Habari za Punde

Hotuba ya Mgeni Rasmi Dk Issa H Ziddy - Mkutano wa kwanza wa asasi za kiraia



MKUTANO WA KWANZA WA ASASI ZA KIRAIA (26-27 Januari 2017)
Kuelekea kwenye mazungumzo endelevu ndani ya Asasi za Kiraia.

HOTUBA YA MGENI RASMI

USULI
Ndugu zangu washiriki wa Mkutano huu muhimu unaozikutanisha Asasi mbalimbali zisizo za Serikali pamoja na wadau wengine wote. Asalama alaykum.

Shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu aliyetujaalia kufika hapa leo tukiwa na hali hii njema ya afya. Bila ya shaka sote tunaelewa sababu na malengo makuu yaliyotukusanya hapa.  Miongoni mwa malengo hayo ni kufanya mazungumzo makini nay a wazi ambayo yana azma ya kuzijenga vyema zaidi Jumuia na Asasi zisizo za Serikali (AZS) za hapa Zanzibar ambazo historia ya kale ya Zanzibar inatuonesha kwamba Asasi zenye misingi hii zilianza tangu ilipoanza mikusanyiko ya watu hapa Zanzibar karne nyingi zilizopita.

Lakini kutokana na anuwai ya watu wa Zanzibar, aghalabu Asasi hizo kwa wakati ule zilikuwa ni za kimakundi maalumu zikiwa na malengo ya kawaida ya kusaidiana, kupata ardhi za kuzikana, kupeana mwega wakati wa matukio ya furaha, huzuni na misiba, kusaidiana kiuchumi na kutaalimishana.

Mwelekeo wa Asasi hizi uligeuka kidogo kuanzia mwishoni mwa karne ya 19 (1890) na mwanzoni mwa karne ya 20 pale Mkoloni alipowagawa watu kisheria kutokana na “makabila” yao. Tangu wakati ule AZS zikaelekea mwelekeo huo ambapo takriban Asasi zote ziliambatanishwa na neno “Association”.  Ilipofika katikati ya karne ya 20, Asasi hizo zikageuka tena kutokana na kuathiriwa na utandawazi wa wakati ule ambapo harakati za kisiasa zilitanda dunia nzima na hasa Afrika. Nyingi ya Asasi hizo zikajikuta zinatumbukia katika harakati za kisiasa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Na nyengine ziligeuka na kuwa vyama kamili vya kisiasa.

Hata hivyo, harakati na shughuli za Asasi nyingi zisizo za serikali Zanzibar, zilipungua kasi kuanzia katikati ya miaka ya 60 ya karne ya ishirini. Badala yake zikazuka Asasi nyingi nyengine ambazo zilikuwa zinafanya kazi kama vyama vya ushirika.

Harakati na shughuli za AZS kwa mfumo tulionao sasa ziliibuka tena mnamo miaka ya 1980 ambapo Serikali iliweka mkazo maalumu kutokana na kuamini kwamba Asasi hizo ni “important force and a necessary tool in strengthening economic and social development” (NGO Policy March 2009). Hadi kufikia mwaka 2007, AZS 510 zilikuwa zimesajiliwa rasmi Zanzibar na Asasi 50 zilisajiliwa kama Jumuia za maendeleo katika vijiji.

Kwa mujibu wa Sera hiyo tuliyoitaja, Serikali iliainisha wazi kwamba: “kuna kila sababu ya kuzijengea AZS mazingira mazuri ili ziweze kushirikiana zenyewe kwa zenyewe kwa upande mmoja na kushirikiana na Serikali kwa upande mwengine kwa lengo la kumfikishia kila mwananchi huduma bora ifikapo mwaka 2020”.
Kwa hivyo ndugu zangu washiriki, miongoni mwa sababu kuu zilizotukusanya hapa leo hii ni pamoja na kutambuwa umuhimu wa mazungumzo na mijadala chanya kwa ajili ya kuzidisha mashirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya Asasi zetu na pia mtu mmoja mmoja. Kwa sababu historia yetu na ya wenzetu kwa jumla inatuonesha kuwa ni muhali kuzishinda changamoto za maendeleo ambazo sote ndiyo tunazopigana nazo bila ya sisi wenyewe kujijengea misingi wa pamoja inayojali utu na ubinaadamu wetu (ubuntu).

Kwa hakika washiriki nyote mnaelewa mafunzo ya dini zetu yanavyotusisitiza tushirikiane katika mambo mema yatayotufikisha kwenye lengo la kuumbwa kwetu.
Ndugu washiriki, mazungumzo na mijadala chanya ndiyo tunu tulizoachiwa na dini zetu. Tumefunzwa tujadiliane na wenzetu kwa lengo la kujenga. Tujadiliane na hata wasioamini tunayoyaamini kwa lugha njema, bila ya kunga’nga’nia upande mmoja, (bali ubora wa mambo ni kuwa kati na kati), uaminifu na kwa akili zilizo wazi na zenye kuzingatia maslahi ya jamii.

Kwa hakika ni lazima kila wakati tunapozungumza na kujadiliana baina yetu tukumbuke kwamba sote tunakusudia kupingana na adui yuleyule ambaye ni umasikini, kuharibika kwa mazingaira, hali ya hewa, afya, unyanyasi wa kijinsia, uwezeshaji wa vijana na uongozi usiobora. Kwa hivyo dhima na nafasi yetu iwe ni kushikamanisha nguvu na uwezo wetu katika mapambano haya na siyo kujigawa na kutawanyika kila mmoja na lake.

HALI HALISI YA AZS KWA SASA
Matokeo ya utafiti uliofanywa hivi karibuni na Mpango wa Kuzisaidia Taasi Zisizo za Serikali Zanzibar (ambao ndio waliotukusanya hapa leo na kesho insha Allah), yanaonesha kuwa idadi ya AZS zilizosajiliwa rasmi Zanzibar hivi sasa zinafikia1600, zikifanya shughuli zake katika sekta mbali mbali zikiwemo zinazohusiana na masuala ya wafanyakazi, uchumi, siasa, kilimo, afya, kujenga uwezo, sheria na haki, walemavu, kupunguza umasikini, jamii, watoto, utawala bora, kuwezesha kiuchumi, mazingira, elimu nk. 

Hata hivyo, utafiti huo umebaini kwamba nyingi ya Asasi hizo zinasuasua. Ni asilimia 15-20 tu ambazo zipo hai na zinajihusisha na shughuli za kimaendeleo katika ngazi mbalimbali. Matokeo hayo yameorodhesha vikwazo na changamoto kadhaa ambazo zinazikwaza AZS na kuzikwamisha zisifikie malengo yake. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kukosekana:

- rasilimali, uaminifu, utaalamu wa kutekeleza mamlaka na uongozi bora, mtazamo wa kimkakati na dira, uratibu imara, umoja na uwazi. Changamoto nyengine ni kutoaminiana, kutuhumiana baina ya serikali na AZS, kuchafuana majina, kutokuwepo uwezo wa kujenga hoja kwa kutumia utafiti na vielezo bainifu, kutokuwa na Umoja endelevu baina yao, kutochangiana taarifa, mafanikio na matatizo na kutofanya kazi kwa pamoja.

Na kwa kweli naamini kuwa changamoto hizo nilizozitaja hapo juu ndizo zilizowasukuma wenzetu hawa kukusanya uwezo wa hali na mali hadi wakafanikiwa kuzikutanisha AZS zilizopo hapa, pamoja na wadau wengine wanaohusiana na maendeleo ya Asasi  hizo, ikiwa ni watoa huduma au ni watekelezaji, kwa ajili ya kuzipatia uwanja muwafaka na nafasi ya kutosha ya siku mbili ya kuzungumza na kujadiliana kwa uwazi, upana na kwa undani kuhusiana na mustakbali, maendeleo na namna ya kuziimarisha AZS Zanzibar ili hatimaye zifikie malengo yanayotarajiwa bila ya kusuasua au kuwepo mivutano baina ya AZS zenyewe kwa zenyewe au baina yake na Serikali.

UMUHIMU WA MKUTANO HUU
Kwa mantiki iliyojitokeza katika utafiti tulioutaja hapo juu, bila ya shaka makusudio ya mkutano huu wa mashauriano yanajikita katika mazungumzo yatayopelekea kufahamu na kuamini au kukataa kuwepo kwa changamoto zilizotajwa, kuzihakiki na kupendekeza kwa pamoja njia, mikakati, taratibu, mbinu na namna ya utatuwaji wake. Aidha madhumuni mengine ambayo ninashauri tuyazingatie wakati wa mazungumzo na mijadala yetu ni pamoja na haya yafuatayo:

1.     Kubadilishana taarifa na maoni miongoni mwa wadau mbalimbali muliopo hapa kuhusiana na hali halisi ya AZS na Jumuia za Kiraia Zanzibar hasa taarifa zinazogusa utekelezaji wa uongozi bora kwa mapana yake yote.

2.     Kufanyika mazungumzo ya wazi yatayoratibiwa vyema yatayogusia masuala ya uongozi katika ngazi mbalimbali, changamoto za utolewaji wa huduma, ushirikiano baina ya Taasisi za umma na za binafsi, uwajibikaji wa kijamii, utambuzi wa mambo na mahitaji ya kiraia na haki za kijamii na kisiasa.  Yote hayo yajadiliwe kwa lengo la kuainisha mahusiano yake katika kuendeleza au kuviza AZS.

3.     Kutathmini namna bora ya kuwepo mahusiano, mazungumzo na ushiriki wa kisera ulio bora na wenye tija za pamoja baina ya serikali na AZS.

4.     Kuwafikiana juu ya hadidu bora za rejea zitazoongoza mazungumzo ya pande hizo mbili kwa sasa na baadae.

Ndugu washiriki wa mkutano huu, ninaweza kusema kwamba, kwa uzoefu wangu unaopindukia nusu karne, huenda ikawa Mkutano wa aina hii ambao umezikusanya sekta nyingi tafauti, na wadau wengi kutoka nyanja mbalimbali ni wa kwanza kufanyika hapa Zanzibar. Kinyume na ilivyo katika nchi za wenzetu ambako mikutano kama hii huwa inafanyika mara nyingi na kuonekana kuwa na mchango mkubwa wa kimaendeleo katika nchi hizo.

Aidha, huenda mkutano huu wa mashauriano ya umma, ambao umezialika AZS za mirengo mbalimbali ukawa ni jaribio la awali litalofungua mchakato, wigo na milango ya kushirikiana kwa karibu zaidi baina ya aina tafauti ya AZS katika yale mambo yenye maslahi ya pamoja na yanayoshughulikiwa nazo. Mambo hayo ni kama vile kupunguza umasikini, utelekelezwaji wa haki na mambo ya kuwaletea wananchi maendeleo. Vilevile mkutano huu unaweza ukawa ni fursa nyengine ya kuendeleza majadiliano ya wazi na serikali kwa njia zilizo rasmi, zinazoushirikisha umma.

Kwa upande mwengine, mashauriano kama haya hayapaswi kuwa ya kupita tu, bali nategemea mtakubaliana kuwa yawe yanafanyika kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kutathmini shughuli za mwaka uliopita, kutafakari kwa pamoja, kujifunza kwa wengine, kuratibu na kupanga mikakati ya pamoja, kuona ya wengine na hata kuiga mafanikio yaliyofikiwa nao. Mtazamo huu utapofanikiwa, washiriki nyote kwa pamoja mtakuwa na heshima kubwa ya kuwa ni waasisi wa mazungumzo endelevu ndani ya AZS na baina yenu na Serikali.

Nina imani thabiti kwamba vilawa/matokeo chanya ya mchakato huu mtaouanza hivi punde, pamoja na makubaliano na maazimio mtayoyaazimia hapa hayatapotea hivihivi tu. Bali yataingizwa katika mikakati ya waandalizi wa mkutano huu, pamoja na kuusaidia Umoja wa Ulaya na washirika wengine wa maendeleo kubaini maeneo ya kuyapa aula na vipaumbele ambavyo wanaweza kuviingiza katika mipango yao ya baadae itayosaidia kuboresha Asasi zetu kwa kuendeleza mazungumzo yatayoibua maeneo mapya ya kuyapa aula.

Kwa upande mwengine, sina shaka kuwa vilawa vya mkutano huu vitawasilishwa kwa njia rasmi katika Kamisheni na wanachama wa jumuia ya Ulaya, washirika wa maendeleo na wadau wengine ambao kwa nafasi zao wataziagiza Asasi zao zinazofanya kazi katika nchini wayaingize maazimio mtayoyafikia katika mipango mikakati yao kama ni Ramani elekezi kwa ajili ya Asasi za Kiraia za Tanzania kama walivyofanya katika nchi nyengine. Aidha, kuna uwezekano mkubwa, maazimio hayo yakaingizwa katika mchakato unaoratibiwa na washirika wa maendeleo wanaojihusiha na kusaidia mipango ya kuimarisha utawala bora kwa kuzisaidia Jumuia za Kiraia za Zanzibar kufikia azma hiyo ya utawala bora, jambo ambalo ni sharti moja wapo miongoni mwa masharti ya usaidizi wao kwa Jumuia za Kiraia.

HITIMISHO
Ndugu washiriki, ninaelewa kuwa, miongoni mwa faida mtazozipata katika mkutano huu ni pamoja na kuzielewa kwa undani kazi za Jumuia hii muhimu inayoshughulika Mpango wa Kuzisaidia Taasisi Zisizo za Serikali Zanzibar, na upeo wa kazi zake zikiwemo za kuzijengea uwezo AZS, kusaidia shughuli za utafiti, kuchangia maendeleo na kuongeza muonekano wa shughuli za Jumuia ya Ulaya.  Kwa maana hiyo, ninaamini kuwa AZS zilizoitikia wito wa kushiriki katika mkusnayiko huu, zitashiriki kikamilifu katika mkutano huu kwa lengo la kugundua fursa zitazojitokeza ili kufaidika nazo kwa lengo la kuimarisha Asasi zetu za kiraia za Zanzibar ili ziimarike zaidi kama zilivyoimarika Asasi za wenzetu katika nchi za Jumuia ya Afrika ya Masharika, nchi za SADC na Afrika kwa jumla.  Nchi ambazo  zimetumia fursa za nafasi kama hii ya kujuana mashirika kama haya, kufahamu kazi zao vyema na hatimaye kujenga mahusiano mema nazo.

Ushauri mwisho ninaoutowa ni kwamba, tuwe wasikivu wazuri, wachangiaji mahiri, waulizaji makini wanaolenga kufahamu, na washiriki wenye malengo ya kuzijenga na kuziimarisha Asasi zetu ambazo kama mlivyoona katika matokeo ya utafiti tuliyoyadondoa katika utangulizi, ni kwa namna gani Asasi zetu nyingi zilivyo nyuma na kwa kweli zinahitaji majukwaa kama haya ili kuziimarisha, kuzihuisha na kuzijengea uwezo.   

Asanteni kwa kunisikiliza, ninakutakieni mkutano mwema wa mashauriano, ambao naamini utakuwa na tija kubwa kwa Asasi zetu zisizo za Serikali na taifa kwa jumla.


Wasalamu alaykum warahmatu Allahi wabarakatuhu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.