Mgeni Rasmin wa Kongamano la Asasi za Kirais Zanzibar Dr.Issa Haji Ziddy, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi Jamii na Taaluma za Lugha.(SUZA) akitowa hutuba yake kwa Washiriki wa Kongamano hilo linalowajumuisha washiriki 150 kutoka Unguja na Pemba wac Asasi za Kiraia linalofanyika kwa muda wa Siku mbili katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Zanzibar.
MKUTANO WA KWANZA WA ASASI ZA KIRAIA (26-27 Januari 2017)
Kuelekea kwenye mazungumzo endelevu
ndani ya Asasi za Kiraia.
HOTUBA
YA MGENI RASMI
USULI
Ndugu zangu washiriki wa Mkutano
huu muhimu unaozikutanisha Asasi mbalimbali zisizo za Serikali pamoja na wadau
wengine wote. Asalama alaykum.
Shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu
aliyetujaalia kufika hapa leo tukiwa na hali hii njema ya afya. Bila ya shaka sote
tunaelewa sababu na malengo makuu yaliyotukusanya hapa. Miongoni mwa malengo hayo ni kufanya
mazungumzo makini nay a wazi ambayo yana azma ya kuzijenga vyema zaidi Jumuia
na Asasi zisizo za Serikali (AZS) za hapa Zanzibar ambazo historia ya kale ya
Zanzibar inatuonesha kwamba Asasi zenye misingi hii zilianza tangu ilipoanza
mikusanyiko ya watu hapa Zanzibar karne nyingi zilizopita.
Lakini kutokana na anuwai ya watu wa
Zanzibar, aghalabu Asasi hizo kwa wakati ule zilikuwa ni za kimakundi maalumu
zikiwa na malengo ya kawaida ya kusaidiana, kupata ardhi za kuzikana, kupeana
mwega wakati wa matukio ya furaha, huzuni na misiba, kusaidiana kiuchumi na
kutaalimishana.
Mwelekeo wa Asasi hizi uligeuka kidogo kuanzia
mwishoni mwa karne ya 19 (1890) na mwanzoni mwa karne ya 20 pale Mkoloni
alipowagawa watu kisheria kutokana na “makabila” yao. Tangu wakati ule AZS
zikaelekea mwelekeo huo ambapo takriban Asasi zote ziliambatanishwa na neno “Association”. Ilipofika katikati ya karne ya 20, Asasi hizo
zikageuka tena kutokana nakuathiriwa na utandawazi wa wakati ule ambapo
harakati za kisiasa zilitanda dunia nzima na hasa Afrika. Nyingi ya Asasi hizo
zikajikuta zinatumbukia katika harakati za kisiasa kwa njia ya moja kwa moja au
isiyo ya moja kwa moja. Na nyengine ziligeuka na kuwa vyama kamili vya kisiasa.
Hata hivyo, harakati na shughuli za Asasi
nyingi zisizo za serikali Zanzibar, zilipungua kasi kuanzia katikati ya miaka
ya 60 ya karne ya ishirini. Badala yake zikazuka Asasi nyingi nyengine ambazo
zilikuwa zinafanya kazi kama vyama vya ushirika.
Harakati na shughuli za AZS kwa mfumo
tulionao sasa ziliibuka tena mnamo miaka ya 1980 ambapo Serikali iliweka mkazo
maalumu kutokana na kuamini kwamba Asasi hizo ni “important force and a
necessary tool in strengthening economic and social development” (NGO
Policy March 2009). Hadi kufikia mwaka 2007, AZS 510 zilikuwa zimesajiliwa
rasmi Zanzibar na Asasi 50 zilisajiliwa kama Jumuia za maendeleo katika vijiji.
Kwa mujibu wa Sera hiyo tuliyoitaja,
Serikali iliainisha wazi kwamba: “kuna kila sababu ya kuzijengea AZS mazingira
mazuri ili ziweze kushirikiana zenyewe kwa zenyewe kwa upande mmoja na
kushirikiana na Serikali kwa upande mwengine kwa lengo la kumfikishia kila
mwananchi huduma bora ifikapo mwaka 2020”.
Kwa hivyo ndugu zangu washiriki,
miongoni mwa sababu kuu zilizotukusanya hapa leo hii ni pamoja na kutambuwa
umuhimu wa mazungumzo na mijadala chanya kwa ajili ya kuzidisha mashirikiano na
kubadilishana uzoefu baina ya Asasi zetu na pia mtu mmoja mmoja. Kwa sababu
historia yetu na ya wenzetu kwa jumla inatuonesha kuwa ni muhali kuzishinda
changamoto za maendeleo ambazo sote ndiyo tunazopigana nazo bila ya sisi
wenyewe kujijengea misingi wa pamoja inayojali utu na ubinaadamu wetu (ubuntu).
Kwa hakika washiriki nyote mnaelewa
mafunzo ya dini zetu yanavyotusisitiza tushirikiane katika mambo mema
yatayotufikisha kwenye lengo la kuumbwa kwetu.
Ndugu washiriki, mazungumzo na mijadala
chanya ndiyo tunu tulizoachiwa na dini zetu. Tumefunzwa tujadiliane na wenzetu
kwa lengo la kujenga. Tujadiliane na hata wasioamini tunayoyaamini kwa lugha
njema, bila ya kunga’nga’nia upande mmoja, (bali ubora wa mambo ni kuwa kati na
kati), uaminifu na kwa akili zilizo wazi na zenye kuzingatia maslahi ya jamii.
Kwa hakika ni lazima kila wakati
tunapozungumza na kujadiliana baina yetu tukumbuke kwamba sote tunakusudia
kupingana na adui yuleyule ambaye ni umasikini, kuharibika kwa mazingaira, hali
ya hewa, afya, unyanyasi wa kijinsia, uwezeshaji wa vijana na uongozi usiobora.
Kwa hivyo dhima na nafasi yetu iwe ni kushikamanisha nguvu na uwezo wetu katika
mapambano haya na siyo kujigawa na kutawanyika kila mmoja na lake.
HALI HALISI YA AZS KWA SASA
Matokeo ya utafiti uliofanywa hivi
karibuni na Mpango wa
Kuzisaidia Taasi Zisizo za Serikali Zanzibar(ambao ndio waliotukusanya hapa leo na kesho insha Allah),yanaonesha
kuwaidadi ya AZS zilizosajiliwa rasmi Zanzibar hivi sasa zinafikia1600,
zikifanya shughuli zake katika sekta mbali mbali zikiwemo zinazohusiana na
masuala ya wafanyakazi, uchumi, siasa, kilimo, afya, kujenga uwezo, sheria na
haki, walemavu, kupunguza umasikini, jamii, watoto, utawala bora, kuwezesha
kiuchumi, mazingira, elimu nk. Hata hivyo, utafiti huo umebaini kwamba nyingi
ya Asasi hizo zinasuasua. Ni asilimia 15-20 tu ambazo zipo hai na zinajihusisha
na shughuli za kimaendeleo katika ngazi mbalimbali. Matokeo hayo yameorodhesha
vikwazo na changamoto kadhaa ambazo zinazikwaza AZS na kuzikwamisha zisifikie
malengo yake. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kukosekana:
-
rasilimali, uaminifu, utaalamu wa kutekeleza mamlaka na uongozi bora, mtazamo
wa kimkakati na dira, uratibu imara, umoja na uwazi. Changamoto nyengine ni
kutoaminiana, kutuhumiana baina ya serikali na AZS, kuchafuana majina,
kutokuwepo uwezo wa kujenga hoja kwa kutumia utafiti na vielezo bainifu,
kutokuwa na Umoja endelevu baina yao, kutochangiana taarifa, mafanikio na
matatizo na kutofanya kazi kwa pamoja.
Na kwa
kweli naamini kuwa changamoto hizo nilizozitaja hapo juu ndizo zilizowasukuma
wenzetu hawa kukusanya uwezo wa hali na mali hadi wakafanikiwa kuzikutanisha
AZS zilizopo hapa, pamoja na wadau wengine wanaohusiana na maendeleo ya
Asasi hizo, ikiwa ni watoa huduma au ni
watekelezaji, kwa ajili ya kuzipatia uwanja muwafaka na nafasi ya kutosha ya
siku mbili ya kuzungumzana kujadiliana kwa uwazi, upana na kwa undani kuhusiana
na mustakbali, maendeleo na namna ya kuziimarisha AZS Zanzibar ili hatimaye
zifikie malengo yanayotarajiwa bila ya kusuasua au kuwepo mivutano baina ya AZS
zenyewe kwa zenyewe au baina yake na Serikali.
UMUHIMU
WA MKUTANO HUU
Kwa
mantiki iliyojitokeza katika utafiti tulioutaja hapo juu, bila ya shaka
makusudio ya mkutano huu wa mashauriano yanajikita katika mazungumzo
yatayopelekea kufahamu na kuamini au kukataa kuwepo kwa changamoto zilizotajwa,
kuzihakiki na kupendekeza kwa pamoja njia, mikakati, taratibu, mbinu na namna
ya utatuwaji wake. Aidha madhumuni mengine ambayo ninashauri tuyazingatie
wakati wa mazungumzo na mijadala yetu ni pamoja na haya yafuatayo:
1. Kubadilishana taarifa na maoni miongoni mwa wadau mbalimbali
muliopo hapa kuhusiana na hali halisi ya AZS na Jumuia za Kiraia Zanzibar hasa
taarifa zinazogusa utekelezaji wa uongozi bora kwa mapana yake yote.
2. Kufanyika mazungumzo ya wazi yatayoratibiwa vyema yatayogusia
masuala ya uongozi katika ngazi mbalimbali, changamoto za utolewaji wa huduma,
ushirikiano baina ya Taasisi za umma na za binafsi, uwajibikaji wa kijamii,
utambuzi wa mambo na mahitaji ya kiraia na haki za kijamii na kisiasa. Yote hayo yajadiliwe kwa lengo la kuainisha
mahusiano yake katika kuendeleza au kuviza AZS.
3. Kutathmini namna bora ya kuwepo mahusiano, mazungumzo na
ushiriki wa kisera ulio bora na wenye tija za pamoja baina ya serikali na AZS.
4. Kuwafikiana juu ya hadidu bora za rejea zitazoongoza
mazungumzo ya pande hizo mbilikwa sasa na baadae.
Ndugu
washiriki wa mkutano huu, ninaweza kusema kwamba, kwa uzoefu wangu unaopindukia
nusu karne, huenda ikawa Mkutano wa aina hii ambao umezikusanya sekta nyingi
tafauti, na wadau wengi kutoka nyanja mbalimbali ni wa kwanza kufanyika hapa
Zanzibar. Kinyume na ilivyo katika nchi za wenzetu ambako mikutano kama hii huwa
inafanyika mara nyingi na kuonekana kuwa na mchango mkubwa wa kimaendeleo
katika nchi hizo.
Aidha,
huenda mkutano huu wa mashauriano ya umma, ambao umezialika AZS za mirengo
mbalimbali ukawa ni jaribio la awali litalofungua mchakato, wigo na milango ya
kushirikiana kwa karibu zaidi baina ya aina tafauti ya AZS katika yale mambo
yenye maslahi ya pamoja na yanayoshughulikiwa nazo. Mambo hayo ni kama vile
kupunguza umasikini, utelekelezwaji wa haki na mambo ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Vilevile mkutano huu unaweza ukawa ni fursa nyengine ya kuendeleza majadiliano
ya wazi na serikali kwa njia zilizo rasmi, zinazoushirikisha umma.
Kwa
upande mwengine, mashauriano kama haya hayapaswi kuwa ya kupita tu, bali
nategemea mtakubaliana kuwa yawe yanafanyika kila mwaka kwa lengo la
kubadilishana uzoefu, kutathmini shughuli za mwaka uliopita, kutafakari kwa
pamoja, kujifunza kwa wengine, kuratibu na kupanga mikakati ya pamoja, kuona ya
wengine na hata kuiga mafanikio yaliyofikiwa nao. Mtazamo huu utapofanikiwa,
washiriki nyote kwa pamoja mtakuwa na heshima kubwa ya kuwa ni waasisi wa
mazungumzo endelevu ndani ya AZS na baina yenu na Serikali.
Nina
imani thabiti kwamba vilawa/matokeo chanya ya mchakato huu mtaouanza hivi
punde, pamoja na makubaliano na maazimio mtayoyaazimia hapa hayatapotea
hivihivi tu. Bali yataingizwa katika mikakati ya waandalizi wa mkutano huu,
pamoja na kuusaidia Umoja wa Ulaya na washirika wengine wa maendeleo kubaini
maeneo ya kuyapa aula na vipaumbele ambavyo wanaweza kuviingiza katika mipango
yao ya baadae itayosaidia kuboresha Asasi zetu kwa kuendeleza mazungumzo
yatayoibua maeneo mapya ya kuyapa aula.
Kwa
upande mwengine, sina shaka kuwa vilawa vya mkutano huu vitawasilishwa kwa njia
rasmi katika Kamisheni na wanachama wa jumuia ya Ulaya, washirika wa maendeleo
na wadau wengine ambao kwa nafasi zao wataziagiza Asasi zao zinazofanya kazi
katika nchiniwayaingize maazimio mtayoyafikia katika mipango mikakati yao kama
ni Ramani elekezi kwa ajili ya Asasi za Kiraia za Tanzania kama walivyofanya
katika nchi nyengine. Aidha, kuna uwezekano mkubwa, maazimio hayo yakaingizwa
katika mchakato unaoratibiwa na washirika wa maendeleo wanaojihusiha na
kusaidia mipango ya kuimarisha utawala bora kwa kuzisaidia Jumuia za Kiraia za
Zanzibar kufikia azma hiyo ya utawala bora, jambo ambalo ni sharti moja wapo
miongoni mwa masharti ya usaidizi wao kwa Jumuia za Kiraia.
HITIMISHO
Ndugu
washiriki, ninaelewa kuwa, miongoni mwa faida mtazozipata katika mkutano huu nipamoja
na kuzielewa kwa undani kazi za Jumuia hii muhimu inayoshughulika Mpango wa
Kuzisaidia Taasi Zisizo za Serikali Zanzibar,naupeo wa kazi zake zikiwemo
za kuzijengea uwezo AZS, kusaidia shughuli za utafiti, kuchangia maendeleo na
kuongeza muonekano wa shughuli za Jumuia ya Ulaya. Kwa maana hiyo, ninaamini kuwa AZS zilizoitikia
wito wa kushiriki katika mkusnayiko huu, zitashiriki kikamilifu katika mkutano
huu kwa lengo la kugundua fursa zitazojitokeza ili kufaidika nazo kwa lengo la
kuimarisha Asasi zetu za kiraia za Zanzibar ili ziimarike zaidi kama
zilivyoimarika Asasi za wenzetu katika nchi za Jumuia ya Afrika ya Masharika, nchi
za SADC na Afrika kwa jumla. Nchi
ambazo zimetumia fursa za nafasi kama
hii ya kujuana mashirika kama haya, kufahamu kazi zao vyema na hatimaye kujenga
mahusiano mema nazo.
Ushauri mwisho
ninaoutowa ni kwamba, tuwe wasikivu wazuri, wachangiaji mahiri, waulizaji makini
wanaolenga kufahamu, na washiriki wenye malengo ya kuzijenga na kuziimarisha
Asasi zetu ambazo kama mlivyoona katika matokeo ya utafiti tuliyoyadondoa
katika utangulizi,ni kwa namna gani Asasi zetu nyingi zilivyo nyuma na kwa
kweli zinahitaji majukwaa kama haya ili kuziimarisha, kuzihuisha na kuzijengea
uwezo.
Asanteni
kwa kunisikiliza, ninakutakieni mkutano mwema wa mashauriano, ambao naamini
utakuwa na tija kubwa kwa Asasi zetu zisizo za Serikali na taifa kwa jumla.
Wasalamu
alaykum warahmatu Allahi wabarakatuhu
No comments:
Post a Comment