Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Afungua Mahakama ya Watoto Mahonda Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                            7.2.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa licha ya kuwepo taasisi zinazosimamia haki na sheria lakini bado tatizo la udhalilishaji wa wanawake na watoto limeendelea kushamiri katika jamii.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya ufunguzi wa Mahakama ya Watoto huko Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni miongoni mwa muendelezo wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Sheria, Zanzibar kwa mwaka huu.

Katika hotuba yake kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa vitendo vya aina hiyo ni kinyume na mafundisho ya dini, malezi pamoja na Katiba na Sheria zilizopo ambazo baadhi yake zimepata tunzo kwa ubora wake ikiwemo Sheria ya Mtoto Namba 6 ya mwaka 2011 ambayo imepata tunzo huko Geneva kutokana na ubora wake duniani.

Hivyo, Dk. Shein alizitaka taasisi zinazosimamia haki na Sheria kuitumikia Serikali yao kwa uwazi na ukweli kwa lengo la kufikia malengo yaliowekwa pamoja na kuitaka jamii kutoa mashirikiano katika kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Dk. Shein alisema kuwa Jamii ina dhamana kubwa ya kulea vyema watoto kwani ni dhahiri kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na maslahi yao yanazingatiwa kuanzia kwenye ngazi za familia na siyo kwenye vyombo vya sheria pekee yake.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa taarifa za Kitengo cha Urajisi cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, zinathibitisha kuongezeka kwa kesi za aina mbali mbali katika jamii zinazovunja haki za watoto ambazo zimeripotiwa katika mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka 2015.

Alieleza kuwa katika mwaka 2016, idadi ya kesi za watoto waliopewa ujauzito zilizoripotiwa ni 26, ikilinganishwa na kesi 19 zilizoripotiwa mwaka 2015 ambapo wamo watoto wa darasa la sita hadi Kidato cha Nne (Form 4).

Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa chombo kinachoonesha vimelea vya urithi vya wazee (DNA) katu sio sababu ya kumaliza tatizo hilo katika jamii kwani chombo hicho kinasimamiwa na mwananadamu ambapo jambo kubwa linalotakiwa ni kubadilika na kutofanya kazi kwa mazoea.

Dk. Shein alisema kuwa fedha nyingi zimetumika katika ujenzi wa jengo hilo ikiwa ni kwa lengo la kutekeleza haki za watoto sambamba na kupiga vita udhalilishaji wa watoto kwa kuuondoa kabisa kadhia hiyo huku akieleza kuwa taasisi husika zitawekwa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo kama alivyofanya kwenye changamoto ya takwimu hivi karibuni.

Alisema kuwa juhudi mbali mbali zimechukuliwa na Serikali katika kuhakikisha vitendo hivyo vinaondoshwa kabisa ikiwa ni pamoja kuanzisha Kampeni ya miaka miwili ya Kupiga Vita Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto Zanzibar iliyozinduliwa Disemba mwaka 2014  ambapo Serikali kupitia Wizara husika imeamua kufanya tathmini.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwenda kutoa ushahidi pale unapohitajika ili kuepuka kesi za udhalilishaji kuishia majumbani hatua ambayo pia, itaisaidia Serikali kufikia malengo yake iliyojiwekea.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Majaji, Mahakimu, Makadhi na Watumishi wote wa Mahkama kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kutoa haki kwa wananchi.

Mapema, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema kuwa atahakikisha Wizara yake inaendela kutoa mashirikiano na taasisi nyengine ili kuhakikisha sheria na haki nyengine zote za mtoto zinapatikana.

Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar  Omar Othman Makungu alieleza kuwa tayari taratibu zote za kuanzishwa kwa Mahkama hiyo zimekamilika, zikiwemo za kutoa Tangazo la Kisheria katika gazeti rasmi la Serikali ikiwa ni pamoja na kumteua Hakimu wa Mkoa wa kuendesha Mahkama hiyo Nayla Abdulbasit.

Jaji Makungu alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajali kuthamini sana utu na maendeleo ya watoto jambo ambalo linathibitishwa na uwepo wa elimu bila ya malipo, matibabu bure na kuweka sheria ya watoto Nam. 6 ya mwaka 2011 ambayo inataka kuundwa kwa Mahkama maalum za watoto ambayo hiyo ni moja wapo.

Alisisitiza kuwa Mahkama kwa upande wake inashirikiana na Serikali katika kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto na kuhakikisha kesi za aina hiyo zinapewa kipaumbele na hazichukui muda mrefu katika kumalizika kwake ambapo haitozidi miezi sita.

Akitoa taarifa ya mradi wa jengo hilo la Mahkama ya Watoto,  Mrajis wa Mahakama Kuu, George Joseph Kazi alisema kuwa ujenzi wa Mahkama hiyo umedhaminiwa na Shirika la Maendeleo ya Watoto Ulimwenguni (UNICEF) ambalo lengo lao kuu ni kutoa msaada wa kitaalamu na kifedha kwa ajili ya maendeleo ya haki ya mtoto kulingana na sheria ya Mtoto No. 6 ya mwaka 2011.

Alisema kuwa ujenzi huo ulianza rasmi tarehe 04.10.2015 na kukamilika mwezi Disemba mwaka 2016 mradi ambao ni wa jengo moja ambalo linajumuisha Ofisi ya Hakimu wa Mahkama ya Watoto, Ofisi ya Waendesha Mashtaka, Ofisi ya Makarani, Ofisi ya Ofisa wa Ustawi wa jamii, chumba cha Computer, mapokezi na nyenginezo.

Kwa maelezo ya Mrajis huyo wa Mahakama Kuu, ujenzi wa Mahkama hiyo umegharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 106,996,220.

Mwakilishi wa UNICEF katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Maniza Zaman katika hotuba yake alisisitiza kuwa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa litaendelea kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha watoto wanaendelea kupata haki zao za msingi.  

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika Hafla hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame,  Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Majaji, Mahakimu na viongozi wengine wa Serikali na vyama vya siasa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.