Habari za Punde

Muhtasari wa Ripoti ya kamati ya fedha, biashara na kilimo ya BLW 2016/17


MUHTASARI WA RIPOTI YA KAMATI YA FEDHA, BAISHARA NA KILIMO YA BARAZA LA WAWAKILISHI KWA MWAKA 2016/2017
Mheshimiwa Spika,
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mwenye kurehemu aliyetujaalia afya na uzima na tukaweza kukutana tena hapa katika Baraza hili kwa ajili ya kutekeleza majukumu yetu tuliyokabidhiwa na wananchi. Vile vile, sina budi kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa hii kuwasilisha mbele ya Baraza hili kwa niaba ya Kamati yetu Ripoti ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo, tunaomba kwa ruhusa yako Muhtasari huu usomwe sambamba na Ripoti yetu na ziingizwe kwenye Hansard.
Mheshimiwa Spika,
Kwa dhati kabisa, tunatoa shukrani zetu kwa mashirikiano makubwa tuliyoyapata wakati wa kutekeleza majukumu yetu ya Kamati kwa uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko pamoja na pamoja na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hizo ambao ndio wahusika wakuu waliofanikisha hadi Kamati yetu inawasilisha Ripoti hii mbele ya Baraza lako.
Mheshimiwa Spika,
Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wadau na wananchi wote wa Unguja na Pemba ambao walishiriki kikamilifu pale Kamati ilipotaka kukutana nao kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Kamati, jambo hili liliipa faraja kubwa sana Kamati kuona ni kwa kiasi gani wananchi wapo karibu na chombo chao cha Baraza la Wawakilishi na kuthamini juhudi zinazofanywa na Wajumbe wa Baraza lako tukufu.

Mheshimiwa Spika,
Vile vile, naomba nitoe shukrani kwa wajumbe wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo pamoja na Makatibu wetu ambao ndio waliofanikisha ufanisi na umahiri wa wajumbe katika kutekeleza majukumu yao. Naomba kwa ruhusa yako niwatambue kwa majina Wajumbe na Makatibu hao kama hivi ifuatavyo:

1. Mhe.  Yussuf Hassan Iddi                   -           Mwenyekiti

2. Mhe. Hamida Abdalla Issa      -           Makamu Mwenyekiti

3. Mhe. Ali Salum Haji                          -           Mjumbe

4. Mhe. Bihindi Hamad Khamis            -           Mjumbe

5. Mhe. Ussi Yahya Haji                       -           Mjumbe

6. Mhe. Moh’d Mgaza Jecha                -           Mjumbe

7. Mhe. Hamad Abdalla Rashid           -           Mjumbe

8. Ndg. Salum Khamis Rashid           -           Katibu

9. Ndg. Asma Ali Kassim                   -           Katibu

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO

Mheshimiwa Spika,

Ni ukweli kwamba Wizara hii ndio roho ya nchi yetu kwani imepewa jukubwa kubwa sana la kusimamia ukusanyaji wa mapato ya nchi na usimamizi wa matumizi ya fedha za wananchi. Kamati yetu imeridhishwa na juhudi za ukusanyaji wa mapato zinazofanywa na Wizara pamoja na Taasisi zake ikiwemo Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa mapato ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka ulioisha. Kuongezeka kwa mapato haya kumetokana na juhudi na mikakati ya Wizara katika kuhakikisha makadirio ya mapato yaliyokusudiwa kukusanywa na Serikali yamefikiwa lengo.


Mheshimiwa Spika,

Hata hivyo, pamoja na mikakati hiyo iliyowekwa Kamati yetu inaamini kuwa bado tatizo la kuvuja kwa mapato lipo na vile vile bado yapo maeneo ya ukusanyaji wa mapato hayajafikiwa, kwahivyo Kamati yetu inaitaka Wizara kuongeza juhudi ya kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha mapato ya nchi hayavuji na kila anayestahiki kulipa kodi basi alipe bila ya kuwa na muhali wowote.

Mheshimiwa Spika,

Kuna kauli ambazo huzungumzwa na baadhi ya watu kuwa, mapato yote yanayokusanywa na TRA – Zanzibar hupelekwa Tanzania Bara, Lakini naomba kuchukuwa nafasi hii kuwaambia wananchi kuwa, mapato yanayokusanywa na TRA – Zanzibar yanaingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na yanatumika Zanzibar, wanaokaa wakisambaza fikra potofu kama hizo kwa wananchi hawaelewi ukweli wa mambo na tunaomba wananchi wa Zanzibar waondoe fikra hizo na waone kuwa Muungano wetu haupo kwa kukandamiza Zanzibar bali ni kwa kuinua uchumi wa Zanzibar.

 Mheshimiwa Spika,

Katika suala la usimamizi wa fedha za umma kwa ujumla bado kuna tatizo, hii inatokana na ukweli kwamba Sheria ya Manunuzi na Kanuni zake hazifuatwi apasavyo, na sote tunafahamu kuwa asilimia 70 ya matumizi ya fedha yanakwenda kwenye manunuzi. Ukiukwaji huu wa Sheria ya Manunuzi unapelekea upotevu mkubwa wa fedha za umma, kwani Kamati imebaini kuwa zipo baadhi ya Taasisi ambazo hufanya manunuzi hewa lakini vile vile kutokana na uhaba wa maafisa wanunuzi zipo baadhi ya Taasisi ambazo wahasibu au washika fedha ndio wanakuwa wanunuzi. Tunaomba sana wakati itakapoanza kutumika Sheria mpya ya Manunuzi iliyopitishwa na Baraza hili iwe ndio suluhisho la matumizi ya fedha yasiyofuata utaratibu wa Sheria.

Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu ilifanya ziara katika mashamba ya Mipira kisiwani Pemba, katika ziara hiyo Kamati ilikutana na viongozi na wafanyakazi wanaoyashughulikia mashamba hayo ambao wameunda kikundi kinachojulikana kwa jina la JIWEZESHE GROUP. Kabla ya mashamba hayo kutumiwa na kikundi hiki, Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliingia mkataba na Kampuni ya AGROTEX ambapo Kampuni ilitakiwa kulipa USD 100,000/- (Dola laki moja) kwa kila mwaka.  Hatima yake, Kampuni hii ilishindwa kulipa fedha hizo kwa Serikali kwa kipindi cha miaka minne (4) na vile vile iIishindwa kulipa mishahara kwa wafanyakazi. Hadi Kamati yetu inawasilisha Ripoti mbele ya Baraza hili, Kampuni hii inadaiwa na Serikali USD 400,000/- (Dola laki nne) kama ni kodi ya mashamba hayo.
Wafanyakazi ambao walikuwa wanayashaghulikia mashamba haya, waliamua kujikusanya pamoja na kuunda kikundi hicho kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uvunaji wa mpira. Idhini ya matumizi ya mashamba hayo yalitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini – Pemba kupitia barua ya tarehe 10 Februari, 2016 yenye Ref: NO. MKP/K.6/3/1/VOL.VII/115.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu haikuridhishwa na uidhinishaji wa matumizi ya mashamba hayo uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kwani wakati uamuzi huu unafanywa mkataba kati ya Serikali na AGROTEX bado haujavunjwa.
Vile vile, Kamati yetu imesikitishwa sana kuona kuwa azma ya kuanzishwa kwa mashamba haya ambayo ilikuwa ni kuinua pato la Taifa na uchumi wa nchi haijafikiwa, kwani mapato mengi ya Serikali yaliyokusudiwa kuingia katika Mfuko wa Serikali kupitia mashamba haya yamepotea.
Maoni na maagizo ya Kamati juu ya kadhia hii yanaonekana katika ripoti ya Kamati, lakini Kamati inasisitiza kuwa Wizara ihakikishe Kampuni ya Agrotex inalipa deni hilo.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu inampongeza sana Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi kifupi alichokaa katika nafasi hii mabadiliko yamenza kuonekana katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha. Kamati imeridhishwa na utaratibu ulioanza kwa baadhi ya Taasisi kukusanya mapato kwa kulipa Bank na sio kulipa cash, jambo hili ni moja kati ya mambo yaliyopelekea kuongezeka kwa mapato, hata hivyo Kamati yetu inamtaka Mhasibu Mkuu wa Serikali utaratibu huu wakulipia benki utumike kwa Taasisi zote za Umma ili kuziba mianya ya kuvuja kwa mapato.

Mheshimiwa Spika,

Suala la uwekezaji ni moja sekta ambazo zinasimamiwa na Wizara hii kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), juhudi zinazofanya na ZIPA zinaonekana kwani ipo miradi mingi inayoendelea ambayo imetokana na kuwepo kwa Mamlaka hii. Hata hivyo, bado yapo malalamiko makubwa sana juu utendaji wa Mamlaka hii ambapo malalamiko haya yanaleta picha mbaya katika sekta ya uwekezaji nchini. Kamati inaitaka Wizara ya Fedha na Mipango kukaa pamoja na ZIPA kuona chanzo cha malalamiko haya yaliyopo yanasababishwa na nini (ni utendaji kazi wa Mamlaka au ni Uendeshaji wa Afisi ya Mamlaka). Vile Kamati inaitaka ZIPA itekeleze majukumu yake kwa uwazi ili kuepusha malalamiko yaliyopo na kuweza kuwavutia wawekezaji nchini.

Mheshimiwa Spika,

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambao upo chini ya Wizara ya Fedha unalojukumu kubwa la kulipa viinua mgongo na pencheni kwa wastaafu, hata hivyo kwa kutaka kuimarisha Mfuko huu miradi mbali mbali ya maendeleo imeanza kufanywa ili kuimarisha maendeleo ya Mfuko kwa maslahi ya wanachama wake. Kamati inaitaka ZSSF kuhakikisha inasimamia vizuri miradi yake ili lengo lililokusudiwa la kuimarisha Mfuko lifikiwe kwa maslahi ya wanachama wake. Vile vile, suala la ukataji wa Bima katika miradi hii ni la msingi sana ili kuifanya miradi hii iwe salama zaidi na kutumika kwa muda mrefu, lakini bado ipo miradi ya ZSSF ambayo haijakatiwa Bima. Kamati inaitaka Wizara ya Fedha kusimamia ukataji wa Bima kwa miradi ya ZSSF katika Shirika Bima la Zanzibar.

WIZARA YA BIASHARA, VIWANDA NA MASOKO
Mheshimiwa Spika,
Wizara hii ni moja ya Wizara ambazo imekusanya sekta muhimu sana katika kuimarisha uchumi wa nchi. Ni ukweli usiopingika kuwa nchi nyingi zilizoendelea zimeendelea kutokana na kuimarika kwa sekta ya viwanda na biashara, kwani sekta huinua uchumi wan chi kwa kasi kubwa sana. Kuimarika kwa sekta hizi kunatokana na kuwepo kwa Sheria na Sera ambazo zitaweka mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji katika kuanzisha viwanda ambavyo baadae hupelekea kuimarika kwa biashara.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa azma ya Serikali katika awamu hii ni kuimarisha sekta ya viwanda nchini bado ipo haja kubwa sana ya kuziangalia Sheria na Sera zetu zinazohusu masuala ya uwekezaji wa viwanda nchini, lakini vile vile kuwe na mipango madhubuti ambayo itapelekea kuimarika kwa sekta hii, hata hivyo kuwa na mipango ni suala moja na kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo ni suala la jengine, kwa hivyo mambo haya mawili yanatakiwa yaende sambamba ili kuona kuwa mipango tunayojipangia inatekelezwa. Kamati yetu pamoja na Wajumbe wa Baraza hili tunaamini kuwa jambo litakalowezesha kufanikiwa katika kuimarisha sekta hizi ni ni kuwepo kwa mashirikiano ya dhati baina ya Serikali na wawekezaji.

Mheshimiwa Spika,
Moja ya chombo muhimi ambacho kinaweza kupelekea mazingira bora ya uwekezaji na biashara ni Baraza la Kusimamia Utoaji wa Leseni ambalo limeundwa kwa mujibu wa Sheria Namb. 13 ya 2013 ambapo jukumu kubwa la Baraza hili ni kusimamia Taasisi zote zilizopewa mamlaka ya utoaji wa leseni kwa lengo la kuweka mazingira bora ya utoaji wa leseni. Kamati yetu inampongeza Waziri wa Biashara kwa kuliunda Baraza hili hivi karibuni. Baraza hili kutokana na upya wake linakabiliwa na Changamoto kama zinavyoonekana katika ripoti ya Kamati. Hata hivyo, Sheria iliyounda Baraza hili limetoa uwezo kwa Baraza kutaka taarifa zinazohusuana na masuala ya leseni kwa Taasisi yoyote inayohusika na utoaji wa leseni, lakini bado kuna baadhi ya Taasisi ambazo zimetakiwa kuwasilisha taarifa hizo lakini bado hazijawasilisha. Chombo kipo kwa mujibu wa Sheria na kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, tunaomba sana Taasisi yoyote ambayo ilitakiwa kuwasilisha taarifa zake mbele ya Baraza basi kamati inawaomba wawasilishe taarifa hizo.

Mheshimiwa Spika,
Zao la Karafuu ni zao ambalo linaingiza mapato katika nchi na kuchangia pato la taifa, usimamizi wa zao hili ni suala moja muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar tunalitegemea zao hili katika kuimarisha uchumi wetu. Ni wazi kuwa asilimia zaidi ya 90 ya zao hili inatoka katika kisiwa cha Pemba, ipo haja kubwa sana ya kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wakulima wa zao hili ili washajihike katika kuliimarisha zao la karafuu. Tunafahamu kuwa Serikali inayodhamira ya dhati katika kuhakikisha inaimarisha zao hili, hii inatokana na kuwepo kwa Sheria maalumu ambayo inasimamia masuala ya karafuu.

Mheshimiwa Spika,
Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada mbali mbali katika kuhakikisha inazuia magendo ya karafuu jambo ambalo limekuwa ni tatizo kubwa sana hasa katika kisiwa cha Pemba, lakini bado tatizo hili limeonekana kuwepo kwa baadhi ya watu kuendelea na biashara hii ya magendo ya karafuu jambo ambalo linaweza kupelekea athari kubwa sana kwa karafuu yetu ya Zanzibar katika masoko ya nje. Kamati inaiomba sana Serikali kuzidisha juhudi katika kuhakikisha kuwa inadhibiti moja kwa moja magendo ya karafuu na kama sheria ya karafuu ina mapungufu basi tunaiomba wizara ilete marekebisho ya sheria hiyo ili tuipe meno na nguvu zaidi kwa ajili ya kuilinda na kuihifadhi karafuu yetu.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu ilifanya ziara katika nyakati tofutti kisiwani Pemba na kutembelea baadhi ya vituo vya kuuzia karafuu, ni jambo la kusikitisha sana kuona kuwa asilimia kuwa ya karafuu inazalishwa Pemba lakini hadi hii leo vituo vya kuuzia karafuu vinatumia vifaa vya zamani katika kusafisha karafuu. Kamati yetu inaitaka Serikali kupitia Wizara ya Biashara kuhakikisha kuwa inapeleka mashine za kisasa za kusafisha karafuu kisiwani Pemba ili kupungunguza gharama za karafuu kuanza kusafishwa Pemba na baadae zikifika Unguja zisafishwe tena.

Mheshimiwa Spika,

Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) ni moja ya Taasisi ambayo inasimamiwa na Wizara ya Biashara, na jukumu lake kubwa ni kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinazoingia nchini zinakuwa na ubora kwa ajili ya matumizi ya mwanaadamu. Taasisi kwa Zanzibar bado ni changa lakini hata hivyo tayari imeshaanza kutekeleza majukumu yake. Uchanga wa Taasisi hii na ufinyu wa Bajeti bado unapelekea kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Hata hivyo, Kamati imeridhishwa na jitihada za Serikali kutaka kuipatia ZBS vifaa mbali mbali vya maabara pamoja  kujenga maabara za kisasa.


Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu inaendelea kusisitiza kuwa, utendaji kazi wa taasisi hii unategemea wataalamu, maabara za kisasa na vifaa vya maabara, tunaomba sana ili kumlinda mtumiaji kuweza kutumia bidhaa yenye ubora Serikali iharakishe kuimarisha taasisi hii.

Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu ilipata kutembelea Afisi za Shirika la Ubora la Tanzania (TBS) na kuona hatua kubwa zilizofikiwa za kimaendeleo kwa Shirika hili ikiwemo pamoja na kuwepo kwa maabara zenye mashine za kisasa kwa ajili ya kupima ubora wa bidhaa mbali mbali. Vile vile imeanzisha Afisi zake katika baadhi ya Mikoa ya Tanzania ambayo inapitisha bidhaa kwa wingi. Maendeleo haya hayakufikiwa isipokuwa ni kupatiwa bajeti za kutosha pamoja na kuwa na wataalamu ambao hutumia taaluma zao kwa ajili ya maendeleo ya Shirika.

WIZARA YA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI

Mheshimiwa Spika,

Ni dhahiri kuwa Wizara hii ndio uti wa mgongo wan chi yetu, uhai wa wananchi upo katika Wizara hii. Wizara hii imejumuisha sekta nne muhimu sana katika maisha ya mwanaadamu ambazo ni sekta ya kilimo, sekta ya maliasili, sekta ya mifugo na sekta ya uvuvi. Katika kila siku za maisha yetu sekta hizi tunazifanyia kazi na wadau wakuu wa sekta hizi ni wakulima, wafugaji na wavuvi na wanaonufaika na sekta hizi ni wananchi wote kwa sababu kila siku sote tunakula kupitia bidhaa za kilimo, tunajenga na kupika kupitia maliasili, tunawekeza kupitia bidhaa za mifugo na za baharini. Mifano hii ni kuthibitisha kuwa Wizara hii ndio uhai wa wananchi na hakuna anaweza kubeza umuhimu wa kuwepo kwa Wizara hii.

Mheshimiwa Spika,

Wajumbe wa Baraza hili pamoja na wananchi wanapaswa kufahamu kuwa jukumu la kuimarisha sekta hizi sio la Serikali wala sio la Waziri bali ni jukumu letu sote, na majukumu haya yatafanikiwa pale tutakapokuwa na mashirikiano mazuri baina ya Serikali, Wajumbe wa Baraza hili na wadau wa sekta hizi pamoja na wananchi wote. Kamati imeridhishwa na jitihada za Serikali kupitia Waizri wa Kilimo katika kuhakikisha kuwa sekta hizi kuu nne zinaimarika, na ni wazi kuwa kuimarika kwa sekta hizi ni kuimarisha uchumi wa nchi na kuinua kipato cha mwananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Spika,

Suala la kuwepo kwa wataalamu wa kutosha ni jambo lisiloweza kuepukika katika nchi yoyote ambayo inajipanga kupiga hatua ya maendeleo, na moja ya Wizara ambayo inatakiwa kuwa na wataalamu wa kutosha basi ni Wizara hii kwani Wizara hii inatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi kupitia sekta zake. Hata hivyo, Kamati yetu imebaini kuwepo kwa tatizo la wataalamu wa kutosha katika Wizara hii jambo linapelekea malalamiko makubwa kwa wadau wa sekta hizi. Pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Wizara katika kuhakikisha kuwa inasomesha watumishi wake lakini pia bado kuna tatizo la kuweka vipao mbele vya kuwasomesha watumishi ili kupunguza uhaba wa wataalamu. Katika suala hili, Kamati yetu inaitaka Wizara sasa ianze kuweka mpango maalumu wa kuwa na vipao mbele kulingana na mahitaji ya wataalamu katika Wizara wakati wanapotoa nafasi za kuwasomesha watumishi wao. Lakini vile vile suala hili liende sambamba na kuweka masharti maalumu kwa mtumishi yoyote atakayesomeshwa na Wizara kuendelea kubaki katika Wizara kwani imeonekana kuwa lipo tatizo kwa baadhi ya wataalamu wakishakusomeshwa na Wizara kuacha kazi au kuchukuwa likizo bila ya malipo.

Mheshimiwa Spika,

Naomba kwa ufupi sana kwa umuhimu wake niizungumzie Sekta ya Uvuvi, sekta hii  ni moja ya sekta ambayo Serikali inaitegemea kupata mapato yatokanayo na sekta hii. Lakini bado mapato katika sekta ya uvuvi Zanzibar kulingana na rasilimali ya bahari tuliyonayo hayaridhishi na hayaendani na ukubwa wa rasilimali yetu. Kwa mfano; katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Makadirio ya bajeti katika sekta ya uvuvi ni Tshs. 1,000,949,000/- katika pato la Taifa.

Kulingana na ukubwa wa rasilimali ya bahari tuliyonayo mchango wa Sekta ya uvuvi katika pato laTaifa bado ni mdogo sana. Hatahivyo, Kamati yetu inaipongeza Serikali kupitia Wizara hii kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kuimarisha sekta ya uvuvi nchini kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi na pato la Taifa.

Tunaomba sana jitihada za Serikali zizidishwe katika kuhakikisha kuwa rasilimali tuliyonayo ya bahari inatumika ipasavyo kwa lengo la kuimarisha uchumi wan chi yetu. Tunaamini kuwa Zanzibar inaweza kujiendesha kwa kuitumia bahari tu kwani ipo mifano ya nchi nyingi za visiwa zilizoendelea kwa kutumia bahati tu. Kwa mfano, baadhi ya wajumbe wa Kamati yangu walibahatika kutembea katika visiwa vya Maldeves ambavyo ni visiwa vilivyoendelea sana na uchumi wao wanategemea bahari na utalii tu. Kwakuwa na sisi rasilimali hii tunayo hatuna sababu na sisi kwanini tusiwe zaidi ya wao. Hivyo kamati inaishauri Serikali Kuu kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa kuhusiana na safari ya Maldeves hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Spika,

Naomba nikumbushie kwa Serikali kufanya uharaka wa kuieleta Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri mbele ya Baraza hili ya Muungano ili kukidhi masharti ya kifungu cha 132 cha Katiba ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Suala la kutumia baadhi ya maliasili katika nchi limeruhusiwa kufuatana na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni au Miongozo inayotolewa na Wizara. Hivi karibinu Wizara ya Kilimo imekuwa ikitoa matangazo mbali mbali juu matumizi ya maliasili ya mchanga jambo ambalo limepelekea kuelewaka vibaya kwa baadhi ya wananchi na kuzidi kujengeka khofu juu ya kuendelea kutumia maliasili hiyo. Kutokana na uelewa huo mdogo wa wananchi, Kamati yetu inaitaka Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuwasilisha taarifa maalumu kuhusu “Hali halisi ya uchimbaji wa Mchanga Zanzibar” ili Wajumbe wa Baraza hili na wananchi wote wapate kuelewa faida na athari zilizopo na muwelekeo wa Serikali kwa baadae.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,

Naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wajumbe wote wote wa Baraza hili kwa utulivu wao katika kipindi chote ambacho nilikuwa nikiwasilisha Muhtasari huu wa Ripoti yetu ya Kamati. Nawaomba sana waijadili kwa kina ripoti hii na hatimae kuikubali.

Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.






……………

Mhe:Yussuf Hassan Iddi
Mwenyekiti,
Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo,
Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.