Habari za Punde

Balozi Seif akaribisha Taasisi na makampuni ya uwekezaji ya Mauritius

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Kati kati akizungumza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Sekta ya Utamaduni kutoka Mauritius ukiongozwa na Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius Bwana Santaram Baboo aliyekaa Kulia yake uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

 Balozi Seif  Kushoto akisisitiza umuhimu wa wawekezaji wa Mauritius kuitumia fursa ya uwekezaji iliyopo Zanzibar alipokuwa akimueleza Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Nchi hiyo wa kwanza Kulia.
 Balozi Seif akimpatia zawadi za Viungo { Spice }Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius Bwana Santaram Baboo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.

 Balozi Seif akiwazawadia bidhaa za Viungo Viongozi wa Sekta ya Sanaa na Utamaduni kutoka Visiwa vya Mauritius waliofika Ofisini kwake kwa mazungumzo ya pamoja.
 Balozi Seif akiwazawadia bidhaa za Viungo Viongozi wa Sekta ya Sanaa na Utamaduni kutoka Visiwa vya Mauritius waliofika Ofisini kwake kwa mazungumzo ya pamoja.
Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius Bwana Santaram Baboo akimpatia zawadi Maalum Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza haja kwa Taasisi na Makampuni ya Uwekezaji ya Visiwa vya Mauritius kuanzisha miradi yao ya Kiuchumi na Biashara Zanzibar ili kuitumia vyema fursa iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Sekta ya uwekezaji vitega Uchumi.

Aliitaja Sekta ya Utalii  Zanzibar kuwa imebarikiwa na mazingira mazuri ya rasilmali mbali mbali zinazotoa nafasi pana kwa Miradi ya Kitalii  kama Hoteli pamoja na Usafiri wa Anga kuendelea kuwekezwa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa msisitizo huo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius Bwana Santaram Baboo aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Sekta ya Utamaduni kutoka Mauritius uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 

Alisema Visiwa vya Mauritius vimepiga hatua kubwa kimaendeleo katika Sekta ya Utalii ndani ya kipindi kifupi hatua ambayo Wawekezaji hao hao wanaweza pia kufungua milango ya Uwekezaji hapa Zanzibar katika azma ya kuendeleza ushirikiano wa pande hizo mbili zinazofanana Kiutamaduni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Mauritius kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuwakaribisha Wawekezaji wa Visiwa hivyo kwa kufunga mikataba ya uanzishwaji wa miradi hiyo wakati wowote kuanzia sasa.

Mapema Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Visiwa vya Mauritius Bwana Santaram Baboo alisema upo uhusiano mkubwa wa Kihistoria unaofanana kati ya Zanzibar na Nchi yake hasa katika masuala ya Utamaduni pamoja na uhifadhi  wa urithi wa Kimataifa.

Bwana Baboo alisema Zanzibar  kama ilivyo Mauritius kwa uzuri wake wa maumbile katika rasilmali za Baharini inaweza kutumiwa na Wasanii mbali mbali wa Kimataifa kurikodi Vipindi tofauti vinavyoweza Kuelimisha, kufurahisha lakini pia Kuitangaza  Zanzibar Kiutalii Ulimwenguni.

Waziri huyo wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius alisema mpango huo pia unaweza kuinyanyua Zanzibar Kiuchumi kama ilivyofanikiwa Nchi yake ambayo kwa sasa imekuwa ikipokea watalii Milioni 1.6  kwa  mwaka wakati Visiwa vyenyewe vina Idadi ya wakaazi Milioni 1.3.

Bwana Santaram Baboo  alielezea kufurahishwa kwake na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar kiasi kwamba mbali ya kurejea kwao kushawishi Makampuni na Taasisi za Uwekezaji za Nchi hiyo lakini pia na yeye binafsi ameshawishika kutaka kuwekeza katika miradi ya Hoteli.

Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Visiwa vya Mauritius Bwana Santaram Baboo na Ujumbe wake umekuja Tanzania na Zanzibar kwa ziara maalum ya kuangalia maeneo ya uwekezaji ambayo Nchi hiyo inaweza kuyatumia katika kuanzisha miradi ya Kiuchumi itakayoendeleza uhusiano kati ya pande hizo mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.