Habari za Punde

Waliokatisha masomo yao waombwa kujiunga na kituo che elimu mbadala


Na Salmin Juma , Pemba

WAZAZI na walezi Kisiwani Pemba, wametakiwa kuwashajiisha watoto wao waliokatisha masomo na waliokwenye ndoa ambao hawajavuuka umri wa miaka 22, kuijunga na kituo cha elimu mbadala, ili wapate elimu ya kujikomboa.

Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa elimu mbadala na watu wazima Pemba, Hija Hamad Issa, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, baada ya kufunguliwa jengo la chuo kilichopo Wingwi Pemba.

Alisema kama kuna vijana wa kike ambao wameshaolewa, kuzaa kabla ya ndoa au wengine waliokatisha masomo au hawakusoma kabisa na wanafikia umri wa miaka 15 na hawazidi 22, nafasi ya kuijunga na Kituo hicho bado ipo.

Mratibu huyo alisema, elimu inatolewa kwenye Kituo hicho ikiwemo ya ufundi, ushairi nasaha na kazi za amali, zinaweza kuwakomboa vijana ambao wanajiona wameshapoteza mwelekeo.

Mratibu huyo alifafanua kuwa, ndani ya kituo hicho kipya ambacho kwa sasa kina wanafunzi 68 wakiwemo wawili ambao wako kwenye ndoa, wanaendelea vyema na wanatarajia miezi sita ijayo kuongeza idadi ya kozi.

“Kituo cha elimu mbadala na watu wazima, kipo sasa hakuna sababu kwa jamii kukosa elimu, maana hapa kama una umri unaotakiwa hata kama umeshaolewa au kuoa unaruhusiwa’’,alifafanua.

Kwa upande wake Msaidizi Mwalimu Mkuu wa kituo hicho, Yussuf Mohamed Adballa, amesema changamoto kubwa iliopo Kituoni hapo ni uhaba wa waalimu, 25 ambapo kwa sasa wapo watano.

“Lengo letu hasa kila fani kama ya umeme, ushauri nasaha na ushoni iwe na waalimu wawili, sasa tunao wawili tu, hivyo ni vyema taasisi husika ikatuongezea ili tutimize ndoto za vijana na wazee wetu’’,alifafanua.

Hata hivyo alisema elimu ya ushairi nasaha na ufundi inayotolewa kwenye Kituo hicho inaweza kuwa mwarubaini kwa vijana mara wanapomaliza.

Katika hatua nyengine Msaidizi huyo Mwalimu Mkuu wa Kituo hicho, alisema wanahitajia nyumba mbili za waalimu pamoja na uzio kwa ajili ya kukilinda kituo hicho.

Baadhi ya wananchi wanaoishi Wingwi, wameipongeza wizara ya Elimu kwa mpango wake huo wa kujenga kituo hicho, ambacho kimewakomboa watoto wao.

“Kituo kimetusaidia maana wapo watoto wetu ambao walishakata tamaa kwenye masomo baada ya kukatisha masomo, na sasa wamerejea tena kituoni hapo’’,alisema Mwashamba Kassim Khamis.

Nae Mwalimu Kombo Hassan, aliiomba wizara wizara husika kujaza vifaa vya kufanyia mafunzo kwa wanafunzi wanaomaliza masomo yao, ili wakimaliza waweze kujitegemea.

Kituo hicho cha ghorofa moja cha elimu mbadala na watu wazima, kinapokea wanafunzi waliokatisha masomo au kutosoma kabisa wakiwa na umri usiopungua miaka 15 na hawazidi umri wa miaka 22.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.