Habari za Punde

Mama Mwanamwema Shein Awataka Wanawake Kujitokeza Kugombea Nafasi za Uongozi.


Na.Rajab.Mkasaba. Pemba. 
MKE wa Rais wa  Zanzibar Mama Mwanamwema Shein ametoa pongezi za dhati kwa wanawake wote wa Unguja na Pemba  kwa kujitokeza katika kuwania nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi mkuu uliopita, hapa Zanzibar na Tanzania nzima kuanzia nafasi ya Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.
Mama Mwanamwema Shein aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Skuli mpya ya Sekondari ya Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba katika mkutano kati yake na Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wa Wilaya ya Mkoani, mkutano wenye lengo la kusalimiana, kupongezana na kubadilishana mawazo.

Katika maelezo yake Mama Shein, alitoa pongezi maalum kwa wanawake wote waliojitokeza kuwania nafasi hizo na wakaweza kuibuka kuwa washindi katika nafasi ya Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.

Alisema kuwa ushindi uliopatikana ni muhimu sana kwa maendeleo ya wanawake na wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla kwani ushindi huo umeongeza ushiriki katika nafasi za uongozi wa juu na kuwaweka katika nafasi nzuri kwenye suala zima la kufanya maamuzi ya nchi yao.

Mama Shein alisema kuwa ni faraja kubwa kwa wanawake kuona kwamba Serikali zote mbili zilizopo madarakani hivi sasa zina hamasisha na kuunga mkono ushitriki wa wanawake katika nafasi za uongozi kwa kuwapa nafasi mbali mbali za uongozi.

Aidha, Mama Shein alitoa shukurani kwa uongozi wa Serikaloi ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kutoa nafasi nyingi za uongozi kwa vijana na wanawake na kutoa wito kwa akina mama wenzake kuendelea kuwa watendaji wazuri, wenye bidii na uadilifu.

Katika mkutano huo jumla ya wanachama wapya 30 waliojiunga na Jumuiya ya UWT walikabidhiwa kadi za Jumuiya hiyo na Mama Mwanamwema Shein.

Nae Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Balozi alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kuwashukuru wanachama na viongozi wa Jumuiya hiyo huku akiwasisitiza kuendeleza amani na utulivu hapa nchini.

Mjane wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Mama Fatma Karume nae alitumia fursa hiyo kutoa historia ya wanawake kabla na baada ya Mapinduzi na kuwasisitiza wanachama na viongozi wa Jumuiya hiyo kutumia muda wao kusoma historia ya Zanzibar.

Aidha, alisema kuwa mbali ya wao kuijua na kuisoma historia ya Zanzibar pia, alieleza haja ya kuwafahamisha na kuwafundisha vijana na watoto wao historia ya Zanzibar kwa kujua walipotoka, walipo na wanakokwenda.

Nao viongozi na wanachama wa Jumuiya hiyo katika risala yao walieleza jinsi wanavyoshirikiana na kusaidiana katika nyakati zote hasa pale mara baada ya uchaguzi mkuu uliopita kutokana na baadhi yao kususiwa katika misiba, harusi na shughuli nyengine za kijamii ikiwa ni pamoja na baadhi yao kupewa talaka kutokana na msimamo wao wa kuiunga mkono CCM.

Wanajumuiya hao walimpongeza Mama Mwanamwema kwa uwamuzi wake wa kuwapongeza na kuzungumza na wanachama na viongozi hao kutokana na ushindi mkubwa uliopatikana katika uchaguzi mkuu uliopita huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono Dk. Shein na kumpongeza kwa hekima, busara, uvumilivu na uwezo  mkubwa alionao katika kuwaongoza wananchi wa Zanzibar.

Wakati huo huo, Mama Shein pia, alikutana na viongozi na wanachama wa Jumuiya ya (UWT), Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba huko ukumbi wa Kituo cha Walimu Wingwi.

Mama Mwanamwema Shein katika hotuba yake alisema kuwa kwa upande mwengine akina mama kupitia umoja wa UWT wanapaswa kuwapongeza wanawake wenzao wote waliojitokeza kugombania kwani ushindi walioupata una umuhimu mkubwa kwa maendeleo na ustawi wa wanawake. 

Aidha, Mama Shein aliwataka wanawake kuongeza kasi katika kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuwawezesha wananchi kiuchumi, hasa wanawake na vijana.

Alisema kuwa lengo la Serikali ni kuona wanannchi wanaondokana na changamoto ya utegemezi wa kipato ambapo juhudi hizo, vile vile zinalengo la kjupunguza na hatimae kuondoa umasikini hapa nchini.

Katika mkutano huo ambao Mama Mwanamwema Shein alipata mapokezi makubwa, ambapo mapema mke wa Makamo wa Pili wa Rais, Mama Asha Balozi aliwataka viongozi wakishapata madaraka warudi kwa wananchi waliowachagua na wakikosa wasiwakimbie na kutowajali.

Nae Mama Fatma Karume aliwataka viongozi hao kuendelea kukimarisha chama chao pamoja na kuwataka viongozi waliochaguliwa na wananchi Majimboni kuwasaidia wananchi waliowachagua ikiwa ni pamoja na kutumia fedha maalum za Majimbo wanazopewa Bungeni na Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya wananchi.

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.