua.
Alitumia fursa hiyo
kukishukuru Chuo Kikuu cha Haukeland na Serikali ya Norway kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa jengo jipya la watoto pamoja
na kuweka vifaa vipya.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza kwamba wale wote waliopewa dhamana ya kusimamia mpango na utaratibu
wa kuagiza na kugawa dawa kwa wananchi lazima waongeze ari ya uadilifu na
uaminifu mkubwa huku wakihakikisha kuwa dawa zinazoagizwa zinakidhi viwango
vilivyowekwa na zinawafikia wananchi, kama ilivyopangwa.
Katika hotuba yake,
Dk. Shein aliitaka Wizara ya Afya kuwaajiri wale wote waliotayari kufanya kazi
sehemu zote za Unguja na Pemba kwa mujibu wa Mkataba wa ajira ulivyo na
kutowaajiri wale wote wasiotaka kufanyakazi Pemba au mashamba.
Aliitaka wizara hiyo
kuwaagiza wamiliki wote wa maduka ya dawa, Unguja na Pemba, kuzingatia taratibu
za uuzaji dawa, kwa mujibu wa sheria na vibali walivyopewa.
Agizo hilo la Dk.
Shein limekuja kutokana na hivi sasa kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa
wananchi juu ya kutokuwepo na utaratibu mzuri wa kufuatilia na kudhibiti uuzaji
dawa unavyofanywa na wamiliki wa maduka ya dawa Unguja na Pemba.
Dk. Shein aliitaka
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS),
kulishughulikia ipasavyo kadhia ya ongezeko la kuwepo dawa bandia ambazo baadhi
yake zinatengenezwa majumbani na kuishia katika maduka ya dawa pamoja na
uingizaji wa bidhaa za vyakula na vinywaji visivyokidhi viwango na kuwachukulia
hatua wale wote wanaohusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Nae Waziri wa Afya
Mahmoud Thabit Kombo alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuendelea
kutekeleza kwa kasi ahadi zake alizowaahidi wananchi wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment