Habari za Punde

WAKULIMA wa mboga mboga wakabidhiwa vifaa vya umwagiliaji wa matone

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAKULIMA wa mboga mboga na migomba kisiwani Pemba, wametakiwa kuvitumia vifaa vya umwagiliaji wa matone walivyokabidhiwa na serikali, kwa lengo la kuongeza uzalishaji ili watunishe pato lao.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi Zanzibar kwa niaba yake, wakati Mkuu wa Mradi wa kuimarisha Kilimo na Ufugaji ASSP, dk Talib Saleh Suleiman akizungumza na wanavikundi hao mjini Chakechake.

Mkuu huyo wa program ya ASSP, alisema kwa wanavikundi hao vya mboga mboga na mtu mmoja mmoja, lazima kuwe na tofauti kabla na baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo.

Alisema, vifaa hivyo vya umwagiliaji kwa njia ya matone, kama wakiyatumia vyema, anaamini uzalishaji wao utapanda sambamba na pato lao.

Dk Talib alisema, walipokea maombi ya wananchi kadhaa wanaohitaji mipira na matangi ya kuhifadhia maji kwa ajili ya kuimarisha kilimo chao, hivyo kwa hao waliobahatika, lazima wazingatie kuwa kilimo bora.

“Leo tunawakabidhi matangi na mipira maalumu kwa ajili ya kuendeleza kilimo chenu cha mboga mboga, sasa sisi tunachosubiri ni kuona mnaongeza pato lenu, ili kupunguza umaskini’’,alisema.

Aidha dk Talib, alieleza kuwa baada muda mfupi atatuma maofisa wao, kuwakagua na ikitokeza yupo mkulima au kikundi wanasita sita kwenye kazi zao, watapaswa kuyarejesha.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo wa ASSP-ASDP-L Pemba Asha Omar Faki, alisema kilimo cha mboga mboga na migomba, kinaweza kuwakombo wakulima pindi wakipatiwa vifaa kama hivyo.

“Sisi kama watu wa kuimarisha kilimo na ufugaji, tunaamini sana kuwa, wakulima wakikabidhiwa vitenda kazi kama mipira ya maji na matangi ya kuhifadhia maji, wanaweza kuukimbia umaskini’’,alifafanua.

Hata hivyo alisema kutokana na mabadiliko ya tabianchi yalivyojitokeza na kuwaathiri wakulima hasa wanaotegemea mvua, ndio maana serikali kupitia wizara yake ya kilimo ikakabidhi vifaa hivyo.

Wakulima mmoja mmoja waliokabidhiwa vifaa hivyo, kwa wilaya ya Wete ni Msanifu Ali Faki alipewa mipira ya maji ya matone seti mbili na tanki la maji lenye ujazo wa lita 1000.

Wengine Salim Kombo Hamad seti mbili za mipira, Kombo Hamad Yussuf seti mbili za mipira, Mohamed Rashid Ali tanki la lita 1000 na mipira seti mbili, wakati kwa wilaya ya Mkoani ni Salim Hamad Mohamed (seti mbili mipira), Said Omar Mohamed tanki la lita 5000, Issa Mohamed Ussi tanki la lita 1000, mipira seti mbili.

Kwa wilaya ya Micheweni ni ushirika wa ‘tujali wakati’ seti mbili za mipira, ushirika wa ‘vikunguni’ mipira seti mbili, wakati kwa wilaya ya Chakechake ni Rashid Salum mipira seti mbili, ushirika wa ‘mwisho wa ubaya’ tanki la lita 5,000 na mipira yake, mkulima Khamis Juma Kheir takini la lita 1,000 na mipira.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Tibina Issa Maligha kutoka Kiwani, alisema watahakikisha vifaa walivyokabidhiwa vinaongeza pato lao.

Hata hivyo walisema, bado wapo wenzao kadhaa wanahitaji vifaa kama hivyo, kutokana na mashamba yao kukauka na kuhatarisha vilimo vyao.

Wizara ya Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi imeshatumia zaidi ya shilingi milioni 130 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya mipira ya maji ya umwagiliaji kwa njia ya matone, matangi (simtank) kwa ajili ya wakulima mmoja mmoja na vikundi vilivyowekeza kwenye kilimo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.