Habari za Punde

UVCCM: Magufuli amekonga nyoyo kuzuia kupanda kwa bei ya umeme

Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam

Umoja wa Chama Cha Mapinduzi  (UVCCM) umesifu msimamo imara  ulioonyeshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujali na kupigania maslahi  ya wananchi wanyonge hatimaye  kuzuia mpango batili  wa Tanesco  kupandisha bei ya umeme nchini .

Pia Umoja huo umeelezea kufurahishwa kwao na kuunga mkono  uamuzi huo ambao umethibitisha  kuwa Dk Magufuli ni mtawala anayejali, kuthamini na kupigania maslahi ya wananchi wanyonge na wenye vipato vya chini.

Matamshi hayo yametakwa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa 
UVCCM Shaka Hamdu Shaka mara baada ya kikao cha watumishi wa UVCCM kutathmini utendaji wa mwaka 2016 na kuweka mikakati ya utendaji kwa mwaka 2017 kilichofanyika katika ukumbi wa UVCCM makao makuu Upanga Dar Es Saalam.

Shaka alikitaja kitendo cha Rais Dk Magufuli kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania  (Tanesco ) ameonyesha  ujasiri, uzalendo na upendo kwa wananchi ambao walimpa dhamana ya kuongoza  dola .

Alisema haiwezekani Bodi au Menijmenti ya Tanesco ifikie hatua ya kuamua au kupitisha maamuzi mazito ya kitaifa na kupandisha bei ya umeme bila ya Waziri dhamana wa Wizara ya Serikali asijulishwe .

"Tuko pamoja na  Dk Magufuli , tunampa mkono wa heko  kuzuia kupanda bei ya umeme,  ametazama  maslahi mapana ya wananchi, hali za  watu wanyonge na wenye vipato vya chini, ametetea maslahi ya waliomuweka madarakani"Alieleza Shaka.

Aidha alisema Tanesco kwa kupitia Mkurugenzi wake na Waziri mwenye dhamana waliwaahidi wananchi kwamba bei ya umeme katu haitapanda hivyo bei kama ingependa na serikali kukaa kimya  ingelikuwa ni kituko cha mwaka.

Kaimu katibu mkuu Shaka aliwataka watendaji wa serikali , wakurugenzi wakuu wa mikoa, wajumbe wa bodi  makamishna, makatibu wakuu na wakurugenzi wa halamshauri za wilaya waendelee kutekekeza majukumu yao kwa mujibu wa mipaka yao,  taratibu na shera bila kukurupuka.

"Watumishi na  watendaji wenye dhamana wakae wakijua mambo yamebadilika, zama hii si zama zile zilizopita, Dk Magufuli na serikali yake ni  makini huku wakifuatilia kila pembe, atakayevimbisha mashavu ya ukaidi  si ajabu akatubuliwa" Alisisitiza Shaka

Hata hivyo UVCCM imewahimiza watendaji na watumishi wa serikali waliopo katika sekta za maendeleo kusoma upepo, kutenda haki na kutimiza wajibu na kwamba maamuzi wanayopanga kuyapitisha ni lazima kwanza yajali maslahi ya Taifa.

Shaka alifafanua kuwa  ni vyema  ikafahamika na kueleweka kwamba  Serikali ya Chama cha Mapinduzi imebeba imani, mioyo, matumaini na maisha ya watu hivyo umma wakati unapokitegemea CCM, anapotokea mtu mmoja akaamua kuvuruga utaratibu heri mtu huyo akawekwa  pembeni.

"Tunaipongeza Serikali ya CCM kwa kuendelea kusimamia nidhamu ya kazi, kupigania dhana ya utumishi wa umma , uwajibikaji, uwazi pia kukomesha vitendo vya rushwa, maonevu na ufisadi , tunamshauri  Dk Magufuli aendelee kusimamia majukumu yake bila kutikisika  "Alisema Shaka

Alimaliza kwa kusema huku akiwataka watendaji dhamana kujipanga  kimkakati na kimipango kwa lengo la  kutimiza ahadi  zote  zilizoanishwa katika  ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2015 /2020 kwa sababu huo ndiyo mkataba kati ya wapiga kura na Serikali ya CCM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.